1: Dr. T. V. N. Persaud
Ni Profesa wa Anatomia (sayansi inayohusu mwili na viungo vyake jinsi vilivyo, Profesa wa Matibabu ya watoto na magonjwa yao (Pediatrics) na Afya ya Mtoto, na Profesa wa Ukunga, Jinakolojia (Elimuuzazi), na Sayansi ya mambo ya Uzazi katika Chuo Kikuu cha Minatoba, Winnipeg, Manitoba, Kanada. Hapo, alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Anatomia kwa miaka 16. Yeye ni mashuhuri katika uwanja wake. Yeye ni mwandishi au mhariri wa vitabu 22 na amechapisha vitabu zaidi ya tafiti 180 za kisayansi. Mnamo mwaka 1991, alipokea tuzo ya kipekee kabisa iliyotolewa katika uwanja wa Anatomy huko Kanada, J.C.B. Grant Award kutoka katika Chama cha wana-Anatomia wa Kanada. Alipoulizwa juu ya miujiza ya kisayansi katika Qur'an ambayo aliifanyia tafiti, alisema yafuatayo:“Namna nilivyoelezwa ni kwamba, Muhammad alikuwa mtu wa kawaida. Hakuweza kusoma, hakujua (namna ya) kuandika. Kwa kweli, alikuwa asiyejua kusoma. Sisi tunazungumzia kadiri ya miaka elfu moja na mia mbili [kwa kweli kadiri ya miaka elfu moja na mia nne] iliyopita. Unamkuta mtu asiyejua kusoma na kuandika akitoa matamko na kauli zenye maarifa mengi na cha ajabu ziko sahihi kuhusiana na sayansi. Mimi binafsi yangu, sioni ni vipi hii inawezaje kuwa ni bahati nasibu tu. Kuna mambo mengi sana ya uhakika na, kama Dr. Moore, sioni tatizo katika fikra zangu kuwa hii msukumo au uhusiano utokao kwa Mwenyezi Mungu ndio uliomwongoza yeye atoe kauli hizi.”
Profesa Persaud amejumuisha baadhi ya Aayah za Qur'an na Hadiyth za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika baadhi ya vitabu vyake. Pia aliziwasilisha Aayah na Hadiyth za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mikutano kadhaa wa kadhaa.
2: Dr. Joe Leigh Simpson
Ni Mwenyekiti wa Idara ya Ukunga na Jinakolojia (Elimuuzazi), Profesa wa Ukunga na Elimuuzazi, na Profesa wa Vinasaba vya Kimolekuli na Kibinaadamu katika Chuo cha Utabibu cha Baylor, Houston, Texas, Marekani. Hapo kabla alikuwa Profesa wa Ob-Gyn na Mwenyekiti wa Idara ya Ob-Gyn katika Chuo Kikuu cha Tennessee, Memphis, Tennessee, Marekani. Pia alikuwa Rais wa Chama cha Utungishaji Mimba (Fertility Society) cha Marekani. Amepokea tuzo nyingi, ikiwa ni pamoja na Tuzo ya Utambuzi wa Kijamii ya Chama cha ma-Profesa wa Ukunga na Elimuuzazi, mnamo mwaka 1992. Profesa Simpson alizisoma Hadiyth mbili za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):(Kwa kila mmoja wenu, vijenzi vya kuumbwa kwenu hukusanywa pamoja katika tumbo la uzazi la mama kwa muda wa siku arubaini...) [1].
(Ikiwa siku arubaini na mbili zitapita katika kiinitete, Mwenyezi Mungu Humtuma Malaika ambaye hukitia umbo na kuumba kusikia kwake, kuona, ngozi, minofu na mifupa...) [2]
Alizichunguza Hadiyth mbili hizi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa undani, na kutia maanani kuwa siku arubaini na mbili za kwanza huwa na hatua dhahiri kuzitofautisha za mwanzo wa kiinitete. Yeye binafsi alishawishika na usahihi wa kauli ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). kisha, katika mkutano mmojawapo alitoa maoni yafuatayo.
“Kwa hivyo, Hadith hizo mbili zilizotajwa zinatupatia ratiba makhususi kuhusu maendeleo makuu ya kiinitete kabla ya siku arubaini. Kwa mara nyingine, nukta muhimu imeshawekwa, nadhani kwa kurudiwarudiwa na wasemaji wengine asubuhi hii, Hadiyth hizi haziwezekani kuwa zimepatikana kwa kufuata msingi wa ujuzi wa kisayansi uliokuwepo katika zama za kuandikwa kwake... Kinachofuatia, nadhani, kwamba si tu kuwa hakuna ukinzani baina ya jenetiki na Dini , lakini, kwa kweli, Dini huiongoza sayansi kwa kuongeza ufunuo kwa baadhi ya njia za kisayansi za kimapokeo, kwamba kunakuwepo kauli katika Qur'an zilizoonesha baada ya karne nyingi kuwa thabiti, ambazo zinasaidia kuwa elimu iliyomo katika Qur'an imepatikana kutoka kwa Mwenyezi Mungu."
3: Dr E. Marshal Johnson
Ni Profesa wa Heshima (baada ya kustaafu) wa fani ya Anatomia na Baiolojia ya Makuzi katika Chuo Kikuu cha Thomas Jafferson, Philadelphia, Pennslyvania, Marekani. Hapo, kwa muda wa miaka 22 alikuwa Profesa wa Anatomia, Mwenyekiti wa Idara ya Anatomia na Mkurugenzi wa Taasisi ya Daniel Baugh. Kadhalika, alikuwa Rais wa Jumuia ya Teratolojia. Ameandika machapisho zaidi ya 200. Mnamo mwaka 1981, wakati wa Mkutano wa Saba wa Masuala ya Tiba jijini Dammaam, Saudi Arabia, Profesa Johnson aliyasema yafuatayo katika kuwasilisha taarifa yake:“Kwa ufupi: Qur'an haielezei maendeleo ya umbo la nje tu, bali inafafanua pia hatua za ndani, hatua za ndani ya kiinitete, wa kuumbwa kwake na ukuaji, ikifafanua matukio makubwa yanayotambuliwa na sayansi ya zama hizi.”
Kadhalika alisema: “Kama mwanasayansi, ninaweza kuvishughulikia vitu ambavyo mimi mwenyewe naweza kuviona. Naweza kuelewa elimu ya kiinitete na Baiolojia ya makuzi. Naweza kufahamu maneno ninayotafsiriwa kutoka katika Qur'an. Kama nilivyotoa mfano hapo kabla, ningelikuwa mwenye fursa ya kujibadilishia nafasi ya kuweza kuingia katika kipindi hicho, ilhali nikiwa haya ninayoyajua leo na kuyaeleza mambo, nisingeliweza kuvielezea vitu vilivyoelezwa. Kwa kweli sioni ushahidi wa kukataa fikra kwamba, mtu huyu, Muhammad, alikuwa akitoa maelezo kutoka mahali fulani. Hivyo, sioni kitu hapa kikikinzana na fikra kwamba jambo linalohusiana na Mungu lilihusika katika alichoweza kukiandika.”[3]
4: Dr. William W. Hay
Ni mwanasayansi mashuhuri juu ya masuala ya baharini. Yeye ni Profesa wa Sayansi ya Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Colorado, Boulder, Colorado, Marekani. Hapo kabla, alikuwa Mkuu wa Shule ya Rosentiel inayohusika na Masuala ya Baharini (Marine) na Sayansi ya Angahewa katika Chuo Kikuu cha Miami, Florida, Marekani. Baada ya majadiliano na Profesa Hay kuhusu Qur'an kwamba iliyataja masuala mambo yaliyogundulika hivi karibuni juu ya masuala ya bahari, alisema:“Ninakuta kwamba ni jambo la kuvuta fikra kwamba khabari ya namna hii imo katika maandiko ya kale ya Qur'an Tukufu, nami sina njia ya kujua kwamba huenda yamekuja kutoka wapi, lakini inavuta fikra mno kuwa yangalipo na kwamba, kazi hii inaendelea ili igundue, maana ya baadhi ya vifungu vya maneno.” Alipoulizwa kuhusu chanzo cha Qur'an, alijibu: “Naam, nadhani lazima itakuwa ni Mungu".
5: Dr Gerald C. Goeringer
Ni Mkurugenzi wa Kozi na Profesa Mshiriki wa Elimumadawa ya Kiinitete katika Idara ya Baiolojia ya Chembehai, Chuo cha Tiba, Chuo Kikuu cha Georgetown, Washington, DC, Marekani. Wakati wa mkutano wa nane wa Saudia katika jiji la Riyaadh, Saudi Arabia, Profesa Gorienga alisema yafuatayo katika uwasilishaji wake wa taarifa ya utafiti wake:“Ndani ya Aayah (Aya za Qur'an) chache tu mna maelezo mapana juu ya makuzi ya mwanaadamu kutokea wakati wa kuchanganyika kwa seli pevu za uzazi (gameti) kwa njia ya organogenesis. Hakuna utofautishaji na maelezo kamili ya makuzi ya mwanaadamu mfano wa haya, kama vile uainishaji, maneno na maelezo yaliyokuwepo kabla hapo nyuma. Katika matukio mengi, kama si yote, maelezo haya yanarudi nyuma kwa karne nyingi, nukuu ya hatua kadhaa za makuzi ya kiinitete na fetal, zilizonukuliwa katika maandiko ya sayansi asilia.”
6: Dr. Yoshihide Kozai
Ni Profesa wa Heshima katika Chuo Kikuu cha Tokyo, Hongo, Tokyo, Japan, na alikuwa Mkurugenzi wa Mahali pa kuangalia (jua, mwezi na nyota) Unajimu Kitaifa, Mitaka, Tokyo, Japan. Alisema:“Nimevutiwa sana na kwa kukuta ukweli wa taarifa za kinajimu kutoka ndani ya Qur'an, na kwetu sisi, wanajimu wa zama hizi tulikuwa tukichunguza vipande vidogo sana vya ulimwengu. Nguvu zetu tulizielekeza katika kuelewa sehemu ndogo sana. Kwa sababu, kwa kutumia darubini, tunaweza kuona sehemu chache sana ya anga pasi na kufikiri (juu ya) ulimwengu mzima. Hivyo, kwa kuisoma Qur'an na kwa kuyajibu maswali, nadhani naweza kuipata njia ya baadaye kwa ajili ya kuuchunguza ulimwengu.”
7: Profesa Tejatat Tejasen
Ni Mwenyekiti wa Idara ya Anatomia katika Chuo Kikuu cha Chiang Mai, Chiang Mai, Thailand. Kabla ya hapo, alikuwa Mkuu wa Kitivo cha Tiba katika chuo hicho hicho. Wakati wa mkutano wa nane wa Saudi wa masuala ya tiba jijini Riyaadh, Saudi Arabia, Profesa Tejasen alisimama na akasema:“Katika miaka mitatu iliyopita, nilijikuta nikivutiwa na Qur'an. Kutokana na uchunguzi wangu na kutokana na nilichojifunza katika mkutano huu, naamini kuwa kila kilichoandikwa ndani ya Qur'an mnamo miaka elfu moja na mia nne iliyopita, ni lazima kuwa ni kweli, ambao unaweza kuthibitishwa kwa njia za kisayansi. Kwa kuwa Mtume Muhammad hakuweza kusoma wala kuandika, Muhammad ni lazima kuwa ni Mtume aliyeupokea na kuueneza ukweli huu, ambao ulishushwa kwake kama uongofu kutoka kwa anayestahiki kuwa ni muumbaji. Lazima muumbaji huyu awe ni Mwenyezi Mungu. Hivyo, nadhani huu ndio muda muwafaka wa kusema La ilaaha illa Allaah, hapana mola wa haki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammadur Rasulullah, Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Mwisho, ni lazima nipongeze kwa mipango mizuri sana na ya mafanikio makubwa ya mkutano huu... Si kwamba nimepata kutoka katika nukta ya mtazamo wa kisayansi na wa ki-Dini lakini pia fursa kubwa ya kukutana na wanasayansi wengi mashuhuri na kupata marafiki wengi miongoni mwa washiriki. Kitu cha thamani kubwa kuliko vyote nilivyopata kwa kuja kwangu mahala hapa ni La ilaaha illa Allaah, Muhammadur Rasulullah, na mimi kuwa Muislamu.”
Baada ya mifano yote hii, tumeona juu ya miujiza ya kisayansi katika Qur'an Tukufu na maoni yote haya ya wanasayansi juu ya hili, hebu tujiulize maswali haya:
Inaweza kuwa ni suala la utukizi kuwa maelezo haya ya kisayansi yaliyogundulika hivi karibuni kutoka katika nyanja tofauti tofauti yalikuwa tayari yalishaelezwa katika Qur'an, ambayo iliteremshwa karne kumi na nne zilizopita?
Je, inawezekana kuwa Qur'an hii ilitungwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au mtu mwingine?
Jibu pekee linalowezekana kupatikana ni kuwa Qur'an hii ni lazima kuwa ni maneno khalisi ya Mwenyezi Mungu, na Ndiye Aliyeiteremsha.
(Kwa maelezo zaidi, makala, vitabu au video juu ya miujiza ya kisayansi ndani ya Qur'an zilizounganishwa na kompyuta kuu (online), tafadhali tembelea www.islam-guide.com/science au wasiliana na mojawapo ya mashirika/vyama yaliyoorodheshwa katika ukurasa...
_________________
[1] Imesimuliwa katika Swahiyh Muslim, Na. 2643, na Swahiyh Al-Bukhaariy, Na 3208. Kumb: Kilicho baina ya braketi hizi maalumu (...) ndani ya kitabu hiki ni tafsiri ya kile alichokisema Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Pia tambua kwamba alama Na. inayotumika katika rejeo, inaashiria namba ya Hadiyth. Hadiyth ni masimulizi ya kuaminika yaliyopokewa kutoka kwa Maswahaba wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya alichokisema, kukifanya au kukiruhusu.
[2] Imesimuliwa katika Swahiyh Muslim, Na. 2645
[3] Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ummiy. Hakuweza kusoma wala kuandika, lakini aliwasomea Maswahaba wake Qur-aan na aliwaagiza baadhi yao waiandike
No comments:
Post a Comment