Thursday, 7 June 2012

Qur'an Na Maisha Ya Nyuki


 
Na Mola wako mlezi amemfunulia Nyuki. Jitengezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayoyajenga watu. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizofanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali, ndani yake kina matibabu kwa wanadamu. Akika katika haya ipo ishara kwa watu wano fikiri.
Qur’an 16:68-69

Nyuki ni wadudu ambao mara kwa mara huwa tunakutana nao katika maeneo mengi tunamoishi.Yawezekana tunakutana nao mashambani, porini, au mijini. Kwenye sura hii ya An Nah’l, katika aya ya 68-69 kuna mambo kadhaa ya kuzingatia, lakinia hapa tunayaangalia mambo machache tu, mambo ambayo watu wengi wamekuwa  hawana habari nayo na wala hawayazingatii. Japokuwa ni kwa kipindi kirefu sana, zao linalotokana na wadudu hawa, limekuwa likitumika katika chakula na mambo mbali mbali ya kimatibabu. Mfano; matibabu ya kimwili, kuongeza nguvu na nishati na kadhalika.

Basi na tuangalie kwanza neno lenyewe Annah’l, lina maana gani. Neno ili Annah’l maana yake ni Nyuki, lakini ni Nyuki wa jinsia gani? Annah’l ni jina lenye jinsia ya kike, kwa maana hiyo hicho kiumbe kilicho tajwa hapo basi bila shaka kitakuwa ni chenye jinsia ya kike. Kwa maana hiyo basi nyuki huyu tunaye muona katika harakati zake mbali mbali za kutafuta rizki ni Nyuki jike na si Nyuki dume, kama mawazo ya watu wengi wakiwemo wasomi mbalimbali wa zama hizo na zama zetu hizi. Mwaka 1600 mwandishi mmoja maarufu sana wa vitabu vya fasihi ya kiingereza (literature) aitwae William Shakespeare amemwelezea Nyuki katika kitabu chake kinachoitwa; King Henry ‘V’. Alisema hivi nanukuu, “...the King Bee goes out with his soldiers...” mwisho wa kunukuu. Yaani “...mfalme nyuki hutoka na askari zake...” neno Mfalme (King) ni neno linalotokana na watawala wa kiume, na mara nyingi utawala wa kifalme ni utawala wa kurithishana. Na kama mtawala atakuwa ni mwanamke basi hataitwa Mfalme bali ataitwa Malkia (Queen). Na pia kwa zama za kina William Shakespeare askari wote walikuwa ni wanaume, na ilikuwa si aghlabu kukuta askari wa kike. Hasa kwa miaka hiyo ya 1600 AD. Tofauti na sasa tuna askari wengi tu wa kike. Basi hebu na tuangalie wataalam wa wadudu (Entomologist) hususani, wataalam wa Nyuki wanatueleza nini kuhusu mdudu huyu Nyuki.

Wataalam wanatufahamisha kuwa Nyuki tunaowaona katika mazingira yetu ya kila siku, ni Nyuki wanawake wakiongozwa na Malkia wao ambaye pia ni Nyuki jike. Malkia ambaye ana uwezo wa kutaga mayai mpaka kufikia 3000 kwa siku, hesabu hii ni wastani wa mayai mawili kwa dakika yaani malkia wa nyuki hutaga mayai mchana na usiku. Na huyu wala si Mfalme kama mawazo ya watu wengi wanavyofikilia.

Harakati za Nyuki ni nyingi sana kwa mfano Nyuki mmoja ili atutolee kilo moja ya Asali atahitaji kufanya safari ya nenda rudi nenda rudi maili 300,000 mpaka maili 500,000. Na huwahudumia watoto wao kwa wastani wa siku sita (6). Na watoto wa Nyuki utembelewa kwa wastani wa mara 7850 kwa siku hizo sita.
 

A: Maisha ya Nyuki katika makazi yao:

maisha ya Nyuki katika mzinga wao au makazi yao na jinsi wanavyoitunza Asali isiharibike ni ya ajabu mno, maisha yao ni yenye ushirikiano mkubwa sana na wa kiwango cha juu mno. Unyevunyevu (Humidity) katika makazi ya Nyuki, ndio hukinga asali isiharibike na isipoteze ubora wake, unyevunyevu huwa katika kiwango maalum. Na kama ikitokea kuwa unyevu unakuwa mkubwa sana ama unakuwa mdogo kuliko kawaida, basi hali hii inaweza ikasababisha, asali kuharibika na kupoteza ubora wake sambamba na kupotea kwa lishe iliyomo kwenye asali. Halijoto (temperature) katika makazi ya nyuki, inatakiwa kuwa 320c. Kwa miezi takribani kumi katika mwaka. Na ili kuweza kuweka halijoto, unyevu na hewa ya kutosha katika viwango vinavyotakiwa, kuna kuwa na kundi maalum la nyuki, ambao wao wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanadumisha hali hiyo kwa vipindi vyote vya maisha yao. Nyuki hawa moja ya kazi zao ni kuhakikisha kuwa, wanakuwa karibu na milango ya kuingilia katika makazi yao, ujikusanya na kupiga mabawa yao kwa ajili ya kingiza upepo ndani ya makazi yao, na baadhi yao huitawanya hiyo hewa ndani ya makazi na kulazimishwa upepo huo kutokea upande wa pili wa makazi yao. Kwa jinsi hiyo nyuki wanaweza kudumisha hali ya joto kwa kiwango wanachokitaka wao, na kuondoa uharibifu wa hali ya hewa (Pollution) ndani ya makazi yao.

Nyuki hawaishii kuilinda asali tu kwa kuingiza hewa na kuitoa nje kutoka ndani ya makazi yao, au kulinda na kuhakikisha kuwa unyevu na hali joto vinakuwepo katika viwango vinavyotakiwa, bali wanawajibika kuitunza asali katika kiwango kitakacholeta lishe bora kwa mlaji. Nyuki wanawajibika kuitunza asali kutokana na wadudu wa aina mbalimbali, watakao sababisha bakteria kuingia kwenye asali na kuharibu ubora wake. Siku zote wapo nyuki wanaofanya kazi hiyo ya kuhakikisha kuwa hakuna mdudu yoyote yule anaeingia katiaka nyumba yao, na kuiharibu asali yao. Na kama ikitokea kuwa kuna mdudu au kitu chochote kile, kimeingia kwenye asali, basi nyuki watashirikiana kukishambulia kitu hicho ili kitoke, na kama kitu chenyewe ni kidogo basi watakitoa nje. Kama ikitokea kuwa kitu hicho au mdudu huyo ni mkubwa kiasi ya kwamba wao kwa uwezo wao wanashindwa kukitoa au kumtoa nje ya makazi yao, basi watatumia njia nyingine ya kuilinda asali yao na makazi yao kwa ujumla. Njia watakayo tumia nyuki hao ni kutengeneza ute (Bee Resin) na kuuchanganya na utomvu unaotokana na miti au baadhi ya mimea kama vile, miti ya misonobari (Pine tree), mpopla (Poplar tree) au mti unaoitwa Acacia tree. Kutokana na miti hiyo hutengeneza kitu kinachoitwa Propolis. Propolis ni dawa ambayo ina uwezo wa kuzuia bakteria wa aina yoyote ile asiharibu asali. Watakacho fanya sasa baada ya kutengeneza Propolis ni kukizungushia au kumzungushia mdudu huyo ute huo ambao huwa kama gundi ngumu yenye rangi nyekundu, bila ya kubakisha upenyo hata mmoja, yaani watamzungushia mwili mzima, kwa unene wa milimita moja na nusu 1.5mm. ili kuikinga asali na uharibifu utakaotokea au kusababishwa na kitu hicho au mdudu huyo. Vilevile kama kutatokea nyufa katika mzinga wao, basi hutumia ute huo huo kuzibia nyufa hizo, ute huo unapokutana na hewa ya nje, huganda mara moja na kuwa mgumu sana ili kuzuia baadhi ya wadudu wadogo wadogo na bakteria wa aina mbalimbali wasiweze kuingia ndani ya mzinga, na kuharibu asali.

Haya ni mambo makubwa kabisa kufanywa na wadudu wadogo kama hawa. Ama kwa akika Mwenyezi Mungu ni mkubwa na mwenye Rehma nyingi. Kwa kuwapa iliham wadudu hawa ili waweze kuifanya kazi hii bila ya kuchoka wala kutegeana. Kama anavyosema Mwenyezi Mungu kuwa amewafunulia nyuki, kuwa wajitengenezee majumba yao katika milima, katika miti na katika wanayoyajenga watu na ale kila matunda ili haweze kutengeneza chakula kilicho bora na kilicho na dawa (matibabu/ponyo) ndani yake. Alhamdullilah kwa akika hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila hali.

B: Mzinga wa Nyuki:

Nyuki katika mzinga mmoja hufikia idadi ya nyuki wanaokisiwa kuwa 30,000 na zaidi. Nyuki wanapokuwa katika moja ya kazi zao za kutengeneza masega, huyaweka katika mwinuko wa nyuzi 130, kwapande zote mbili. Na nyuki huepuka kuweka masega sambamba na ardhi ili asali isimwagike chini. Nyuki hujining’iniza na kujishikiza wenyewe kwa wenyewe na kuwa kama duara kuzunguka mzinga wao, katika kila kona ya mzinga. Kwa kufanya hivi husababisha halijoto ya ndani ya mzinga kufanya hutengenezaji wa masega na nta kuwa rahisi. Nyuki uchota nta kwa kutumia miguu yao, iliyo na kama ndoana mbele na kuchanganya na majimaji yanayotoka matumboni mwao. huichanganya nta na majimaji hayo kwa kutumia midomo yao, mpaka kuwa laini ili waweze kuipaka katika kuta za masega yao ya asali. Masega hutengenzwa kuanzia pande nne tofauti tofauti juu kuja chini, toka pande tofauti katika mzinga na kuishia katikati. Na kupata usawa katika masega bila kukosea. Jambo ili la kutengeneza masega na mtindo wanaotumia wa kutengeneza masega yenye umbo la pembe sita limewashangaza wataalam mbalimbali wa kisasa. . Tena hutengeneza bila ya kukosea vipimo. Hutengenezaji ambao kwanza huanza katika kona tofauti tofauti pia kwa vikundi vikundi na kuelekea katikati. Je watu wa elimu ya Nadharia ya evolusheni (Evolution theory) wanayajua haya?  Soma Qur’an 45:4

 Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo ishara kwa watu wenye yakini…
Qur’an 45:4

Umbo ili la heksagoni linafanana na kichwa cha nati ya gali (bolt) na kama tulivyo eleza hapo juu kuwa, kila tundu moja la linanfanana na mwenzake. Japokuwa matundu yapo kwa maelfu. Uhandisi huu wa ajabu ambao unaonyeshwa na viumbe hivi vidogo wafaa kuzingatiwa sana na binadamu, juu ya kuwepo Mwenyezi Mungu. Matundu au masega kama yanavyo julikana, kazi yake kubwa ni kuwatunzia watoto wa nyuki, na kuifadhia asali. Katika mamilioni ya miaka nyuki wamekuwa ni watengenezaji wazuri wa asali, wasio wezwa kuigwa. Yaani ni bidhaa hiliyo bora kabisa isiyo na mpinzani wala mwigizaji aliyejaribu kutengeneza kitu kinacho fanana nacho. Hutengenezaji huu wa asali ya nyuki ni wa miaka zaidi ya milioni nyingi tu lakini sasa kwa nini wame chagua kutengeneza masega yenye umbo la pembe sita zilizo sawa yaani hexagon na si umbo lingine lolote lile mfano wa pembe tatu (Triangle) au pembe nane (Octagon) au pembe tano (Pentagon)? Jibu lake wanalo watu wa mahesabu ya maumbo (mathematician), wao wanasema hivi...

Umbo la hexagon yaani umbo lenye pembe sita zilizo sawa, ni umbo bora na ni zuri sana katika mahesabu ya jiometri. Kwa sababu huchukua nafasi ndogo, lakini huwa na ujazo mwingi katika eneo lake. Na ufanisi wake katika matumizi ni mzuri kwani umbo ili haliachi nafasi isiyoweza kutumika, tofauti na maumbo mengine. Kina chake kiko sawa kwa masega yote ya nyuki, na vilevile mzingo wake yaani mzunguko wake ni mdogo na mfupi na ujazo wake uko sawa. Vilevile hutumia nta kidogo katika kutengeneza masega yao, ukilinganisha na maumbo mengine kama pembe tatu au pembe nne. Kwa hiyo tunaona kuwa umbo la heksagoni hutumia nta kidogo sana wakati wa kutengeneza masega lakini wakati huo huo uhifadhi asali nyingi.  Jibu ili wataalamu wa hisabati katika eneo linalohusiana na hisabu za jiometri wamelipata baada ya tafiti nyingi na za miaka mingi sana. Lakini kwa uhakika ulio wazi kabisa hesabu hizi za kutengeneza masega katika umbo la pembe sita sawa (hexagon), hawakufanya nyuki wenyewe binafsi yaani kwa utashi wao tu, bali ni kutokana na maumbile yao aliyo waumbia Mwenyezi Mungu, kwa sababu tunaelezwa kwenye Qur’an 16:68 kuwa:

Na Mola wako mlezi amemfunulia Nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayo jenga watu... Qur’an 16:68

Isitoshe basi umbo la hexagon katika masega ya nyuki jinsi lilivyo matundu yake yanategemeana yaani umbo kwa umbo kuta kwa kuta na kuta zake ni nyembamba na zinahimili ujazo mkubwa wa asali.


Picha ya masega ya Nyuki nyuzi digrii 130

C: Jinsi nyuki wanavyo wasiliana:

Mawasiliano waliyokuwa nayo wadudu hawa, ni ya kiufanisi wa hali ya juu sana. Kwani utaratibu wao wa kuwasiliana ni wa ajabu mno. Nyuki siku zote husafiri umbali mrefu, ili kujitafutia eneo la malisho (mavuno) yao yaani Necta na Chavua. Nectar ni majimaji yanayopatikana kwenye maua, pamoja na Chavua (flower dust or pollen). Nyuki wana uwezo wa kwenda zaidi ya kilomita mbili, toka katika mzinga wao na kurudi. Nyuki aliyeko mawindoni anapogundua eneo la mavuno (maua), huruka kurudi mzingani ili kuwafahamisha wenzake, ni wapi na ni umbali gani toka kwenye mzinga mpaka kwenye mavuno yao. Je ni jinsi gani basi nyuki huweza kutaarifiana, umbali na eneo yalipo mavuno yao? Wataalam wa nyuki baada ya kuwachunguza wadudu hawa kwa kipindi kirefu, wamegundua kuwa nyuki utaarifiana kwa kutumia vitendo na harufu. Mawasiliano haya ya vitendo yapo ya aina mbili, nayo huitwa (Waggle & Round Dance), yaani mawasiliano ya kujitikisa na kujizungusha kwa kuchachawa.

Angalia mchoro hapa chini.
(Picha ya nyuki wakiwasiliana kwa namna mbili tofauti)

Mchoro wa kushoto chini unaonyesha mawasiliano ya kujizungusha kwa maana ya duara (Round Dance). Kabla ya yote yale, nyuki hukimbia huku akielekea kule kwenye mawindo (First it runs straight for short distance, the angle of the run indicating the direction of the source). Na hapo uchezesha tumbo lake pamoja na kuchezesha eneo la nyuma, kabla ya kufanya mzunguko wa kutengeneza duara. Na hii inamaanisha kuwa mawindo yao hayapo mbali ni chini ya mita mia (100). Na mchoro wa pili kulia juu ni mawasiliano ya kujitikisa na kuzunguka (Waggle Dance), na kuwa kama wanatengeneza umbo la namba nane, kuna maanisha kuwa mawindo yao yapo mbali, yaani zaidi ya mita mia moja (100). Kwa hiyo mapigo ya kuchezeza miili upokezana wao kwa wao, mpaka wote wanakuwa wameelewa ni wapi na kwa umbali gani, na pembe (angle) gani mawindo yao yanapatikana. Mfano wakitaka kufahamishana umbali wa mita 250, basi huchezesha eneo la chini ya tumbo mara tano kwa nusu dakika. Unaweza ukajiuliza kuwa, je hawa nyuki mbona hata usiku huwa wakiruka na kufanya harakati zao? Jibu lake ni rahisi tu. Ni kuwa macho ya nyuki jinsi yalivyo umbwa kwanza yana umbo la pembe sita (hexagon) na yapo zaidi ya mia, yenye lenzi zinazo jirekebisha zenyewe (involuntarily), kila baada ya dakika moja, ili kuwa sambamba na machweo ya jua. Kwa jinsi hii ya maumbile ya macho yao, nyuki hawawezi kupoteza mwelekeo wao hata mara moja, hata wakiruka hewani kwa zaidi ya dakika  kumi na tano (15). Vilevile macho ya nyuki yanasaidiwa na mionzi inayoitwa utraviolet rays. Kutokana na na mionzi hii inakuwa ni rahisi kwao kufanya kazi hata kwenye kiza.

               Aina ya pili ya mawasilano ya nyuki kama nilivyo ainisha hapo juu, ni kwa kutumia harufu, nyuki wanauwezo mkubwa wa kuhisi (sentient). Nyuki huwa hawana muda wa kupoteza katika kazi zao. Kwani nyuki hata siku moja huwa hawatui kwenye ua ambalo limekwisha tembelewa na nyuki mwenzake, kwa maana ya kuwa limekwisha tolewa chamvua. Ni vipi basi nyuki ufahamu kuwa ua analotaka kutua limekwisha tembelewa na mwenzake, na kuamua kulipita bila ya kupoteza muda kwenye ua hilo? Ili ni jambo dogo sana kwao, kwani nyuki anapotua kwenye ua na kuchukua alichofuata hapo, uacha harufu (Pheromones) kwenye ua hilo ili kila nyuki apitae hapo atambue na kufahamu kuwa ua analolipitia limekwisha tembelewa tayari. Kwa hali hiyo anakuwa hana muda wa kupoteza nguvu zake hapo.   

D: Ubora wa asali:

Makisio ya hutengenezaji wa asali kwa mwaka kutokana na idadi ya nyuki milioni hamsini (50 million), ni tani zipatazo 900,000 (haya ni makisio ya mwaka 2000 kutoka kitabu cha Leader’s Digest kiitwacho Why in The World?). Wataalamu kwa karne nyingi wamejaribu kutengeneza asali, lakini wameshidwa na hii ni kutokanan na asali kuwa na michanganyiko mingi ya sukari na virutubisho vya kiasili. (The bees’ way of making honey, too, is complex and difficult to copy). Hebu basi na tuangalie tunapata nini kutokana na asali, kwani Mwenyezi Mungu ametatufahamisha kwenye Qur’an 16:69 kuwa

…Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina MATIBABU kwa wanaadamu. Akika katika haya ipo ishara kwa watu wanao fikiri.
Qur’an 16:69

 Asali ni chakula bora cha kiwango cha juu sana ambacho, Allah (swt) ametuteremshia kupitia wadudu hawa aina ya nyuki. Na vilevile tunafahamishwa katika sura hii ya 16 kuwa asali ina uwezo wa kutibu. Sasa basi Asali ni nini? Asali ni mchanganyiko wa virutubisho mbali mbali, zikiwemo aina ya sukari zinazojulikana kwa jina la Glukosi (Glucose) pamoja na Fruktosi (Fructose), na madini mbalimbali vikiwemo; Magnesium, Copper, Iodine, zinc, Potassium, Calcium, Sodium, Chlorine, Sulfur, Iron na Phosphate, pamoja na vitamin B1, B2, B3, B5, B6, na vitamin C. Vitamin mara nyingi ubadilika kulingana na ubora wa necta, pamoja na chavua. Vile vile kwenye asali, kunapatikana aina mbalimbali za Hormones. Kama inavyoelezwa kwenye Qur’an, kuwa asali ni ponyo(kinywaji chenye kutibu) kwa wanadamu, na haya yamethibiti kwa wanadamu hivi leo. Kama ilivyotokea katika mkutano wa wanasayansi,  uliofanyika mwaka 1993 mwezi Sept. tarehe 20-26. Mkutano huu ulifanyika nchini China, na ulijulikana kwa jina la World Apiculture Comference. Na kuchapishwa katika jarida la Horriget News Paper, la tarehe 19th.Oct.1993. Katika mkutano huo matibabu ya kutumia asali yalijadiliwa kwa mapana sana, wanasayansi wa Kimarekani wao walielezea kuwa, ndani ya asali kuna vitu vinaitwa; Royal Jelly, chavua, na ute (Propolis, Bee resin), vitu hivi husaidia sana katika matibabu ya magonjwa mengi. Naye Daktari kutoka Romania, yeye aliwahi kujaribu kutibu mtoto wa jicho (Cataract), kwa wagonjwa 2094, kati yao 2002 walipona kabisa, na hii ni sawa na asilimia 96% ya wagonjwa waliopona kabisa. Daktari huyo alieleza kuwa Bee Resin au ute unaotokana na nyuki, unasaidia kuponyesha magonjwa mengine, mfano magonjwa ya ngozi (Skin Diseases), magonjwa ya kuvuja kwa damu (Haemorrhoid), magonjwa ya uzazi (Gynaecological Diseases) n.k.

 Siku hizi ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi umeongezeka kwa kiwango cha juu sana, katika nchi zilizo endelea na zinazo endelea. 


E: Baadhi ya faida nyingine za asali:

  • Sukari iliyoko kwenye asali humengenyuka kwa urahisi sana, na kugeuka kuwa glukosi na fruktosi kwa haraka. Hata kwa wale wenye matumbo mabovu (yenye maradhi).
  • Asali husaidia pia figo na utumbo kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
  • Asali ina kalories chache sana, ukilinganisha na kiwango cha sukari kilichomo kwenye asali, cha ajabu ni kuwa hutoa nishati (energy) nyingi katika mwili, lakini haisababishi ongezeko la mwili yaani unene. (Cholesterol)
  • Asali huyeyuka kwa haraka sana kuingia kwenye damu, ukilinganisha na vinywaji vingine, kama maji ya kawaida.  Asali huchukua takriban dakika saba tu kuingia katika mfumo wa damu.
  • Asali husaidia hutengenezaji wa damu mwilini, kwani hutoa nishati au nguvu inayosababisha hutengenezaji wa damu kuwa rahisi. Vilevile asali usafisha damu, katika mzunguko wake, na kusaidia mzunguko wa damu kuwa rahisi na mwepesi. Asali husadia kulinda mishipa ya damu isiathirike na maradhi yanayoshambulia mishipa ya damu. Asali pia husaidia kulinda ubongo na kuuwezesha kufanya kazi vizuri na upesi zaidi. Asali husaidia kuua bakteria wa aina mbalimbali inapotumiwa kwa matibabu na hasa kwenye vidonda. Pia asali husaidia kuondoa matatizo ya tishu (Tisue Difficiency) na udhaifu kwenye mwili (Body Frailty).

1 comment:

Qur'an 5:32