Sunday 16 August 2015

MCHANGO WA UISLAMU KATIKA MAENDELEO YA MWANADAMU


Katika maelezo mafupi namna hii haiwezekani kuwepo kwa suala la kutaka kuorodhesha namna ambavyo utamaduni wa Kiislam ulivyochangia katika maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu.

Hatuna njia ila kutaja japo kwa uchache tu wa ugunduzi muhimu uliotokana na vipaji vya watafiti wa Kiislam na pia kutaja wachache kati ya wasomi, wanafalsafa na waandishi wa kiislam walioongeza hamasa katika elimu ya sayansi na fasihi, na kuzivuta fikra za watu wa Magharibi (wazungu).

Unajimu (Astronomy): Elimu ya Anga na Sayari

Elimu na sayansi za kwanza kuvuta shauku ya wasomi wa Kiislam zilikuwa ni unajimu na Hisabati. Fikra zao zote bila ya shaka na mweleko wao uliwafanya Waislamu kuiendea sayansi ya uhakika.

Unajimu hasa sio tu uliwavutia wanasayansi, bali pia Makhalifa wa Mashariki na wa Magharibi kutoka Hispania na wa Kirusi na Makhan wa Kihindi pia walivutiwa na taaluma hii. Vituo vyya uchunguzi wa anga vilianza kujengwa katika kila mji maarufu katika Himaya ya Kiislam. Vile vya jiji la Baghdad, Cairo, Cordova, Toledo na Samarkand vilijipatia umaarufu sana duniani.

Chuo cha Unajimu cha Baghdad kilijulikana tangu enzi za utawala wa AL-Mansur, Khalifa wa pili wa ukoo wa Abbassid aliyetawala miaka ya 754 na 775, na ambaye pia alikuwa mnajimu. Hata wakati wa tawala za warithi wake, Harun al-Rashid na AL- Mamun, Chuo hiki kiliendelea kutoa kazi nzuri. Nadharia za zamani zilidurusiwa na makosa kusahihishwa na pia Majedwali ya Kigiriki yalisahihishwa. Chuo cha Baghdad kinastahili sifa kwa ugunduzi wa mizunguko ya sayari na jua, tathmini ya upotofu uliokuwepo juu ya umbile lake na utaratibu wa upunguaji wa mmuliko (ukali wa mwanga) wake, na pia ugunduzi wa kipimo halisi cha hesabu ya mwaka.

Chuo cha Baghdad kiligundua kuwa maeneo ya juu ya mwezi hayafuati kanuni maalum. Pia walitabiri kuwepo kwa vituo vya jua, kupatwa kwa mwezi na jua na kuwepo kwa vimondo na madude mengine angani. Walitafiti na kubaini kuwepo kwa mzunguko wa dunia kwa jua. Pia walikuwa watafiti wa kwanza kugundua Copernicus na Kepler.

Matokeo ya tafiti mbalimbali za vituo vilivyoasisiwa na Chuo cha Baghdad yaliwekwa kumbukumbu katika Jedwali la Unajimu lililothibitishwa, na Yahya bin Abu Mansuranaaminika kuwa muasisi na mtayarishaji wa jedwali hili.

Baadhi ya wasomi waliotokana na Chuo hicho ni pamoja na AL-Baitani, ambaye Lalande amemworodhesha kuwa ni miongoni mwa wanajimu ishirini (20) bingwa na maarufu waliowahi kutokea duniani. Mwingine ni Abu Wefa, ambaye matokeo ya utafiti wake yalikuwa na ubora wa zaidi ya karne kumi mbele ya ule ulio tolewa na Msomi wa Denmark aliyeitwa Tycho-Bracho, ambaye alihusishwa na ugunduzi wa Abu Wefa kuhusu tofauti ya vipindi vya mwandamo wa mwezi.

Ali Ibn Younis, mgunduzi wa (pendulum) timazi au mizani ya saa na vipimo vya jua, ambaye Khalif AL-Haken aliyetawala mnamo miaka ya 990 – 1021, alimwekea kumbukumbu kwa kujengewa kituo cha utafiti wa anga katika Mlima Mucaddam, anaaminika kuwa mmojawapo wa waanzilishi wa Chuo cha Cairo. Alilipitia jedwali la Hakim na kulihakiki na kuliwekea usahihi ambao haukuwahi kufikiwa na mtu yeyote hapo nyuma. Wakati huo huo, Hassan Ibn AL-Haitan, mnajimu mwingine na mwanahisabati wa chuo cha Cairo, alitayarisha tasnifu (treatise) au makala yake maarufu juu ya elimu ya Nuru (optics) au uoni, iliyosaidia kuweka msingi wa kazi iliyofanywa baadae na Roger Bacon na Kepler. Haishangazi kusikia kuwa Ibn Haitan alikuwa mtaalam wa kwanza kupendekeza lijengwe Bwawa maarufu la Aswan nchini Misri ili kuinua kiwango cha maji ya mto Nile.

Utafiti wa Anga ulitiliwa mkazo pia na utawala wa kiislam nchini Hispania. Amir wa Cordova, Abd aL-Rahman wa pili, alionyesha shauku na nia ya kuendeleza elimu ya sayansi hii. Kwa bahati mbaya ni tafiti ndogo tulizoweza kuzipata kutoka Hispania ilipokuwa chini ya utawala wa kiislam. Karibu kazi zao zote ziliharibiwa kutokana na vita vya kidini, ingawa tunaelewa kuwa kwa wakati huo, vituo vya utafiti wa anga katika miji ya Toledo na Cordova vilikuwa maarufu. Historia imeweza kutuhifadhia majina ya baadhi ya wasomi wa Andalusia kama Maslamah AL-Mahrebi, Omar Ibn Khaldun, Ibn Rushd (Averroes) na wengine wachache. Mtu anaweza kuhisi ubora wa kazi za Waislam hao zilizoharibiwa kutokana na kazi zilzotolewa baadaye na wasomi wa Kikristo waliosoma kwao na wengine waliosoma baadhi ya kazi za Waislam. Hivyo, inaonyesha kuwa Majedwali ya kinajimu ya Mfalme Alfonso (X) wa Kumi, yalitokana na kwa kiasi kikubwa na kazi za wasomi wa Kiislam.

Vita na migogoro ya ndani ambayo tangu karne ya kumi na moja vilivyozikumba nchi za Asia, viliathiri sana maisha ya kisomi yaliyokuwa yamekwisha jengeka katka jamii ya Kiislam. Bila shaka, vita hii ilizorotesha maendeleo ya ustaarabu wa dunia, ingawa havikuyasimamisha kabisa. Chuo cha Baghdad kwa mfano, kilinusurika na maanguko ya kisiasa ya Makhalifa wa Nchi za Mashariki, yaliyoisambaratisha dola ya Kiislam. Ubunifu wa Chuo hicho haukukoma ila uliendelea hadi katikati ya karne ya (15) kumi na tano. Wakati huohuo, mvuto wake ulienea hadi kuzifikia nchi za Asia ya Kati, India na hata Uchina. Mmojawapo wa wasomi wa Kiislam Abd aL-Rahman Mohammed bin Ahmad AL-Birun aliyejenga mahusiano kati ya elimu ya Wasomi wa Shule ya Baghdad na ile ya wasomi wa Kihindi, hakukosekana hata mara moja katika Ikulu ya Mahmud hapoGhazna, aliyeishi mnamo miaka ya 997 – 1030. Mojawapo ya kazi zake nyingi ni uchapisho wa vipimo vya kijiografia vya Longitudo na Latitudo za miji mikubwa duniani.

Sultani wa Seljuk Malik Shah aliyeishi mnamo (1072 – 1092), alikuwa msomi na mtawala aliyevutiwa na taaluma ya unajimu. Uchunguzi alioukazania ulisababisha kufanyika kwa marekebisho yaliyosahihisha na kuiboresha kalenda, karne kumi mbele ya marekebisho yaliyofanywa kwenye kalenda ya Kigrigori (Gregorian calender). Heshima na sifa za marekebisho hayo yanamwendea hasa Abdur Rahman Hassan na Omar Khayyam, ambao kazi yao imewafanya kuwa watu mashuhuri wasioweza kusahaulika duniani.

Watawala wa Kimongoli nao waliikazania elimu ya sayansi. Hulagu, mtawala aliyekuwa mkatili na ambaye ndiye aliyeuharibu mji wa Baghdad, naye alijenga kituo cha utafiti wa anga hapo Meragah, na alimteua Nasr ed – Din Tusi kuwa Mkurugenzi wake. Huyu alihusika na ukamilishaji wa vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumika kuchunguzia anga. Kutoka katika kituo hicho kipya, matokeo ya kazi za Chuo cha Baghdad na Cairo yalifikishwa hata Uchina ilipokuwa chini ya utawala wa Kubilai Khan.

Lakini ilikuwa ni wakati wa utawala wa Ulug Beg, mjukuu wa Tamburlaine, ambapo unajimu wa Waislam ulipopata mafanikio makubwa kabisa. Ulug Beg ambaye jina lake kama la baba yake Shah Ruh, linahusishwa kwa karibu sana na kazi nzuri za usanii na harakati za ufasaha (taaluma ya fasihi) zilizoendeshwa na Timuridh; alikuwa mpenzi wa taaluma ya unajimu. Inaaminika kuwa alikuwa mmojawapo wa wasomi wa mwisho mwisho waliotokana na Shule ya Baghdad. Kazi yake, ambayo ilichapishwa mwaka 1437, ilitoa picha halisi juu ya maarifa ya unajimu kwa siku hizo na mwelekeo wa taaluma hiyo kwa siku zijazo.


Somo la Hisabati (Mathematics)

Pamoja na unajimu, Hisabati ni sayansi iliyopendwa sana na Waaislamu. Kanuni nyingi za hesabu, jiometri na aljebra ziligunduliwa na wasomi wa Kiislam.

Katika hesabu, mpaka leo bado tunatumia tarakimu na njia za kufanyia hesabu zilizogunduliwa na Waiskamu. Uvumbuzi wa aljebra unahusishwa moja kwa moja na Waislamu. Wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Maarifa, Khalif AL- Mamun alimteuaMohammad Bin Mussa Bin Khwarizimi kuwa Mkuu wa Kituo hicho.

Tasnifu yake katika aljebra inaitwa: "AL–Gebr WaL-Muqabala (yaani Hesabu kwa njia ya Alama)".Ni kutokana na sehemu ya kwanza ya kazi yake hii tulipopata jina la hesabu za "algebra"na kutokana na jina lake pia tumepata "algorithm".

Kazi hii, kama ilivyotafsiriwa na Mzungu aitwaye Gerad mwenyeji wa Cremona, alisema: "baada ya kuwa msingi wa jumba la hesabu lililojengwa na Waislamu waliomfuatia baadaye, alikuwa na wazo la kuanza kuwafundisha watu wa Magharibi juu ya ubora wa kutumia aljebra katika kufanya hesabu za ukokotozi (algebraic calculus) pamoja na decimali."

"Mojawapo ya mawazo bora ya kisayansi toka kwa wasomi wa Kiislam, AL- Khwarismi bila shaka ni mtu aliyetoa mchango bora katika maendeleo ya somo la Hisabati wakati wa zama za karne za Kati na hata sasa", kama anavyodhani Philip Hitti.

Kazi yake iliendelezwa na Thabit bin Gharrah, aliyefasiri Almagest, kazi ya Ptolemy, aliyegundua matumizi ya algebra katika hesabu za changanuzi (jiometri au geometry).

Trigonometria (elimu ya hesabu za pembe tatu) ni mojawapo ya elimu ya hesabu ambayo Waislamu waliiendeleza kwa bidii kutokana na matumizi yake katika uchunguzi wa anga.

Hatua za awali katika elimu hii zinaanzia kwa AL-Baitani, aliyekuwa na kipaji cha kugundua hesabu za vipande vya mduara (arc), ambazo Wagiriki walizitumia katika kufanyia mahesabu yao. "AL- Baitani alikuwa wa mwanzo kutumia katika kazi zake za mahesabu, maneno ya ‘sine’ na ‘cosine’. Pia alikuwa mwanzilishi wa hesabu za ‘tangent’ wakati huo ikiitwa: kivuli endelevu (au extended shadow)."

Uanzishaji wa matumizi ya "tangent" (au msitari unaogusa duara bila ya kuukatiza) umeonyesha kuwa na manufaa makubwa. Wanahisabati wa zama zilizofuata hawakufurahishwa na uvumbuzi huo hadi baada ya kupita miaka mia tano ambapo pia ulihusishwa na Regimontanbus, lakini hata karne moja baadaye, Corpenius hakuwa na taarifa nao.

Uvumbuzi wa namba "ZERO" wa Muhammad bin Ahmad mwaka 976 ulileta mageuzi makubwa katika taaluma ya hisabati, ingawa haikutumiwa katika nchi za Magharibi hadi mwanzoni mwa karne ya kumi na tatu (13).

Mwisho tunaweza kusema kuwa Nasr Ed-Din Tusi alikuwa mtu wa kwanza kutilia mashaka kutoshambulika kwa jiometria ya Euclide. Anapaswa kuchukuliwa kama mtu aliyekuwa amewatangulia tena kwa mbali kitaaluma akina Lobatchevsky na Rieman katika jiometri isiyokuwa ya Ki- Euclide. 

Somo la Fizikia (Physics)

"Ni Waislamu wenye asili ya Kiarabu ambao wanapaswa kuchukuliwa waasisi wa elimu ya Fizikia", kama asemavyo A.Humboldt. Ni bahati mbaya kwamba makala maalum kuhusu fizikia, nyingi zilipotezwa. Nyingi zinajulikana tu kwa majina, ila chache tu ya kazi zao zimeweza kupatikana na hili limethibitisha maoni ya Humboldt.

Tasnifu juu ya taaluma ya uoni (optics) au nuru ya Ali Haitan (Alhasen) aliyeishi mnamo 965 – 1039, lilikuwa ni jambo muhimu katika sayansi. M. Charles anasema kuwa:"lilikuwa ndilo chimbuko la sayansi ya leo kuhusu taaluma ya (uoni) nuru."

Kazi hii inaeleza namna ya ujengekaji wa taswira katika kioo, maji na hata viwango vya ukubwa wa taswira hizo, pamoja na matumizi ya vyumba vya giza (dark rooms) katika taaluma ya utengenezaji wa picha. Utafiti wa Hassan Ali Haitani kuhusu Lenzi za miwani na za kukuzia maumbo (microscope), ulihamasisha kufanyika kwa majaribio mengi juu ya sayansi ya uoni yaliyofanywa na Roger Bacon, Kepler na wengine wa nchi za Ulaya. Akikosoa nadharia ya Euclid na Ptolemy, Alhasen alikuwa wa kwanza kutoa maelezo sahihi juu ya sura halisi ya umbile la jicho, uono wa Lenzi na darubini.

Elimu ya Waislam juu ya Umekanika ilikuwa imeendelea hasa kwa wakati huo. Tunaweza kupata dokezo kutokana na vifaa au zana walizokuwa wamezitengeneza na kuzitumia katika tafiti zao mbalimbali na ambazo pia zimetumiwa na watafiti wa nchi za Magharibi.E. Bernard kutoka Oxford ameeleza maoni yake kwamba ni Waislamu waliogundua matumizi ya (pendulum) timazi au mizania katika kutengeneza saa ya kuhesabia majira. Kwa vyovyote vile, hakuna shaka walikuwa na chombo cha saa chenye kutumia mizania tofauti na (clepsydra). Benjamin aliyekuwa mwenyeji wa Tudela ambaye katika karne ya 12 alitembelea jamii za Kiyahudi hapo Levant alielezea saa maarufu iliyokuwa ndani ya Msikiti Mkuu mjini Damascus.

Hakuna ubishi pia kuwa kompasi ilivumbuliwa na Wachina. Lakini ilirekebishwa na kusahihishwa na wasomi wa Kiislam kwa kuiwekea mshale ulioendeshwa kwa kutumia nguvu ya sumaku na kuiwezesha kutumika katika safari ndefu hasa za baharini na jangwani. 

Somo la Kemia (Chemistry)

Halitakuwa jambo la ajabu mtu kusikia kwamba Kemia (elimu ya uchangayaji wa kemikali) ni sayansi ambayo haikujulikana kabla ya matokeo ya utafiti wa Waislamu. Bila shaka, Wagiriki walifahamu mambo kiasi katika elimu ya madawa, bali hawakujua kuwapo kwa kitu chochote kiitwacho pombe, au asidi ya salfuriki, naitriki n.k. Ni Waislamu waliogundua yote haya yakiwemo matayarisho ya zebaki, silva natreti, potasium na sal ammoniaki. Kama tukiongeza pia kwamba mojawapo ya taratibu (processes) za kemia, kama utoneshaji (distillation), ni ugunduzi wa Waislam, na kwamba walikuwa watu wa mwanzo kutumia kanuni za usafishaji (sublimation), ugandishaji (crystallization), uunganishaji (coagulation) na chujaji (cupellation) wa kemikali mbalimbali. Hivyo, msomaji analazimika kuamini kwamba mchango wa Waislam ulikuwa ni wa msaada sana katika maendeleo ya elimu ya sayansi.

Orodha kubwa ya msamiati utumikao katika somo la kemia kama alcohol, alembic, alkali, elixir, n.k, asili yake ni katika lugha ya Kiarabu.

Bila ya shaka yoyote, Mkemia maarufu sana wa Kiarabu alikuwa ni Abu Mussa Djafar AL- Kuhi (Djeber) aliyeishi katika sehemu ya pili ya karne ya Nane (8). Kazi zake zimefanywa kuwa ni sehemu ya ensaikolopidia ya Kisayansi na zimetoa muhtasari na mwelekeo wa somo la Kemia kwa zama hizi. Nyingi katika kazi zake kuhusu somo la Kemia zimefasiriwa katika Lugha ya Kilatin. Maarufu kati ya hizo ni kitabu chake chenye maana ya "Jumuisho la Usahihi," kilichofasiriwa katika Lugha ya Kifaransa mnamo mwaka 1672.

Abu Bakr Zakaria AL- Razi (Razes), katika kitabu chake kiitwacho AL- Hawi, anaonyesha kuwa mtaalamu wa kwanza kuelezea namna ya utengenezaji wa salfuriki asidi na pombe kali (alcohol) kutokana na taratibu ya utoneshaji wa nafaka zenye wanga au sukari, baada ya kuchachishwa kwa kuvundikwa.

Katika sayansi hii, Waislamu waligundua kanuni nyingi kutokana na kuhusisha Nadharia katika ufanyaji wa Majaribio.

Majaribio ya kemia katika taaluma ya madawa (pharmacy) ni mojawapo ya mchango mkubwa na wenye manufaa kwa binadamu uliotolewa na wasomi wa Kiislam. Idadi kubwa ya bidhaa zenye matumizi ya kila siku kama kafuri (camphor), maji halisi yaliyotoneshwa (distilled water) kama yatumikayo kwenye betri. Bidhaa zingine ni pamoja na plasta, shira (syrup) na dawa nyingi za kujipaka (ointments) ni matokeo ya uvumbuzi wa Waislamu.

Maendeleo yao katika kugundua kemikali zenye matumizi ya viwandani yanaonyeshwa na ufundi wao mkubwa katika kutia rangi nguo, utengenezaji na usindikaji wa ngozi na uchovyaji wa vyuma.

Katika uvumbuzi uliokuwa na maana sana kwa maendeleo ya viwanda, ni pamoja na utengenezaji wa baruti, karatasi kutokana na pamba na marapurapu ya nguo. Ugunduzi wa baruti kwa bahati mbaya ulikuwa umehusishwa na akina Roger Bacon, Alberus Magnus na Berthold Shwarz. Na wakati mwingine ulihusihwa na Wachina. Huu sio ukweli kwani utafiti uliofanywa na Reinud na Fave umeonyesha dhahiri kwamba "kutokana na ugunduzi wa shura (saltpetre) wa Wachina, na matumizi yake katika milipuko, ni Waislamu pekee waliovumbua baruti kama kitu chenye kusababisha mlipuko. Na hii inaonyesha kuwa ndio waliokuwa wa kwanza kutengeneza silaha za moto, walizozitumia mnamo mwaka 1342 kuihami Algeziras iliposhambuliwa na Mfalme Alfonso wa XI."

Haitakuwa vibaya kukazia tena ugunduzi wa karatasi, ugunduzi ambao ulifunua ukurasa mpya katika ustaarabu wa mwanadamu. Kuenea kwa vitabu na zoezi la kuanza kujifunza kusoma na kuandika, yote yamewezekana baada ya Waislamu wa Kiarabu kuanza kutumia karatasi kama tuzijuavyo leo hii, badala ya matumizi ya kizamani ya vipande vya ngozi na vipande vya nguo hasa za hariri kama walivyokuwa wakivitumia Wachina.

Sayansi ya Maumbile (Natural Science)

Katika sayansi asilia, baada ya kuelewa maoni ya waandishi wa Kigiriki, Waislamu wa enzi hizo nao walianza kuitafakari na kuichunguza (nature) asili ya maumbile na kutoa mahitimisho (observations) yao wenyewe. Kutokana na juhudi zao waliweza kutaja nyongeza ya mimea 2000 katika idadi ya mimea iliyokuwa inajulikana. Taaluma ya Waislamu ya Madawa ilihusisha matumizi ya mimea na michanganyiko ya vitu ambavyo havikujulikana kwa Wagiriki. Matumizi ya sukari badala ya asali yalisababisha kuwepo kwa madawa mbalimbali yenye harufu na ladha ya kuvutia kwa wanywao katika uponyaji. Kwa kutumia sukari, Waislamu waliweza kutengeneza madawa mbalimbali pamoja na uwezo wa kuhifadhi mboga na matunda.

Waislamu ndio waliowaonyesha walimwengu haswa ulimwengu wa Kimagharibi aina mbalimbali za manukato na viungo vilivyotokana na mimea, maua, na mbegu mbalimbali.

Kahawa, bidhaa muhimu sasa hivi duniani asili yake ni katika nchi ya Yemen. Miongoni mwa wanyama wa kufugwa, farasi bora anapatikana Uarabuni, na mbuzi bora pia anapatikana Asia ndogo wakati kondoo wazuri wanapatikana nchini Morocco. Waislamu ndio walioiendeleza elimu ya kilimo bora na pia walijishughulisha na taaluma ya miamba (geology) 

Elimu ya Madawa (Medicine)

Baada ya hisabati na kemia, elimu ya utengenezaji wa madawa ilikuwa miongoni mwa sayansi iliyowavutia sana Waislam. Wakati wa karne za mwanzo za Hijra, taaluma hii ilifanywa kuwa mojawapo ya sehemu muhimu katika mfumo wa elimu kwa jumla. Ndio maana walitokea madaktari wazuri na maarufu pamoja na tasnifu (makala) zao mbalimbali juu ya taaluma hii.

Madaktari wa Kiislam walileta changamoto muhimu katika sayansi ya madawa kwa nchi za Magharibi. Kwa karne nyingi vitabu vya AL-Razi (Razes), Ibn Sina (Avicenna), Abul Cassis na Ibn Zohar vimekuwa ni msingi wa elimu ya tiba katika Vyuo Vikuu vyote vya Ulaya. Chuo cha Tiba hapo Salerno na hasa Montpellier kilisifika sana duniani. Machapisho ya kazi za tiba ya AL-Razi yaliyojulikana kama Havi (au Maisha Bora), pamoja na kitabu chake kiitwacho Mansuri, viliendelea tena kwa karne nyingi kuwa vitabu vya kiada (miongozo) kwa taaluma ya tiba.

Havi, ni mojawapo ya juzuu tisa (9) zilizokuwa katika Maktaba ya Kitivo Cha Tiba cha mjini Paris, Ufaransa katika mwaka 1395. Humo kunapatikana maelezo ya dalili za homa za magonjwa mbalimbali kama ya ndui na surua. AL-Razi alianzisha matumizi ya dawa baridi za kumharisha mgonjwa katika kulainisha tumbo lake. Pia alitoa dalili za ugonjwa wa kiharusi na matumizi ya maji baridi (sponging) katika kupunguza homa kali. Anahusika pia na ugunduzi wa seton, kwani alikuwa akiitumia mara kwa mara. Vitabu vya AL-Razi vilitafsiriwa katika lugha ya Ki-Latin na kuchapishwa nakala mara nyingi na hasa katika miaka ya 1505 hapo Venice, mwaka 1428 na 1578 hapo jijini Paris, Ufaransa. Makala yake juu ya ugonjwa wa ndui ilichapishwa tena mwaka 1745.

Abu Ali Al-Hussein Ibn Abdallah, aliyejulikana kote Ulaya kama Ibn Sina na kwingineko Ulimwenguni kama Avicenna, bila shaka alikuwa daktari maarufu. Kitabu chake cha Kanuni za Tiba (Canun Fi’l Tib) kilichapishwa kwanza katika lugha ya Kiarabu hapo mjini Roma mwaka 1593. Kilitolewa katika juzuu tano katika fani za fiziolojia (elimu ya viungo), kanuni za Afya, patholojia (elimu ya magonjwa), elimu ya Tiba (therapeutics) na taaluma ya famasia (yaani ya utengenezaji wa madawa (pharmacy).

Kwa takriban miaka mia sita hivi kuanzia karne ya 12 hadi ya 17, vitabu hivi vilisaidia kuwa msingi wa Taaluma ya Tiba katika Vyuo Vikuu nchini Italia na Ufaransa. Katika karne ya 15 vilihaririwa mara 15 katika lugha ya Ki-Latin na mara moja katika Kiebrania (Kiyahudi).

Vilichapishwa tena na tena hadi kufikia karne ya 18 na hata mwanzoni mwa karne ya 19 ambapo mihadhara kutokana na mafunzo yake, iliendeshwa katika Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha hapo Montpellier. Licha ya hayo, naye Ibn Sina aliandika kitabu chake juu ya Tiba ya ugonjwa wa Moyo na hata mashairi kuhusu elimu ya madawa. Kamusi yake yenye orodha ya madawa na tiba zake iliainisha madawa yapatayo 760.

Mojawapo ya hatua muhimu iliyofikiwa na madaktari wa Kiislam ni katika nyanja ya upasuaji (surgery). Hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya 11 walishaelewa jinsi ya kutibu magonjwa ya macho (hasa mtoto wa jicho), kutokwa na damu puani, na matumizi ya tiba za dawa joto (caustics). Pia wasomi wa Kiislam walishajua matumizi ya ganzi(anaesthetics), ingawa yamekuwa yakichukuliwa kuwa ni uvumbuzi wa siku hizi. Wao, kabla ya kumfanyia mgonjwa operesheni (upasuaji), walimnywesha kwanza dawa ya kumtia usingizi mzito, iliyotokana na mmea ulioitwa ‘danel’, hadi hapo alipoonekana kuzimia.

Daktari wa Kiislam maarufu katika upasuaji aliitwa Abul-Qasim Khalaf bin Abbas(Abulcassis), aliyeishi mjini Cordova na kufariki mwaka 1107. Mwanafisiolojia maarufu Haller anadai kwamba "kazi za Abulcassis ndizo zilizokuwa chanzo ya changamoto kwenye taaluma ya upasuaji hadi kufikia kwenye karne ya 15." Elimu ya upasuaji ya Abulcassis ilichapishwa kama kitabu katika lugha ya Ki-Latin mwaka 1497.

Chini ya tawala za Kiislam, Hispania nayo iliweza kutoa madaktari bingwa na miongoni mwao ni Ibn Zohar na Averroes (Ibn Rushd). Ibn Zohar, alianzisha katika fani ya tiba, kanuni ya uchunguzi kwanza. Jambo muhimu katika matibabu yake ni kuanzia kwenye mwili wenyewe kwamba una uwezo asilia (immunity) wa kujikinga na baadhi ya magonjwa. Alikuwa mtu wa kwanza kuunganisha somo la tiba, upasuaji na madawa na kuliweka kama somo moja. Maandishi yake juu ya taaluma ya upasuaji ndiyo ya mwanzo kuelezea sura halisi ya koromeo (bronchotomy), na maelezo ya kina juu ya magonjwa ya mifupa, viungo na taratibu za tiba zake.

Averroes (Abul Walid Mohammed Ibn Rushd) kama mtu aliyeendeleza kazi za Aristotle, hatimaye alikuja kuwa daktari bingwa, na pia alitoa Tahariri (commentary) juu ya kitabu cha Ibn Sina (Avicenna) kiitwacho "Canun" na pia kile cha Galen. Kwake tumfaidika kutokana na makala yake kubwa kuhusu "theriac" na pia kitabu chake juu ya homa na sumu mbalimbali pamoja na tiba zake. Kazi yake kubwa ni pale alipotoa kitabu cha Tiba kiitwacho Kulliyet, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1490 hapo mjini Venice na baadae kiliendelea kuchapishwa katika nchi mbalimbali duniani.

Tiba ya macho inayoendelezwa hivi sasa duniani asili yake ni katika elimu ya sayansi ya Waislamu. Kitabu cha "kumbukumbu ya Kanuni za Tiba ya Macho", alichotunga Ali Ibn Isaa kiliendelea kutumika kama kitabu cha kiada (reference) hadi majuzi kwenye karne ya 19. Operesheni ya kwanza ya kuondoa mtoto wa jicho ilifanywa kwa mafanikio makubwa na Al Muhsin mwaka 1256, na ndiye aliyegundua sindano (hollow needle) yenye uwezo wa kuingiza dawa katika mwili wa mwanadamu.

Ibn AL-Nafis, Msyria aliyefariki mwaka 1289 hapo Damascus, alikuwa ameshaelezea, tena kwa usahihi kabisa mzunguko wa damu mwilini, miaka ipatayo 300 kabla ya maelezo yaliyotolewa na Mreno aliyeitwa Serget, ambaye dunia imekuwa ikimdhania kuwa mtaaalam wa mwanzo kuelezea jambo hili.

Maelezo juu ya sura ya Mapafu na mzunguko wa hewa ndani yake yalitolewa na msomi kutoka Misri aliyeitwa Muhy Al-Dine Tatarui, katika Tasnifu (thesis) yake aliyoitayarisha kabla ya kuhitimu kwake katika Chuo Kikuu cha Freiburg mwaka 1924.

Maelezo mafupi juu ya somo la afya yanaweza kufanyika kama ifuatavyo. Sote tunaelewa kwamba Dini ya Uislam imejaa kanuni bora kabisa juu ya utaratibu unaomwezesha mtu kuishi kiafya, kama kuoga na kunawa mara kwa mara, makatazo juu ya ulaji wa nyama ya nguruwe na unywaji wa pombe. Zaidi ya hayo, Madaktari wa Kiislam walisisitiza zifuatwe taratibu za kiafya wakati wa kutibu magonjwa. "Hospitali za Kiislamu", anaeleza Gustave Le Bo, "zilijengwa katika misingi bora ya afya kuliko hospitali nyingi za siku hizi. Yalikuwa ni majumba makubwa makubwa yaliyoruhusu mzunguko huru wa hewa na zilikuwa na maji ya kutosha kabisa,"

Somo la Falsafa (Philosophy)

Kuna mambo mengi ambayo yametokana na mchango wa Uislam katika fani ya Falsafa, kama mtu akifuatilia historia hatua kwa hatua. Hapa tutaeleza mawazo ya jumla jumla tu ya Kiislam yaliyochangia kuleta maendeleo ya somo la Falsafa hasa yaliyochukuliwa na wasomi wa nchi za Magharibi.

Katika Ulimwengu wa Kiislam, mawazo ya Falsafa yalianza kuibuka mapema sana. Kuna wakati baadhi ya waandishi walikataa kabisa falsafa ya Kiislam. Walidai kwamba dhana yoyoye nje ya maelezo ya Qur’an au mawazo juu ya kuwepo kwa dini nyingine hayakuwa na nafasi katika Uislam. Hivyo kikawa ni kigezo cha baadhi ya wasomi hasa wa Magharibi kukataa utambuzi wa mchango wa Uislam katika maendeleo ya somo la Falsafa.

Hivyo, haikuchukuwa muda mrefu tangu vitabu vya Historia vilipoanza kufundisha kwamba Waislamu wenye asili ya Uarabuni walipovamia Misri, Khalifa Omar Ibn Khattab aliamrisha ichomwe Maktaba maarufu ya mjini Alexandria, akidai kwamba "kama vitabu vyake vinaendana na falsafa ya kiislam, basi havina maana yoyote, na kwamba kama haviendani nayo basi ni vya hatari."

Hakuna mtu leo mwenye kujua vizuri somo la Historia ya Uislam, anayeweza kujali tena dai hilo kutokana na ushahidi uliokwishathibitishwa kihistoria wenye kupinga maoni kama hayo. Wala sio haki au vyema kudharau mawazo ya Uislam kwa kuyapendelea mawazo hafifu ya kijakazi ya wanafalsafa wa Kiyunani.

Falsafa ya Kiislamu imeweza kuthibitishwa kuwepo kwake tangu karne ya mwanzo ya zama za Uislam kama ulivyoenezwa na Mtume Muhammad (S.A.W), ambayo imehusishwa moja kwa moja na theolojia ya uislam. Kuwepo kwa Mwenyezi Mungu mmoja, upekee wake, uwezo wake Mkuu, Mtenda Haki (asiyedhulumu), Mwenye Huruma (kwa viumbe vyake), na sifa nyinginezo nyingi ni miongoni mwa mada ambazo zilihitaji kutafakariwa kwa kina ili kuweza kuzielewa kiusahihi.

Mawazo mbalimbali yaliibuka wakati wa mijadala ambayo wakati mwingine ilikuwa mikali kabisa. Makundi yenye mitizamo tofauti yaliibuka kuhusu masuala ya hatima ya watu iliyokwisha kadiriwa (na Mwenyezi Mungu), uhuru wa imani (kuabudu), ukombozi kwa njia ya vitendo au imani, Khalifa wa Mtume kama kiongozi wa muda wa kuiongoza jamii ya Kiislam mara baada ya Mtume kufariki na masuala mengine mengi.

Haya yalikuwa ni makundi ambayo yaliyojulikana kama Kharidji, Murdji na Kadari.Mwanzoni mwa karne ya 2 Hijria, lilizuka kundi la Mu’tazili. Yote haya yalisababisha zidurusiwe tarehe za tafsiri za Wagiriki, ambazo hazikuwa zimefanyika hadi wakati wa Ukhalifa wa AL-Mansur mnamo miaka ya 735 – 774, na pia ni ushahidi wa kuwepo kwa maendeleo tofauti ya uislam yaliyojitegemea.

Kwa kuidurusu, kuisambaza na kuitumia elimu ya watu wa kale, Falsafa ya Uislam ilitokea kuwa changamani (complex) na pambanuzi (subtle). Katika karne ya 3, wakati wa utawala wa AL– Kindi, kundi la wasomi wenye kushabikia somo la Falsafa lilianzishwa. Kundi hili lilichambua mafundisho ya Kiyunani (Kigiriki) na ya Plato. Wasomi wengi wa Kiislam walishughulika zaidi na kuoanisha mawazo ya Plato na Aristotle na kuyahusisha na mafundisho ya Dini. Katika Falsafa, kama ilivyo katika sayansi yoyote, wasomi wa Kiislam walionyesha kila aina ya shauku ya kutaka kujiendeleza kielimu. Matatizo yote yenye kuhusu kiini cha mambo kama yanavyotafakariwa na mwanadamu, aina zote za tafakari, kupitia kwenye Nadharia ya Kushuku na Mantiki, yaliweza kuelezeka katika mitizamo mbalimbali ya kifalsafa.

Tunaweza kuuchunguza usomi wa Kiislam kwa undani zaidi kutokana na umuhimu wa ushawishi (influence) wa wahubiri wake walivyokuwa makini na masuala ya Dini, na pia kutokana na wasomi hawa kuwa misingi ya falsafa iliyojengeka Ulaya kuanzia karne za zama za Kati. Avicenna (Ibn Sina) na Averroes (Ibn Rushd), walisifika sana katika Ulimwengu wa Magharibi kuliko Mashariki, ambako walijulikana tu kama madaktari au watabibu.

Umashuhuri wa Ibn Sina, ambaye alifikiriwa na watu kuwa kigezo cha kilele cha usomi wa karne za Kati, ni kutokana na kazi aliyoitoa katika seti ya vitabu vyenye kuzungumzia mada mbalimbali. Tulishaelezea kazi zake katika taaluma ya Tiba. Pia, alifanya mengi katika fani za Sayansi na Falsafa. Anaheshimika kutokana na kuanzisha taratibu za kisayansi zilizodumu kwa karne nyingi bila ya kubadilishwa. Kama msomi mkuu, alianzisha somo la Falsafa na kulitolea mwelekeo wa siku hizo na za baadae. Mawazo ya Aristotle na Plato pamoja na kuyasoma, hayakuathiri asili ya mawazo yake mwenyewe. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kumjadili Aristotle na pengine aliweza kumkosoa na kutoa hitimisho lenye mantiki. Kazi zake kubwa zilizowekwa katika vitabu ni pamoja na: Kitab AL- Shifa (au Taaluma ya Tiba), AL- Hidayat Fi’l Hikmat (au Mwongozo katika Hekima), Hadithi ya Hayy Ibn Yagzan, Kitab AL-Isharat Wa’al Tanbihat (au Mwongozo wa mafunzo ya Ishara na Tahadhari), n.k. Tafsiri ya kwanza ya Ibn Sina ilifanyika mwanzoni mwa karne ya 12.

Ushawishi wa Ibn Sina katika maendeleo ya somo la Falsafa kwa nchi za Magharibi ulikuwa mkubwa sana. "Hakuna Tasnifu ya msomi yoyote ambaye haikumnukuu Avicenna,kama anavyosema mamaA.M. Gorchon.. Na tafakari zaidi zinaonyesha wazi zaidi kwanba Avicenna alizivutia sana fikra za wanafalsafa wa Ulaya."

Albetus Magnus alimchukulia kama mtu wa mfano mwema ingawa yeye mwenyewe alikuwa msitari wa mbele katika kuishambulia falsafa ya Kiislamu. Naye Renan, katika kitabu chake chenye maana ya "Averos na Uaverosi", hakusita kuthibitisha kwamba masomo yaliyotolewa katika Chuo cha Mtakatifu Thomas yalitegemea kwa kiasi kikubwa elimu ya Ibn Sina. Mt. Thomas mwenyewe, ambaye alivutiwa sana na Ibn Sina, hakuwa mgeni wa fikra zake. Papa Yohana wa 21, kabla ya kusimikwa kwake, "alifundisha nadharia ya elimu ambayo aliihusisha na Aristotle badala ya mwenyewe Avicenna." Hayo yamesemwa na wasomi kama akina William mwenyeji wa Auvergne, Alexander wa Hales na wengineo wengi ambao walisoma hapo kwa Mt.Thomas.

Averroce, jina ambalo limepotoshwa kutokana na Abdul Walid Mohammed Ibn Rushd, alikuwa pia na mafanikio makubwa yaliyoonewa wivu na wasomi wa nchi za Magharibi hata kumzidi Ibn Sina. Ni kutokana na Tahariri zake juu ya Aristotle ambazo zilimfanya kuwa maarufu zaidi ya wasomi wenzake wa Kiislam.

Azma ya Averroes (Ibn Rushd) ilikuwa ni kujitwisha dhima ya kihistoria ya kuzifundisha falsafa nchi za pande mbili za ulimwengu yaani Mashariki na Magharibi. Alikubalika kama Mhariri Mkuu wa kazi za Aristotle, msomi mkubwa kabisa, ingawa alishambuliwa na wengine kuwa hakuwa Mcha Mungu. Hata kama Albertus Magnus mara chache sana alimnukuu, kadhia ya Mt. Thomas Aquinas inakanganya. "Mt.Thomas", anasema Renan,"wakati huohuo anaonyesha kuwa adui mkubwa kupita kiasi wa Mawazo ya Ibn Rushd, na mtu anaweza kupata mshangao ulio wazi kuhusu mabadiliko ya ghafla ya mfuasi huyu wa kwanza wa Mwanafalsafa huyo mkuu. Albertus Magnus alitumia mawazo ya Ibn Sina wakati Mt. Thomas yeye alitumia sana mawazo ya Ibn Rushd."

Padri Asin Palacio, aliyesoma sana falsafa ya kidini itokanayo na mafundisho ya Ibn Rushd yaliyofundishwa hapo kwa Mt. Thomas, aliyafananisha na mafundisho yaliyotolewa katika nchi za Latin (Milki ya Kirumi), baada ya kuyachunguza maandishi mbalimbali ya Wanafalsafa wa Cordova na kuyalinganisha na yale ya Ibn Rushd. Kufanana kwa mawazo hayo kunaonyeshwa na matumizi ya misemo inayofanana kiasi kwamba hakuna shaka juu ya mchango (au ushawishi) wa Falsafa ya Mwislam huyu ulivyokuwa mkubwa katika mafundisho ya Wakatoliki.

Karne za 14 na 15 zilishuhudia kilele katika matumizi makubwa ya Falsafa ya Ibn Rushd. Katika Vyuo Vikuu vya Magharibi, Mihutasari yake ilitumiwa kama kiada badala ya makala za Aristotle. Yohana Baconthorp, aliyefariki mwaka 1346, aliyekuwa Askofu wa Jimbo moja nchini Uingereza, na daktari wa Mipango, aliamrisha yaingizwe mafundisho ya Averroes katika mfumo wa elimu katika Chuo chake. Naye Paul mwenyeji wa Venice aliyefariki mwaka 1429, alikiri waziwazi kuzipenda nadharia za Averroes (Ibn Rushd). Alipoliandaa somo la Falsafa mwaka 1473, Louis wa 11 alizifanya nadharia za Aristotle pamoja na Tahariri za Averroes kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wake. Naye Vicomercato alilifundisha somo hilo katika Chuo chake nchini Ufaransa toka mwaka 1543 hadi 1567.

Lakini ni Chuo Kikuu cha Padua kilichokuja kuwa Kitovu cha elimu ya Kiarabu kwa wakati huo. Ibn Rushd ndiye aliyeonekana kuwa bingwa wao. Mafunzo yake yalidumu hadi karne ya 17. Bologna, Ferrara na Venice zililazimishwa kufuata mafundisho ya Kirumi, ingawa hakukutokea pingamizi juu ya Tahariri za Kiarabu juu ya Falsafa ya Aristotle.

Mwaka 1240, Askofu William kutoka mjini Paris aliamuru yaondolewe mawazo ya Kiarabu katika baadhi ya maandishi na vitabu. Mwaka 1269 Etienne Tempier aliyekuwa Askofu wa Paris wakati huo pia, alithibitisha kutekelezwa kwa amri hiyo. Hatua zote hizi hata hivyo, hazikusaidia kuzima harakati za maendeleo ya Falsafa ya Kiislam. Falsafa hii iliendelezwa na Warabu na kuweza kuimarika zaidi. Ukweli Siger de Brabant, anayesemekana kuwa muasisi wa harakati za (Ibn Rushd) Averroes, alikuwa mwalimu wa Falsafa hii katika miaka ya 1266 na 1277 katika Chuo Kikuu cha hapo mjini Paris. Huko kabla mnamo mwaka 1227, aliyekuwa Papa wakati huo, aliamuru yapitiwe upya maandiko, na ndipo makala zipatazo 219 zilizoonekana kuwa za uasi dhidi ya Kanisa zilipopigwa marufuku. Matokeo yake ilikuwa ni kufukuzwa kazi kwa Bwana Siger, na baadaye alihukumiwa na Kanisa kutumikia kifungo cha maisha jela. Pamoja na hatua zote hizi, Uaverosi uliendelea kuimarika zaidi.

Kundi lililokuwa mstari wa mbele katika kuipinga Falsafa ya Averroes ni lile lililoamua kuanza kufuata mafundisho ya Kirumi na Kiyunani tu (lililoitwa the Humanist). Kwa mtizamo wao, walimwona Averroes kuwakilisha fikra za Waislamu, na kwa kuwa sasa walishaelewa moja kwa moja asili ya elimu ya kale, Waaislamu wakawa ni watu wa kushambuliwa, tena kwa nguvu zote.

Bila ya kujali wala ya kuthamini mchango wao mkubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya mwanadamu baada ya kuichambua na kuiendeleza elimu ya Wayunani (Wagiriki), badala yake walishutumiwa kwa kuudumaza na kuupotosha utamaduni wa kale, jambo ambalo kama tulivyokwishaona kuwa halikuwa la kweli.

Petrarch, aliyedhaniwa, na kwa uhakika zaidi kuwa miongoni mwa watu walioasisi ustaarabu unaoendelea sasa hivi duniani, aliandika katika mojawapo ya barua zake kwa rafiki yake aliyeitwa Jean Dondi maneno yafuatayo: "Mimi binafsi nalichukia sana kabila hili (la Waarabu). Kwani inaniwia vigumu sana kwangu mimi kuamini kwamba Waislamu wanaweza kuleta jambo lolote la manufaa (kwa watu)."

Hata hivyo, pamoja na mashambulizi haya yaliyotoka katika sehemu zote mbili, za walimu wa dini (theologists) na wasomi wa Kirumi na Kiyunani (the humanists), Uaverosi (falsafa ya Ibn Rushd) uliendelea na kusambaa kwa wasomi mbalimbali duniani hadi kufikia kwenye karne ya 17.
Harakati za kuendeleza mawazo ya Averroes (Ibn Rushd) zilikuwa kubwa, na kuwepo kwa uhakiki tofauti tofauti juu ya kazi zake ni ushahidi tosha wa jinsi gani alivyokuwa mwana falsafa makini kabisa wa Kiislam. Kumekuwepo na tofauti kubwa kati ya fikra sahihi za Ibn Rushd na mawazo ya wasomi wengine ambayo amekuwa akihusishwa nayo. Falsafa ya Averroes ni kitu kimoja na Uaverosi (Averroism) ni kitu kingine. Mambo hayo mawili hayana budi kutofautishwa.

Si jambo la kubabaisha tu katika kubainisha tofauti hizo. Tunatumai kutokana na maelezo tuliyoyaona hapo nyuma kwamba Ibn Rushd alikuwa amewazidi katika elimu ya Falsafa, wasomi wa Ulaya tena kwa karne nyingi tu, kiasi kwamba nadharia na mafundisho yake, hata yale yaliyopotoshwa ama kufichwa kwa makusudi, yalisaidia katika kujenga muamko wa kielimu katika bara la Ulaya na pia yalichangia katika kuondoa dhana potofu zilizokuwa zimedumaza na kukwaza uhuru wa watu kufanya tafiti na kutoa fikra mbalimbali.

Somo la Fasihi na Lugha (Literature)

Huenda mojawapo ya mafanikio ya Uislam ni katika mchango wake katika maendeleo ya somo Falsafa. Ukilinganishwa, ushawishi wake katika maendeleo ya somo la Fasihi ya Lugha bila shaka haukuwa mkubwa sana. Ila katika baadhi ya sehemu za nyanja hii, uislam ulitoa mchango mkubwa na ulio dhahiri kabisa.

Kama mtu ana shaka na hilo, anaweza kufuatilia asili ya taaluma ya utunzi wa nyimbo na mashairi katika nchi za Ulaya. Lini na wapi yalianza kutokea haya ni jambo ambalo linaloweza kuthibitishwa kwa usahihi kabisa. Yalianza kutokea katika nchi za Hispania na Ufaransa mwanzoni mwa karne ya 12, halafu taaluma hii ilianza kusambaa kupitia Italia na baadaye katika nchi nyingine za Ulaya. Fasihi juu ya mahaba na methali katika nchi ya Hispania ni miongoni mwa vielelezo hivyo. Kipindi cha mwamko wa Fasihi na Lugha katika nchi za Magharibi kilizidi historia ya maendeleo ya usomi. Ni kipindi kilichotoa hatma ya maendeleo ya ustarabu katika nchi za Magharibi.

"Ni vigumu kukosa kusisitiza", anaandika Gustave Cohen, " kwamba ubunifu na thamani ya aina ya ushairi wa Kiislam hasa katika kujenga hisia.. Hakika ni mama wa ushairi wa siku hizi, labda zaidi kuliko ule wa KI-Latin. Bila ya ushairi huu hawezi mtu kuzungumzia tenzi za Kitaliano, Kihispania, wala Kijerumani au Kifaransa."

Lakini, ni zipi hasa tungo za washairi? Tofauti ya mashairi haya na mengine ya kimapenzi yaliyojulikana tangu zamani, ni ulimbwende juu ya mwanamke. Heshima yake kubwa kama mtu mtukufu, pamoja na kuyatukuza sana mapenzi kama mambo ya kiroho. Hiyo ndiyo iliyokuwa dhamira ya mashairi ya watu kama Mfalme William wa 9, mtawala wa Aquitaine, ya Marcabru, ya Jauffre Rudel, Dante, Petrarch na wengine.

Mtu anaweza kujiuliza nini chanzo cha mawazo haya ya ghafla juu ya mwanamke, yaliyokuwa kinyume na utamaduni wa nchi hiyo yalipoanzia. Aina ya mahadhi ya nyimbo hizi bila shaka hayakuwa na asili yake katika jamii ya Wayunani wa kale, wala miongoni mwa Warumi.

Kazi za Julien, Ramon Menedez Pidal, na R. Nycle zinaonyesha kuwepo kwa washairi waliokuwa wakitangatanga kutoka Mashariki ya Kati na Hispania (nchi za Andalusi), waliosababisha kuletwa kwa mabadiliko katika fikra na hisia za watu wa nchi za Magharibi. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo kimoja nchini Hispania umeonyesha kuwepo kwa mashairi yenye mahadhi ya Ki-Andalusi, mifano ya awali ilithibitisha kuwepo kwa mashairi hayo mwishoni mwa karne ya 19.

Mahaba ya Plato, kama yalivyohusudiwa ya kunyenyekea sana matakwa ya mwanamke, utumishi katika jina la mapenzi, uzito wa maumivu ya kimapenzi, yote haya yalikuwa miongoni mwa vibwagizo katika tungo za Waislamu wenye asili ya Kiarabu tangu karne ya 8. Katika Andalusia, aina hii ya ushairi ilianza kuonekana katika karne ya 19 na ilijulikana kwa jina la "zajal".Ni kielelezo cha mojawapo ya mafanikio yaliyotokana na makutano ya tamaduni mbili za Waarabu na Warumi.

Kosa la kusikitisha lililotokana na vita vya kidini (kuukomboa msalaba na ukristo), ni kule kuingilia na kuharibu usanisi (muunganiko) huu uliokuwa umeanza kujitokeza wa kati ya tamaduni mbili za eneo la Mediterani, usanisi ambao ulikuwa ni jambo la kawaida katika maendeleo ambayo yangeleta faida isiyo na kifani katika fani za sanaa na fasihi.

Lakini hata wakati wa vita hii, mahusiano ya kiuchumi, kisayansi na kisanii, hayakukatizwa kabisa. Maingiliano bado yaliendelea kati ya mataifa ya Kiislam, Hispania na ya Kirumi. Katika maingiliano hayo, utunzi wa mashairi na nyimbo yalikuwa miongoni mwa mambo yaliyochukuwa nafasi kubwa. Miji ya Kiarabu iliendelea kuwa vitalu vya kuzalishia washairi, wanamuziki na wacheza dansi ambao walitumbuiza sana katika nchi za kusini mwa Ulaya.

Kazi kubwa ya Asin Palacios juu ya asili ya Tamthilia–chekeshi (comedy) za kiislam, imeonyesha ushawishi mkubwa kwa Dante wa Muhy Ad Din Ibn Arabi na wa mshairi aliyekuwa kipofu aliyeitwa Abul Ala Al-Maari, ambaye tungo zake mahiri zilijaa ndani yake falsafa ya kushuku au kutazamia mabaya.

Riwaya ya Kifalsafa ya Ibn Tofayl, Hay Ibn Yakzan, iliyotafsiriwa katika Ki-Latin na Edward Pococke mwaka 1671 na baadaye katika lugha nyingine, ilimhamasisha piaDaniel Defoe na kumsaidia katika utunzi wa riwaya yake maarufu ya "Robinson Crusoe."

Ibn Hazim, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi bora wa Kiislam kutoka Hispania, aliathiri kwa kiasi kikubwa fasihi za Magharibi. Kama mwandishi mahiri alitunga Hekaya na masimulizi mengi ambayo kuanzia karne ya 13 yalisambaa na kuzikumba nchi zote za Ulaya. Tungo za Hekaya zake zilitafsiriwa katika Kispaniola na mtu aliyejulikana kama Alphonse mwenye Busara, Mfalme wa Castille, na baadaye katika Ki-Latin, Kiyahudi, Kiajemi na Kifaransa. Lafontaine alikiri pia kuwa hekaya hizo zilikuwa ni miongoni mwa vyanzo muhimu katika tungo zake. Boccaccio, Chaucer na wasimulizi wengine wa Kijerumani, kwa kiasi kikubwa walivutiwa na utunzi wa hekaya hizo. Hapa hatuna budi kusisitiza mvuto wa Hekaya maarufu ya "Alfulela Ulela" (au The Thousand And One Nights), kwa watu wengi waliopata kuisoma huko Ulaya na hata hapa Afrika ya Mashariki.
Pia tunapaswa kuuelezea ubora wa tungo za mashairi ya Tennyson na Browning kuwa na asili ya Arabuni.

"Don Quixote", kazi ya Cervante imejaa asili ya Kiarabu. Mtunzi wa kazi hii aliwahi kufungwa kwa muda huko Algeria na aliwahi kuongea kiutani kwamba kitabu chake mwanzo kiliandikwa katika lugha ya Kiarabu.

Hivyo, mtu anaweza kuhitimisha, kama asemavyo Phillip Hitti kwamba, "kwa jumla mchango mkubwa wa Waislamukatika maendeleo ya fasihi na lugha katika zama za kati huko Ulaya, ni katika ushawishi wake katika utokezaji wa miundo ya lugha, kama ulivyoweza kubuniwa na wataalam wa Magharibi na hivyo kuweza kujinasua katika matatizo ya sheria ngumu za miundo ya lugha za awali."

Mtu pia hawezi kuimalizia sura hii juu ya Fasihi ya Kiislam bila ya kutaja ubora wa mashairi ya Waajemi (Wafursi). Mahadhi ya mashairi haya ndilo jambo lililoyafanya kupendwa na hivyo kuweza kusambaa haraka sana. Wataalam wa herufi za Kizungu, walielezea juu ya ushairi wa Waajemi kuwa ulijaa hamasa na shauku. Goethe, akiongea na Chancellor von Mueller aliwahi kusema: "kwa muda wa karne tano Waajemi walikuwa na washairi maarufu saba ambao walidhaniwa kuwa mabingwa, ingawa hata hao wengine ambao hawakuhesabika kuwa mabingwa, walikuwa ni bora zaidi kuliko mimi."

Mabingwa hao saba wa fasihi ya Kifursi ni Firdusi, Djelal Ed Din Rumi, ambaye alikuwa miongoni mwa washairi wakubwna wa ajabu Ulimwenguni kama si mbora wao wote, Sadi, mghani maarufu wa Kishirazi, Anwari, ambaye hakulinganishwa na yeyote katika utunzi wa wasifu, Hafiz, mtunzi mahiri wa mashairi yenye hisia za kimapenzi na ambaye alikuwa kipenzi cha Goethe. Wengine ni Nizami na Djami.

Hafiz alikuwa mshairi wa kwanza wa Kifursi kupata umaarufu huko Ulaya. Alikuwa ni Mjerumani aitwaye von Hammer Purgstall aliyepata heshima ya kumtangaza bingwa huyu wa "ghazal", mashairi ya mahadhi nyororo kwa watu wa Magharibi. Tafsiri ya "Diwan", kitabu chenye tungo zote za Hafiz, ilianza kupatikana kati ya miaka ya 1812 na 1813.

Kama ukweli ukitolewa mwanzo, ni watu wachache tu na labda wawe ni wasomi ndio wenye kuupokea. Lakini lilikuwa ni jambo jingine pale Goethe alipochapisha "West – Ostlicher Diwan" mwaka 1819. Tunaelewa kwamba kitabu hiki kina alama ya maandishi yenye maana kwamba: "Iwapo mtu atataja neno Mke na Roho akaiita Mme, yule mwenye kumsifia Hafiz atakuwa ameshuhudia ndoa ya maneno hayo mawili (mke na mme)." Pia mtu anaweza kusoma pale maneno yasemayo: "Mashariki imekatiza kiajabu bahari ya Mediterranean. Yule tu amjuaye na kumpenda Hafiz ndiye anayeweza kuuelewa wimbo wa Caldrenon."

Diwan ya Hafiz ilitafsiriwa katika lugha zote za Wazungu. Lakini umaarufu wote wa Hafiz, kama wa watunzi wengine wote wa Mashariki na Magharibi, ulizidiwa na ule wa Omar Khayyam. Bila shaka huyu alikuwa miongoni mwa watunzi waliosomwa sana tenzi zao na watu wa pande zote mbili za dunia.
Kuna angalau mpaka leo tafsiri kumi na mbili katika lugha za Kifaransa, Rubayat, Kiingereza, Kijerumani, Kirusi, Kitaliano, Kispaniola, Kidanish, Kihungaria na Kituruki. Na baadhi ya beti zake zilitafsiriwa katika lugha nyingine zaidi.

Klabu ya Omar Khayyam iliyoanzishwa mjini London mwaka 1892, ilsababisha kuanzishwa kwa taasisi nyingine kama hiyo katika nchi nyingi za Ulaya.

Mchango wa Uislam katika Masomo ya Jiografia na Historia

"Hamu yao ya kupenda kusafiri", anasema Renan, "ni mojawapo ya tabia za Waislamu na haswa Waarabu, na mojawapo ya mambo yaliyowafanya kuweka athari katika historia ya maendeleo ya ustaarabu wa aina mbalimbali duniani. Hadi kufikia zama za mwanzo wa safari za upelelezi kwa njia za baharini zilizofanywa na Wareno na Wahispania katika karne ya 15 na 16, hakuna watu waliokuwa wametoa mchango mkubwa kama Waislamu katika kupanua nadharia ya sura halisi ya ulimwengu na hivyo kuitolea maelezo sahihi sayari yetu hii tuishimo ambayo ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya kweli."

Mapema katika karne ya 9, wafanyabiashara wa Kiarabu walikuwa watu wa mwanzo kutembelea nchi mbalimbali, kama China, Afrika na nchi zilizoko kaskazini mwao kama Urusi. Hekaya ya Safari ya Suleiman mmoja, iliyoanza kutungwa mwaka 851 na kumalizika mwaka 880, na mtu aitwaye Abu Zayd, ilikuwa ni kazi ya kwanza kuchapishwa nchini China. Masudi (Hassan Ali Al-Masudi), ambaye umaarufu wake katika masomo ya sayansi ulitambulika mwishoni mwa karne ya 18, alifanya safari katika karne ya 10, ya kuizunguka na kuimaliza Himaya yote ya Kiislam kuanzia pembe moja hadi nyingine. Pia alitembelea nchi za visiwa kama Ceylon, Madagascar na Zanzibar. Katika kitabu chake chenye maana ya "Mbuga za Dhahabu", anaelezea hali ya nchi zote alizowahi kutembelea, milima yake, bahari, mabonde na hata tawala zake, na pia tamaduni mila na mifumo ya ibada katika nchi hizo."

Ibn Haykal al- Biruni, Idrissi na Ibn Batuta ni miongoni mwa wapelelezi na wasomi maarufu, na waandishi wa taarifa muhimu za kijiografia, ambao walisaidia kuwapanua mawazo wenzao Wazungu. Idrissi kwa mfano, aliyezaliwa hapo Palermo, alimtayarishia makala ya kijiografia Mtawala wa Sicily aliyeitwa Roger wa II. Anasema Sellidot kwamba; "Kwa miaka takriban mia moja na hamsini, wachora ramani wa Kizungu hawakuwahi kufanya lolote ila kunakili tu makala hiyo bila ya hata kuifanyia marekebisho makubwa."

Hebu sasa tuitaje ramani ya Ulimwengu iliyotayarishwa na Ulug Beg, mjukuu wa Timur (Tamburlaine), na muasisi wa Jedwali la Unajimu lijulikanalo kwa jina lake. Katika kulitayarisha jedwali hili, alitegemea zaidi taarifa za akina Nasr Ed Din Tusi na Al – Khoshadji, ambaye alilazimika kusafiri hadi nchini China, ili kuhakiki kipimo cha digrii moja ya meridian, pamoja na ukubwa wa Ulimwengu.

Hebu pia tuzungumzie chati (ramani) zilizotayarishwa na Waislamu. Sellidot anaripoti kwamba: "Vasco de Gama alipata kuiona mojawapo ya ramani hizo mnamo mwaka 1497, iliyotayarishwa na Malem Cana, Moor wa Gujarat na hivyo kuitumia katika safari yake ya kuelekea Melinda. Nyingine, iliyotayarishwa na Mwarabu aliyeitwa Omar, ilimsaidia Albuquerque wakati akisafiri katika bahari ya Oman na Ghuba ya Uajemi."
Ni kweli pia kwamba kazi za wasomi wa Kiislam zilisaidia katika ugunduzi wa bara la Amerika. Katika barua aliyoiandika akiwa Haiti ya mwezi Oktoba 1498, Christopher Columbus amemtaja Ibn Rushd (Averroes) lakini kwa jina la Aventuez, kama mtu aliyemsaidia katika kufikia dhana ya kuwepo kwa Nchi Mpya (yaani bara la Amerika).

Ukweli ni kwamba idadi ya wasomi wa Kiislam walioacha kazi zao za Kihistoria ni kubwa sana. Katika Kamusi ya Historia iliyotayarishwa na Katib Tchelebi, ijulikanayo kama"Hadja Khalfa", imekusanya mamia ya majina ya wana-historia maarufu wa kiislam.

Maandishi ya Kihistoria ya zamani zaidi ni yale yaliyofanyika wakati wa zama za Utawala wa ukoo wa Umeyyad. Miongoni mwa waandishi wa kwanza bila shaka ni pamoja na Abu Minaf, aliyenukuliwa na Masudi katika kitabu chenye maana ya "Mbuga za Dhahabu",au (Golden Pastures). Huyu alifariki mwaka 747 A.D (130 A.H). Wasomi wengi wa Ulaya hupenda kuwalaumu wanahistoria wa Kiislam kwamba walipenda zaidi kuandika ukweli wa taarifa au mambo kama yalivyo, bila ya kuyafanyia uchambuzi na kuyaacha mawazo ya jumla jumla bila ya kutafuta viunganishi vya matukio ya kihistoria. Lawama hizi pengine zinaweza kukubalika lakini si katika ujumla wake.

Bila shaka wanahistoria wengi wa Kiislam hawakupata fursa ya kujenga dhana kuu za lengo la somo la Historia, ambazo ndizo zilizoshughulisha zaidi mawazo ya wasomi wa Magharibi na ambazo zimechukuliwa kama Sayansi ya Historia ya siku hizi. Wasomi wa Kiislam, wao walijiona kuwa na jukumu la ukusanyaji wa taarifa mbali mbali na kuziweka katika kumbu kumbu kwa faida ya vizazi vya baadae. Wao walijizuia kutoa tafsiri na maamuzi juu ya mambo ya kale (ya kihistoria).

Dhana hii kuhusu somo la Historia, bila shaka ni kinyume na dhana ya watu wa Magharibi. Lakini je ni jambo la busara ama baya? Ni suala linalohitaji mjadala. Kwa vyovyote vile, mtu ambaye anahitaji kurithisha tamaduni na taratibu ambazo na yeye alirithishwa, bila ya kuzitolea maoni au uhakiki, anaonyesha uaminifu na kutoegemea upande wowote kuliko wale watu watoao nyaraka zilizokwisha dodoswa dodoswa na kuhujumiwa kwa lengo la kuzidhibiti kulingana na malengo ya imani zao.

Baada ya kuyasema hayo, itakuwa si jambo la busara kuwalaumu wanahistoria wa Kiislam eti walikuwa na mawazo finyu na kwamba hawakufanya maamuzi yao kwa makini. Badala yake, wamepata umaarufu kutokana na uono wao mpana, na walielezea hisia zao wazi wazi katika masuala ambayo kwa muda mrefu yalikuwa nje ya upeo wa watu wa Magharibi. Hivyo, ndio maana historia ya Fasihi na uandishi ilionekana sana katika kazi zao. Ndio maana pia, tunashindwa kuwataja wote hapa, ila kwa mifano ya wawakilishi wa wana historia wengi wa Kiislam.

Tabari (Abu Djafar Mohammad Ibn Djarir AL-Tabari)

 Aliyezaliwa mwaka 839 na kufariki dunia mwaka 922, kama mtaalam wa somo la Historia, mwana sheria na mwalimu wa Dini, alipata mamlaka ya heshima ya utoaji wa ushauri katika masuala hayo, heshima ambayo hakuwahi kuipata mtu yeyote katika Ulimwengu wa Mashariki. Masudi namuelezea Tabari kama mtu wa zamani lakini aliyekuwa amemzidi sana yeye, pale aliposema: "Kanuni ya Abu Djafar Mohammad Ibn Djarir AL-Tabari, ni kazi bora kuliko nyingine zote juu ya Historia. Ukweli wa taarifa na taratibu za kisayansi katika ukusanyaji wa taarifa zake, vinakifanya kuwa kitabu cha kufundishia."

Kitabu chake cha "Tarikh", ni miongoni mwa kazi za msingi sana katika somo la Historia ya Kislamu. Thamani yake inatokana na usahihi wa taarifa zake kuhusu mwanzo wa Uislam. Kimejaa taarifa muhimu sana juu ya Lugha, mila na desturi za watu wa enzi hizo. Simulizi ndani ya Tarikh ziliendelezwa hadi mwaka 914 A.D.

Masudi (Hassan Ali AL-Masudi), aliyezaliwa mjini Baghdad mwishoni mwa karne ya 9 na kufariki mjini Cairo mwaka 956, naye aliwafunika wengi kwa umaarufu kama alivyofanya AL-Tabari, kutokana na upeo na ubora wa elimu yake kuhusu masuala mbalimbali. Miongoni mwa mambo ya kumkumbukia ni historia ya utafiti wake katika somo la Fasihi. Anasema Renan kwamba: "mtu anaweza kudai kwamba Masudi, kama mtu aliyetarajia changamoto na uhakiki wa kileo, alitambua mchango unaoweza kutolewa na somo la Fasihi katika historia ya kisiasa na kijamii katika zama zozote husika."

Kazi kubwa za kihistoria za Masudi zimejumuishwa katika kitabu chake kiitwacho:"Akhbar Az-Zaman (Habari za Kale)", ambacho kilitolewa katika juzuu ishirini (20). Kwa bahati mbaya licha ya kupata taarifa juu ya vitabu hivyo, vyenyewe hatukuweza kuvipata. Vitabu vyenye maana ya "Mbuga za Dhahabu" na "Kitabu cha Mafunzo", ndivyo vitabu pekee vya mtaalam huyu ambavyo vimeweza kupatikana.

Ibn Miskawayh, mwanahistoria aliyefariki mwaka 1030, alikuwa miongoni mwa watu waadilifu wa Kiislam. Kazi zake pekee zinatosha kuonyesha kwamba ni lawama zitokanazo na mtizamo finyu zitolewazo kiholela na wasomi wa Kimagharibi kwamba wanahistoria wa Kiislam hawakuwa makini. Kwa fikra zake asilia, huru na zenye kuchukuwa tahadhari, Ibn Miskawayh ni mwandishi wa kitabu kiitwacho: "Tadjarib AL-Ummah" (au Uzoefu wa Mataifa), ambacho kinaelezea historia ya Arabuni na Ajemi ya kale hadi wakati wa uhai wake.

Alikuwa mtoaji wa mawazo yenye mantiki, na alikuwa na msimamo wa wastani juu ya Uislam. Ingawa hakueleza Maisha ya Mtume, lakini alionyesha kuwa Waislamu walianza sera za kujitanua kiutawala hata kabla ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W. Shauku yake kubwa ilikuwa juu ya masuala ya siasa, falsafa na matatizo ya kiuchumi. Ameongelea sana masuala ya miundo ya taasisi za kijamii na utawawa bora.

Katika mlolongo huo huo, kuna kazi zilizofanywa na Makkari (Ahmed Ibn Mohammad AL-Makkari), mwanahistoria maarufu kutoka Hispania ilipokuwa chini ya utawala wa Kiislam, alizaliwa mwishoni mwa karne ya 16 na kufariki mwaka1631.

Tasnifu yake iliyokuwa na kichwa chenye maana ya: "Jumuisho la dondoo za Historia na Fasihi za Waislamuu katika Hispania", ilichapishwa hapo mjini Leyden kati ya mwaka 1855 na 1859. Hiki ni kisima chenye taarifa kutoka sehemu mbalimbali za nchi ya Hispania, juu ya maisha, tamaduni na mila za wakazi wake.

Humo, mwandishi ametoa picha halisi ya maisha ya kila siku ya hapo Andalusia, inayoonyesha kuwa hata hapo kulikuwa na harakati za kisomi, licha ya zile zilizoendeshwa katika miji mikubwa kama Cordova, Granada na Seville. Maelezo ya kina kuhusu hali ya wanasheria, madaktari, wanamuziki na wasomi wa kike katika nyanja mablimbali, yalisaidia katika kuiunda upya jamii ya Kiislam ya watu wa Hispania.

Rashi Ed Din (Fadhl A-Rashid Ed-Din AL-Mamdani) ni miongoni mwa wataalam wakubwa sana wa somo la Historia kutoka Iran. Hamadan, Kazvin na Tebriz ni sehemu zinazobishaniwa kuwa huenda ndiko alikozaliwa bwana huyu. Kama mtaalm wa hali ya juu, alimwandikia Historia ya watu wa Mongolia Mfalme Ghazan Khan baada ya kuombwa kufanya hivyo. Humo aliongezea muhtasari juu ya historia ya makabila mengine na sehemu mbalimbali za nchi ya Mongolia. Kazi yake iliyoko katika juzuu nne (4) ijulikanayo kwa jina la: "Djami AL-Tawarth" (yaani Mkusanyo wa Historia), ilikamilika mwaka 1130. Kazi hii ndio iliyokuja kuwa msingi wa maarifa juu ya kuwepo kwa utawala wa Mongol na Turco. 

Elimu ya Siasa na Sayansi ya Jamii (Sosiolojia)

Kazi zilizoelekezwa kwenye Falsafa ya Siasa na sayansi ya Jamii, ni miongoni mwa vito vyenye thamani sana vilivyotokana na wasomi wa Kiislam. Waandishi, kwa kutumia lugha kuu za Uislam yaani Kiarabu, Kituruki na Kiajemi, walielezea kinaga ubaga maoni tofauti juu ya muundo bora wa serikali na namna bora ya kutatua matatizo mbalimbali ya jamii.
Al-Farabi, mwanafalsafa mahiri wa Kiislam kabla ya Ibn Sina, aliandika Tasnifu yake iliyojaa hisia za kiroho iliyoitwa kwa jina lenye maana ya: "Taifa au Jiji La Mfano (The Model City)."

Akianzia kwenye kanuni ya Plato kwamba binadamu aliumbwa kuishi kijamii, Al-Farabi alihitimisha kwa kusema kuwa muundo sahihi wa Taifa au Dola ni ule utakaohusisha eneo lote lililokaliwa na watu wa aina zote.

Dhana ya kuwa na Taifa moja mara nyingi huamsha hisia za Wazungu juu ya iliyokuwa Dola ya Kirumi, msuguano uliokuwapo kati ya Mamlaka ya Papa na Dola ile wakati wa zama za Kati, n.k. Hata hivyo, hilo halikuwa wazo geni katika falsafa ya Kiislam. Vile vile ni jambo la kiroho lenye kuhimizwa katika Theolojia ya Uislam. Jiji la Mfano, ni mojawapo ya dalili za kuwepo kwa dhana hiyo katika fikra za wasomi wa Kiislam. Kutokana na mwelekeo wa ajabu wa Falsafa yake, mtunzi analipatia Taifa hilo na watawala wake jukumu la kutenda uadilifu. Al-Farabi aliamini kwamba jukumu kubwa la Taifa kama hilo la Mfano ni kuwaundia Serikali sahihi na kamili raia wake itakayowahakikishia amani na usalama katika maisha yao ya hapa duniani na ya Akhera pia. Hivyo jiji kamili lilipaswa kutawaliwa na kiongozi mmoja tu mkuu na mwenye sifa zifuatazo: "mwenye busara na uwezo wa kutumia akili yake vizuri sana, mwenye kumbukumbu sahihi ya mambo, mwenye uwezo mkubwa wa kueleza mambo, asiyerukia mambo na kutoa maamuzi bila ya kwanza kuyatafiti, mwenye kujirudi na kushaurika, mkarimu na mpole kwa raia wake, mpenda kutenda na kutendewa Haki, mwenye msimamo na asiye dhaifu katika kutekeleza maamuzi au maazimio yaliyokubalika." Kama akikosekana mtu mmoja mwenye sifa hizo zote, hapo itabidi watafutwe watu wawili au watatu au wengi zaidi, ambao kwa pamoja, kutokana na sifa za mmoja mmoja, wanaweza kuzikamilisha na hivyo wapewe dhamana ya kuunda Serikali ya Taifa hilo. AL-Farabi, kama Plato, anafikia dhana ya aidha kuwa na serikali adilifu au Taifa la Kifalme (lenye kurithishana utawala).
Upeo wa mawazo ya AL-Farabi, unapingana na maadili ya Ibn Zahr, mwarabu aliyeishi Sicily katika karne ya 12 ambaye kazi yake iitwayo: "Salam AL-Mota", iliyolinganishwa na kitabu cha Machavelli kiitwacho "The Prince" yaani Mtoto wa Mfalme. Ndani ya kitabu hiki kuna maneno ya hekima kama yale yaliyoandikwa na Katibu wa Florentina, ingawa pia kimejaa ulaghai.

Msomi mwingine ni Al-Mawedi aliyeishi katika miaka ya 972 na 1058. Huyu alikuwa mwanasheria mahiri na Hakimu Mkuu hapo Ostowa, karibu na mji wa Nishapur. Alitunga kitabu kiitwacho: "AL-Ahkam Es Sultaniah" (yaani Kitabu cha Hukumu au Kanuni za Utawala bora). Kazi hii, ambayo mtu ataguswa na shauku ya kutaka kuelewa dhana ya Ukhalifa, ilikusudiwa kuongelea masuala ya taasisi za kisiasa, kijamii na kisheria katika dola ya Kiislam. AL-Ahkam Es Sultaniah na kitabu kingine cha AL-Mawedi kilichomaanisha "Kanuni za Serikali", baadaye vilitafsiriwa katika lugha ya Kifaransa.
Msomi mwingine aliitwa Ibn Khaldun. Huyu aliishi mnamo miaka ya 1332 na 1406. Wale wote waliozoea kuushutumu ustaarabu wa Kiislam, ambao huangalia yale yaliyochukuliwa toka kwa Wayunani, na kukataa ubunifu wa Kiislam, wanalazimika kutambua deni la Historia ya Falsafa ya kwanza kuandikwa, si Mwarabu au Mzungu, aliyepata kuwa na maoni juu ya historia ambayo kwa mara moja yamekuwa kamilifu na yaliyojaa Falsafa. Maoni ya watu wote hata ya wale waliomuelekezea lawama Ibn Khaldun, wansaema kwamba bwana huyu alikuwa mwanahistoria maarufu sana aliyepata kutolewa na Uislam na miongoni mwa walio bora na katika zama zote. Hapo zamani kabla ya kuwepo kwa somo la Sosiolojia (sociology) kama tulijuavyo hivi leo, kabla hata ya maelezo ya akina Comte, Vico, Marx na Spengler, Ibn Khaldun alishaelezea historia na hatua za maendeleo ya jamii ya wanadamu, na alijaribu kutoa maelezo ya kina kuhusu umuhimu wa somo la Historia na maendeleo yake kwa siku zijazo.

Ibn Khaldun aliweza kuikusanya Historia ya Ulimwengu mzima katika kitabu chenye juzuu tatu, ambazo zina Utangulizi na Tawasifu (autobiographies). Juzuu ya kwanza ikiwa na utangulizi hufanya sehemu inayoitwa "Prolegomena", (ambayo ilitafsiriwa katika lugha ya Kifaransa na mtaalam mmoja aliyeitwa de Slane mwaka 1868). Sehemu hii ni jambo la kihistoria lenye kudumu ambalo pia limempatia mwandishi, heshima na umaarufu duniani. Humo kuna kumbukumbu ya mambo ya kihistoria, juu ya aina mbalimbali za ustaarabu duniani uliotokana na athari za mazingira na hali ya hewa tofauti, maisha ya makazi ya kibedui (ya kuhamahama) na ya kudumu pamoja na tamaduni tofauti tofauti za jamii hizo na pia taasisi tofauti za kijamii, sayansi na sanaa zao. Mwandishi pia anaongelea masuala ya sayansi, hesabu, muziki na ala zake, kilimo na sanaa kwa mujibu wa Qur’an. Kwa kweli, ni kazi yenye maelezo kuhusu mambo mengi na yaliyoelezwa kifasaha ambapo historia yenyewe imeelezewa kuwa ni sehemu ya somo la Falsafa kwa maneno yafuatayo: "Hebu tutazame undani wa somo la Historia", anasema Ibn Khaldun kwamba, ni uchunguzi na uthibitisho wa taarifa, uchunguzi makini wa sababu za kuwepo kwa mambo (kama yalivyo) na uerevu wa kina wa jinsi mambo yalivyoweza kutokea. Hivyo, Historia ni mojawapo ya sehemu za somo la Falsafa, na inapaswa kutambuliwa kama mojawapo ya elimu ya sayansi." Hii kwa kweli ndiyo dhana ya kileo juu ya somo la Historia, kutokana na kuuona umuhimu na nafasi yake katika uchambuzi wa taarifa mbalimbali na kutafuta chanzo au sababu za mambo. Historia inapaswa kuwa ni elimu ya kudumu katika ustaarabu wa mwanadamu na saikolojia yake.

Ni vigumu kuweza kuchambua kwa kina kazi kubwa aliyoifanya Ibn Khaldun. Uchunguzi wake adilifu juu ya upoteaji na uharibifu wa staarabu mbalimbali, katika mzunguko, na mchango mkuu wa wasomi katika uundaji wa Mataifa mbalimbali, ambao amewanukuu katika jitihada za kuhami dhana yake, ni mambo yenye kuvutia. Ibn Khaldun alipindukia pale alipoainisha maisha ya Taifa lolote na ya watu au ya kiumbe kingine chochote, kwamba hata mataifa yanazaliwa, yanakua na yanakufa. Pia kwamba mataifa yako chini ya kanuni ya mabadiliko asilia. Ibn Khaldun amehusika na uvumbuzi wa kanuni hii ya mabadiliko ya taifa lolote.

Mawazo yake ya kiuchumi kama ya kisiasa, yameendelea kutumika hata leo. Mwandishi huyu kutoka iliyokuwa ikiitwa Maghreb (Morocco) anasema: "Taifa ni sawa na mfanyabiashara mkubwa, kwani ana jukumu la kuhakikisha kuwa pesa azipatazo kutokana na kodi, zinarudi na kuwazungukia watu. Kodi za wastani ni motisha tosha ili watu waweze kujituma katika kufanya kazi. Kwa upande mwingine, kupandisha kodi yoyote tena kiholela holela, kunaweza kusababisha yasipatikane mafanikio ya malengo ya kodi husika." Anachunguza kwa makini sana masuala ya utaifishaji au ushikiliaji wa mali za watu, ukiritimba, usimamizi na udhibiti wa biashara kabla ya kuhitimisha kwa kusema kwamba rasilimali za Taifa, misingi yake mikuu ni watu, ari ya makampuni yake ya kibiashara na tija katika ufanyaji wa shughuli zote za kiuchumi.

Kujiingiza kwa serikali katika utendaji wa shughuli za kiuchumi hupunguza uwezo wa uzalishaji na utumiaji wa rasilimali za Taifa na hivyo huchelewesha upatikanaji wa maendeleo katika jamii. Ukweli ni kwamba, taaluma ya siku hizi katika dhana ya uchumi huria haikuongeza lolote katika mtizamo kama huu, ambao ulishajengeka tangu karne ya 15.

Msomi mwingine ni yule aliyeitwa Abul FazL aliyeishi kati ya miaka ya 1551 na 1602. Huyu alikuwa mwanafalsafa, msomi, mwanasiasa na rafiki mkubwa wa Mfalme msomi pia, Mogul wa India. Kazi yake iitwayo "Akbar Nameh", bila shaka ni miongoni mwa kazi muhimu za Kiislam kutoka bara Hindi. Kazi hii imegawanyika katika sehemu tatu. Ya kwanza inaongelea historia ya uvamizi wa Timur (Tamburlaine) wa nchi ya India, na pia ile ya mtoto wa Mfalme Timuridh aliyeitawala nchi hiyo. Sehemu ya pili inaelezea utawala wa muda mrefu na wa mafanikio wa Akbar, na sehemu ya tatu, inayoitwa Ayn I Akbari, inatoa taarifa muhimu juu ya shughuli za taasisi za serikali, sheria na utawala, juu ya hali ya maisha ya Wahindi na dini zao, falsafa na sheria kwa jumla. Baadhi ya sura zinaelezea juu ya sanaa na ufundi wa Wahindi, vyanzo vya pesa za kuendeshea serikali, takwimu na taarifa za kiutawala na maendeleo yaliyofikiwa katika utengenezaji wa silaha mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya majeshi na pia vitabu vilivyokuwa vimekwishatafsiriwa.

Ayn I Akbari pia ndani yake kina kiasi kikubwa cha maneno ya Hekima, maamuzi ya busara na nukuu mbalimbali za kisiasa za Akbar, ambazo Waziri wake Mkuu na rafiki yake wa karibu alizokuwa akiziandika kila siku.

"Hiyo ni kazi ya ajabu kabisa", anasema Carra de Vaux, "iliyojaa uhai, mawazo na mafunzo, ambamo kila kipengele cha maisha kimechunguzwa, kuorodheshwa na kupangiliwa, ambamo mlolongo wa maendeleo ya mambo mbalimbali hufurahisha macho ya msomaji wake, ni hati ambayo Ulimwengu wa Mashariki umeweza kujivunia. Watu ambao vipaji vyao vimeongelewa katika kitabu hiki, walishapiga hatua za mbele zaidi kuliko hali ya zama walizoishi, wazo katika masuala ya uundaji na uendeshaji wa serikali, na pengine katika udodosi wao katika Falsafa ya Dini. Wale washairi na wanafalsafa, huelewa vyema namna ya kushughulikia mambo ya kidunia. Huchunguza, hupanga, hupima na kukadiria, kisha hutekeleza. Mawazo yote ambayo huwajia hujaribiwa dhidi ya ushahidi uliopo. Kutoka Magharibi tumshukuru Leibnitz, kwa kutuonyesha matumizi ya takwimu, ambazo tunaziona kama ni somo jipya la sayansi, na msaada unaoweza kutolewa na somo lenyewe (la takwimu). Serikali ya Akbar iliweza kuzitumia takwimu kwa makini kabisa katika utawala wake, miaka zaidi ya mia tatu iliyopita, pamoja na kanuni za ustahimilivu kisiasa, utendaji wa Haki na kuthamini heshima na utu wa mwanadamu."

Usanifu wa Majengo na Sanaa za Plastiki

Kukua kwa sanaa ya Kiislam ni mojawapo ya maendeleo yaliyopatikana kwa haraka katika historia ya Ulimwengu. Mwanzoni mwa Hijria, Sanaa rasmi ya Kiislam haikuwapo. Ilianzishwa baada ya Waislamu kuunganisha aina ya mitindo waliyoikuta katika nchi walizoziteka za Mashariki mwa bahari ya Kati. Baada ya kuimarika sanaa hii, upesi sana ilienezwa katika Himaya yote ya Makhalifa. Kanuni ya sanaa hii mpya iliboreshwa zaidi na watu waliokuwa katika jumuia ya Kiislam, kutokana na ubunifu wao asilia, nje ya ushawishi wa watawala hao wapya.

Hivyo, kumbukumbu ya mafanikio ya Cairo au ya Cordova, ni rahisi kuchanganywa na ile ya mafanikio ya Samarkand au Delhi. Mlingano makini wa mipango, uhuru wa kusanifu majengo wa hapo Aleppo na Damascus ni tofauti na ndoto za anasa zilizozikumba kasri za Granada na Seville.

Fikra za kiakili za watu wa jangwani ziliishia katika kubuni vipimo maalum vya mistari ya jiometria, uchoraji kwenye vigae na enameli za kupambia kuta za majengo, kama ilivyotokea hapo Ispahan, mambo ambayo yamekuwa vielelezo vya tafsiri ya ndoto za wasanii wa Iran.

Lakini tofauti hizi hazikuathiri umoja wa Kiislam. Fahari za Kiislam huonekana dhahiri. Umoja huu unatokana na umoja wa kiimani au kiroho katika jamii ya Kiislam na hasa kutokana na mafundisho ya Qur’an. Ni Dini hii iliyowapa wasanii wa Kiislam himizo la kiroho na kuwajengea tabia ya kufikiri au kutumia vyema akili kama tunavyofahamu. Matumizi ya fikra yanajionyesha hasa pale tunapoona ubunifu wao katika sanaa za Kiislam kwa sababu zimebaki kumbukumbu chache ambazo hazikutokana na mafundisho ya dini hii. Kwa bahati mbaya, halikusalia jengo lolote la kale hapo Baghdad, lakini yanapatikana maelezo mengi ya kihistoria kuhusu jiji lililokuwa limejengwa wakati wa utawala wa ukoo wa Abbassid kwamba lilitia fora kwa uzuri.

Uharibifu uliofanywa na Mtawala wa Kimongolia aliyeitwa Halagu katika mwaka 1258, uliuteketeza kabisa mji wa Baghdad enzi hizo, kiasi kwamba leo hawezi mtu kuonyesha hata ilipokuwa imejengwa Ikulu. Ni kutokana na maelezo ya kihistoria tu juu ya kazi za usanii zilizokuwepo kwa wakati huo, kama tunavyosimuliwa katika Alfu Lela U Lela (au Siku Elfu na Moja). Huenda maelezo hayo yangeonekana kuwa si ya kweli kama tusingekuwa na kumbukumbu ya majengo ya Alhambra na Alkazar ya hapo mjini Serville.Na bado hata Alhambra ambayo mpaka leo ni kivutio cha macho (utalii), kwa fikra na maelezo tu bila shaka haiwezi kulinganishwa na kasri au Ikulu nyingine ambazo zimesahaulika kabisa, ingawa bado tuna kumbukumbu ya maelezo yake tu. Mifano inapatikana katika Hispania yenyewe. Kuna jengo lililoitwa Madinat Az Zahar, ambaloAbdur Rahman An Nasir alilijenga kwa heshima ya mke wake alieitwa Zahra.

Sanaa Tukufu zaidi ya Waislam ni usanifu na ujenzi wa Misikiti. Huu ni ushahidi tosha wa aina ya usanifu bora wa majengo ya zamani yaliyoupa sifa Uislam. Sanaa hii pia ilileta ushawishi katika ujenzi wa Makanisa na boma za wakubwa na watawala wa enzi hizo. Hispania, zama hizo iliiga tena bila ya kinyongo aina ya Sanaa iliyopatika hapo Andalusia, wakati ilipokuwa bado chini ya utawala wa moja kwa moja wa Waislamuu. Pia, ushawishi wa sanaa hiyo ulijionyesha katika sanaa ya Wataliano kutokana na ukaaji wa Waislamu hapo njini Sicily. Aina hii ya sanaa iliingia pia nchini Ufaransa kupitia sehemu iliyoitwaSeptimania. Maelezo ya Emile Male, mtaalam wa historia ya somo hili la sanaa ya ujenzi, yanaonyesha umuhimu wa sanaa hii ya Kiislam.

Male ametoa mwanga juu ya ulingano kati ya usanifu wa Kiislam na ule wa Kirumi. Kuna baadhi ya maumbo yenye nakshi za Kiislam katika fani ya ujenzi, kwa mfano mihimili ya pembe tatu, na milango ya mfano wa maua yaliyochanua na mengineyo. Bado majengo hayo tunayaona hapo Auvergne, Notre Dame du Port na Clermont. Mpangilio wa nakshi za Kiislam bado unaweza kuonekana katika Makanisa mengi ya hapo Auvergne.

Usanifu na nakshi zilizoipamba Misikiti ni jambo ambalo pia limeigwa katika ujenzi wa majumba mengi hapo Cordova na Notre du Puy. "Si kwa bahati tu, kwamba usanifu kama huo kuonekana pia katika jengo la Cathedral hapo Puy. Asili ya usanifu huu wa watu wa Mashariki ni katika utamaduni wa Kiarabu katika kuyaremba milango ya majengo yao."

Katika maelezo ya jumla, tulipata fursa ya kutaja ushawishi wa Uislam katika maendeleo ya sanaa ya viwandani. Bidhaa adimu na vya anasa vilivyotengenezwa kutokana na ubunifu wa wasanii wa Kiislam, viliwashangaza sana watu wa Ulimwengu wa Magharibi. Bidhaa hizi bado zimewekwa na kuhifadhiwa kama vito vya hazina kubwa katika majumba ya Wafalme na Makanisa mbalimbali.

Mchango wa Uislam haukuwa kwenye maendeleo ya ubunifu wa bidhaa za viwandani tu. Angalia jinsi F. Diez, katika matokeo ya utafiti wake juu ya sanaa ya Kiislam, anavyoelezea ushawishi uliotokana na maumbo yaliyotokana na sanaa ya uchongaji wa Seldjuk ulivyochukuliwa na kuigwa na watu wa Ulaya, pale alipoandika: "Umuhimu wa sanaa hii ya uchongaji wa vitu vya kawaida kama vionekanavyo katika mazingira ya mwanadamu, unatokana na tabia na uwezo wake katika kujiingiza katika sanaa ya Wazungu hasa wa Ulaya ya Kaskazini. Maelezo juu ya aina hii ya mapambo iliyoshamiri katika zama zakarne za Kati, yanapatikana katika historia ya mabadiliko ya mwelekeo wa misafara ya kibiashara kutoka kusini kuelekea Kaskazini, uliotokana na uhamiaji wa Waturuki kuelekea katika nchi za Magharibi. Mojawapo ya misafara hiyo ya kibiashara ni ule uliotoka Asia ndogo kuelekea Kaskazini, aidha kwa kuzungukia Urals au kwa kukatiza, halafu kupitia Ujerumani ya Mashariki, na Bahari ya Baltic hadi katika kisiwa cha Uingereza. Miji ya kibiashara kama Hamburg, Lubeck, Riga na Novgorod ilianza kujengeka kuanzia sehemu ya pili ya karne ya 12. Vladmir na Sudal, iliyoko mashariki mwa Moscow ni miji iliyovuma sana kuliko hata Kiev katika umaarufu. Maumbo ya milango ya Makanisa ya zamani katika miji hii miwili bado ni ushahidi tosha hadi leo wa jinsi gani sanaa ya Kiislam ilivyoweza kujipenyeza Ulaya."

Hebu tujikumbushe jukumu moja kubwa la Sanaa ya Kiislam katika maendeleo ya msamiati na taaluma ya utengenezaji na utumiaji wa Nembo (helaldry).

Mti wa Uzima, alama au nembo yenye siri kubwa kwa watu wa Mashariki, mchoro uonyeshao wanyama walioelekeana, pia sanaa hii imeweza kukutwa imechongwa katika milango ya Makanisa mbalimbali kama ya watakatifu Etienne de Beauvais, Brice de Chartres, Notre Dame de la Couture, Le Mans na mengine mengi tu. Nembo hii pia ilichorwa katika vitambaa, vifaa vilivyochongwa na kwenye makaratasi na nyaraka za kuandikia. Katika Biblia ya Charles the Bald, wameonyeshwa simba katika sehemu mbili za mti huu wa kiroho, na katika Injili ya Lothair, wamewekwa chui, yote yakithibitisha zaidi asili ya sanaa ya Waislam kama ilivyopokelewa tena kwa shauku na watu wa Magharibi. Na mahali pengine wamewekwa wanyama bila ya kuwekwa mti huu unaoitwa wa Uzima: kama La Trinite ya hapo Caen, St. Germain de Pre la mjini Paris na kwingineko. Michoro ionyeshayo kundi la wanyama wanaotafunana, na ya aina ya wanyama watokanao na fasihi simulizi za kale kama mnyama mwenye mwili na kichwa cha simba na mbawa za tai, au ndege mwenye kichwa cha binadamu, au tai mwenye vichwa viwili, wametokana na sanaa ya Kiislam.

Hizi zote ni Sanaa zilizotokana na ubunifu na dhamira binafsi za wasanii na hivyo ni rahisi hata kuzitambua. Lakini Sanaa ya Kiislam, kwa kawaida ni ya kutumia mkusanyiko wa mistari. Hivyo, inakuwa vigumu wakati mwingine kuamua kama nyingine zilichukuliwa na Wazungu baada ya kuzifanyia marekebisho au la. Unakili wa Sanaa hiyo lazima ulitokea kwani mtu atakuta kwamba katika uhandisi-ujenzi wa Kirumi kuna uchongaji wa herufi za Kiarabu kiasi ambacho zingine zinaweza hata kusomeka kwa wenye kujua kuzisoma. Mifano inapatikana hapo Voute Chillac, Haute Loire, Toulouse na St. Guillaume la Desert na katika jumba la Makumbusho la mjini Lyons, Ufaransa.

Katika miIango ya Cathedral hapo Puy kumechongwa herufi za Kiarabu zinazosomekaMaa’Sha Allah (yaani Kwa Mapenzi ya Mungu). Na pia katika jumba la Makumbusho mjini London, kuna Msalaba uliohifadhiwa tangu karne ya 9 ambao katikati yake kumechongwa maneno ya Kiarabu yasomekayo: Bism Llah (yaani kwa Jina La Mwenyezi Mungu), na pia katika milango ya Mt. Peter kwenye Cathedral moja mjini Milan, ambayo alikabidhiwa Papa Eugene wa IV, kumechongwa herufi za Kiarabu kuzunguka kichwa chote cha sanamu la Yesu, na katika kanzu za sanamu za Mt. Peter na Paul. 

Mchango katika Somo la Muziki

Katika imani sahihi ya Kiislam, muziki ni jambo ambalo halikupendelewa. Mfumo mzima wa ibada na sala katika Uislam umeepukana na matumizi ya nyimbo. Mtazamo wa walimu wengi wa dini na hata waanzilishi wa madhehebu kuu nne za Kiislam walipinga matumizi ya nyimbo na miziki katika ibada. Ni katika amri za kushangaza zilzoitwa Law lewi(zilizojulikana Ulaya kama Amri za Whirling Dervishes, Derkawa huko Afrika Kaskazini), na nyigine za Kisufi zilizoupa umuhimu muziki na nyimbo.

Uimbaji wa tenzi na michezo ya ngoma kwa kutumia Ala za muziki zimehusishwa sana katika kufundishia hasa watoto masomo ya dini. Wasufi waliamini kwamba katika muziki kuna mwangwi wa kudumu wa mambo yasioonekana. Walikusudia kuutumia muziki katika kuitafakari Akhera.
Walimu wa dini na madaktari wa sheria walihofia nguvu ya muziki katika kuutikisa moyo wa mwanandamu na hata kuweza kumletea usumbufu na hatimaye kumpotezea katika mambo ya kidunia na kumsahaulisha jukumu la kujitayarishia Akhera.

Pamoja na hadhari hii, hilo halikuweza kuzuia maendeleo katika fani hii ya muziki katika jamii ya Kiislam. Tangu mwanzo wa Himaya ya Kiislam, muziki ulipewa nafasi kubwa katika Kitala (boma) cha utawala wa Umeyyad mjini Damascus na cha utawala wa Abbassid mjini Baghdad. Khalif Harun AL-Rashid na warithi wake waliupa muziki nafasi muhimu kama ilivyokuwa katika sayansi na sanaa nyingine.

Kuanzia Mashariki, muziki uliingia Spain kupitia Morocco. Kwa maelezo ya Averroes (Ibn Rushd), ni katika Seville ambapo muziki ulipata kuendelezwa na kukuzwa kwa nguvu zaid. Wanafalsafa walijadili umuhimu wa muziki, athari za sauti katika roho ya mwanadamu, na nguvu zake katika kuwasilisha ujumbe au hisia. Historia imetukarimu kwa kutuhifadhia kumbukumbu ya majina ya wanamuziki na waimbaji maarufu. Hapa tutawataja tu Abul Hassan Ali Ibn Nafis, aliyeitwa pia Ziriyab, ambaye alianzia shughuli zake hapo Baghdad na kujiendeleza hadi kuzoeleka katika Kitala cha Abd Ur – Rahman wa II mjini Cordova.

" Katika muziki", anasema Levi – Provencal, "alionyesha kuwa mtu mbunifu na mwenye kipaji cha hali ya juu. Alijenga kisima cha muziki wa Andalusia, ambacho mwanzoni kilifanana na kile cha Chuo cha Elimu ya Mashariki, ambayo baadaye iliendelezwa na Waislam katika nchi za Magharibi."
Na katika maendeleo ya nadharia, miongoni mwa waandishi wa Kiislam kushughulikia taaluma ya muziki alikuwa si mwingine bali mwanafalsafa aliyeitwa AL- Farabi. Kwake tunajivunia kitabu chake kiitwacho Kitab Al- Musiki (Kitabu cha Muziki). Mtunzi, ambaye shauku yake katika muziki ilianzia katika masomo ya Hesabu na Fizikia, alipoweza kuwa mtu wa kwanza kutoa maelezo ya kina juu ya utoaji wa sauti na utengenezaji wa kanuni za utayarishaji wa Ala za Muziki.

Wakianzia kwenye mizania ya Wachina na Wa-Iran, Waislamu walitafiti na kuweza kutengeneza mizania asilia na kupata mafanikio makubwa katika mbinu za utengenezaji wa Ala za Muziki kama magitaa, zumari, ngoma, dufu n.k Pia walitengeneza aina ya kwanza ya piano na kinanda. Ala zote hizi ziliingizwa kwa mara ya kwanza huko Iberia na kisha Ulaya na Waislam wenyewe.

No comments:

Post a Comment

Qur'an 5:32