Qur'an Ni Ya Ajabu


Qur'an Ni Ya Ajabu

Gary Miller

Qur'an kuipa jina la 'Kitabu cha Ajabu' sio jambo lililofanywa na Waislamu pekee, ambao wanaitambua na kuifurahia; bali pia imepewa jina hilo na Wasio Waislamu. Kwa kweli,  hata wale wanaouchukia Uislamu kupita kiasi wameendelea kuipa sifa hiyo ya kuwa Qur'an ni ya Ajabu.

Kitu kinachowashangaza wasio Waislamu wanaokichunguza kitabu hiki kwa ukaribu sana ni kwamba, Qur'an inajitokeza mbele ya macho yao  kuwa katika hali ambayo hawakuitarajia. Wanachofikiri ni kwamba wana kitabu cha kale kilichotokea karne kumi na nne zilizopita kutoka katika jangwa la Arabia; na walitarajia kitabu hicho kionekane kama kitabu cha kale kutoka jangwani. Na kisha wanagundua kwamba hakifanani hata kidogo na vile walivyotegemea. Aidha, miongoni mwa vitu vya awali ambavyo baadhi ya watu wanavifikiria ni kwamba, kwa kuwa ni kitabu cha kale kilichokuja kutoka jangwani, kilipaswa kuzungumzia mambo ya jangwani. Ndiyo, Qur’an imezungumzia kuhusu jangwa   baadhi ya tamathali zake zinaelezea jangwa; lakini pia inazungumzia bahari    kuhusu kuwa kwenye bahari yenye dhoruba. 

Miaka kadhaa iliyopita, kuna kisa kilitufikia kutoka Toronto kikimhusu mmoja aliyekuwa akisafiri ndani ya meli ya biashara na kukaa muda mrefu baharini na kuwa na uzoefu mkubwa wa mambo ya bahari. Mwislamu mmoja alimpatia Qur’an yenye tafsiri ili apate kuisoma. Mfanyabiashara huyo hakuwa akijua chochote kuhusu historia ya Uislamu lakini alivutika kuisoma Qur’an. Alipomaliza kuisoma alimrejeshea Mwislamu kitabu hicho na kumuuliza: “Je, Muhammad alikuwa baharia?” alikuwa amevutiwa na jinsi Qur’an ilivyoielezea bahari yenye dhoruba kwa umakini mkubwa  (hali ya dhoruba kwenye bahari). Alipoambiwa kuwa “Hakika Muhammad aliishi jangwani”, jawabu hilo lilimtosheleza kabisa. Alisilimu hapo hapo. Alivutiwa na maelezo hayo ya Qur’an kwa sababu amekuwa katika bahari yenye dhoruba, na alijua kwamba yeyote yule aliyekuwa ameandika maelezo hayo naye angekuwa ameishi kwenye bahari nyenye dhoruba. Maelezo yasemayo “mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yakiwepo mawingu” sio maelezo ya mtu asiyejua jinsi dhoruba ya bahari inavyokuwa, bali ni maelezeo ya mtu aijuaye vema hali halisi ya dhoruba inavyokuwa. Huu ni mfano mmoja tu wa jinsi ambavyo Qur’an haikujifunga kwenye sehemu moja na muda mmoja tu. Kwa hakika, mawazo na nadharia za kisayansi zilizoelezwa ndani ya Qur’an Tukufu hayaonekani kuwa yalitoka jangwani karne kumi na nne zilizopita. 

Kwa karne nyingi kabla ya utume wa Muhammad, palikuwepo na nadharia maarufu ya kitu kiitwacho atom (kitu kidogo mno au chembe) iliyoendelezwa na mwanafalsafa wa Kigiriki, Democritus. Mwanafalsafa huyo pamoja na wale waliokuja baada yake walikuwa na fikra kwamba maada (matter) ni muungano wa chembe chembe ndogo mno, zisizoweza kuharibiwa, zisizochanguka au kugawanyika ziitwazo atomu. Waarabu nao pia walikuwa na fikra hiyo hiyo, ambapo neno la Kiarabu liitwalo “dharrah” kwa kawaida lilitumika kumaanisha kitu kidogo zaidi kuliko kitu chochote kile. Leo hii, sayansi mpya imegundua
kuwa maada hii ndogo kuliko maada zote (yaani, “atom” yenye sifa sawa na “element” yake) inaweza kugawanywa katika vipande vidogo vidogo zaidi. Hili ni wazo au nadharia mpya iliyoibuliwa karne iliyopita, lakini kitu kinachovutia ni kwamba, ilikuwa imeshathibitishwa na Qur’an Tukufu inayoeleza: 

“Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe (dharrah)  katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho...”

Bila shaka, lau kama maelezo hayo yangetolewa katika zama hizo za karne kumi na nne zilizopita, yangeonekana kuwa ya ajabu hata kwa Mwarabu mwenyewe. Kwani kwake yeye, „dharrah‟ ndicho kilichokuwa kitu kidogo zaidi kuliko vitu vyote. Kwa hakika, huu ni uthibitisho kuwa Qur’an Tukufu haijapitwa na wakati. 


Mfano mwingine wa kitu ambacho mtu angetegemea kukikuta katika “kitabu cha zamani” kinachozungumzia maudhui ya afya na tiba ni dawa na tiba zilizopitwa na wakati. Wanahistoria mbalimbali wanaeleza kuwa Mtume (s.a.w.) alitoa ushauri kadhaa kuhusu afya na usafi, lakini ushauri huu haukujumuishwa ndani ya Qur’an Tukufu. Kwa mara ya kwanza, wale wasiokuwa Waislamu wanaweza kuona suala hili la kutojumuisha ushauri huo wa Mtume ndani ya Qur’an  kuwa ni uzembe mkubwa. Hawawezi kujua kwa nini Mwenyezi Mungu “hakujumuisha” taarifa hizo, muhimu na zenye manufaa, ndani ya Qur’an Tukufu. Baadhi ya Waislamu wanajaribu kufafanua jambo hili kwa hoja ifuatayo: “Ingawa ushauri na maelekezo ya Mtume vilikuwa sahihi na vyenye manufaa kwa zama alizoishi, Mwenyezi Mungu kwa Hekima Yake isiyo na kikomo, alijua kwamba baadaye yangekuja maendeleo ya tiba na sayansi ambayo yangeufanya ushauri wa Mtume uonekane kuwa uliopitwa na wakati. Pindi ambapo ugunduzi mbalimbali ungetokea, watu wangesema kwamba taarifa za ugunduzi huo zinapingana na zile zilizotolewa na Mtume. Hivyo basi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu asingeruhusu kuwepo na mwanya wowote kwa wasiokuwa Waislamu kudai kwamba Qur’an inajipinga yenyewe au ni mafundisho ya Mtume, ndio maana ndani ya Qur’an akaweka taarifa na mifano ambayo ingeweza kufaulu mitihani na majaribio ya kila aina ya wakati au zama”.  

Hata hivyo, tukichunguza ukweli hasa wa Qur’an katika namna ya kwamba ni ufunuo wa Mwenyezi Mungu, suala zima laweza kupata kuchambuliwa haraka na kwa njia sahihi, na makosa yaliyopo katika hoja hiyo hubainika na kueleweka. Lazima ieleweke kuwa Qur’an ni ufunuo wa Mwenyezi Mungu, na kwa hiyo, habari zote zilizomo ndani yake zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Allah aliiteremsha Qur’an kutoka kwake Mwenyewe. Quir‟an ni neno la Mwenyezi Mungu lililokuwepo kabla ya kuumbwa kwa kitu chochote, na kwa maana hiyo hakuna kinachoweza kuongezwa, kupunguzwa au kuondolewa. Kimsingi, Qur’an ilikuwepo na ilikuwa kamili kabla ya kuumbwa kwa Mtume Muhammad, na hivyo isingewezekana kuwa na neno au ushauri wowote wa Mtume mwenyewe. Ujumuishaji wa habari hizo ungepingana, kwa uwazi kabisa, na malengo ya kuwepo kwa Qur’an, kuhatarisha mamlaka yake na kuitoa katika usahihi wake kama ufunuo wa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo, ndani ya Qur'an hakuna “tiba za ndani/nyumbani” (home remedies) ambazo mtu angeweza kudai kuwa zimepitwa na wakati; wala ndani yake hakuna maoni ya mwanadamu kuhusu kitu chenye manufaa kwa afya, chakula kinachopaswa kuliwa, au dawa inayoweza
kuponya ugonjwa huu au ule. Qur'an Tukufu inataja kitu kimoja tu kinachohusika na matibabu, na kitu hicho hakipingwi na yeyote. Inaeleza kuwa kuna ponyo ndani ya asali. Na bila shaka, sidhani kuwa kuna mtu atakayebisha ukweli huo! 

Kama mtu atakuwa na fikra ya kwamba Qu'an ni zao la akili ya mwanadamu, basi mtu huyo atategemea kitabu kiakisi baadhi ya mambo yaliyokuwa yakiendelea katika akili ya mwanadamu huyo “aliyeitunga” (composed). Baadhi ya ensaiklopidia na vitabu kadhaa vinadai kwamba Qur'an ni zao la “maradhi ya kuona kisichokuwepo/ kusikia sauti zisizokuwepo” (hallucinations) yaliyokuwa yamemkumba Muhammad. Kama madai haya ni ya kweli iwapo kweli ilitokana na matatizo ya kisaikolojia katika akili ya Muhammad  basi ushahidi wa madai hayo ungeonekana wazi ndani ya Qur'an. Lakini je, ushahidi huo upo?  Ili kuchunguza kama yapo au hayapo, yatakiwa kwanza kuainisha kile ambacho kingekuwa kikiendelea katika akili yake wakati huo na kisha kuzichunguza fikra na mawazo hayo ndani ya Qur'an. 

Inafahamika na kila mtu kwamba Muhammad aliishi maisha ya shida sana. Mabinti zake walifariki kabla yake isipokuwa mmoja tu, na alikuwa na mke mwenye umri mkubwa aliyekuwa mpendwa wake na muhimu kwake, na ambaye  alimtangulia kufariki dunia wakati Muhammad akiwa katika kipindi muhimu sana cha maisha yake. Kusema kweli alikuwa mwanamke wa kipekee, kwa sababu ufunuo wa mwanzo ulipomfikia Mtume alikimbilia kwa mkewe huyo akiwa ni mwenye hofu kubwa. Bila shaka, hata leo hii utakuwa na wakati mgumu ukijaribu kumtafuta Mwarabu atakayekwambia, “Nilikuwa na hofu kubwa nikakimbilia nyumbani kwa mke wangu”.

Hawako hivyo. Lakini Muhammad alijisikia mwenye utulivu na kuliwazika kwa mke wake kwa kiasi cha kuweza kufanya hivyo. Hivyo ndivyo mwanamke huyo alivyokuwa mhimili na nguzo imara kwake. Ingawa mifano hiyo ni michache kuhusu maudhui ya mambo ambayo yangekuwa katika akili ya Muhammad, inatosha sana kuthibitisha hoja yangu. Pamoja na umuhimu wa mambo hayo kwa Muhammad Qur’an haitaji hata jambo moja katika  hayo  haitaji kifo cha wanawe, wala kifo cha mkewe mpendwa, wala hofu aliyokuwa nayo mwanzoni mwa kupewa ufunuo, ambayo alimshirikisha mkewe  haikutaja chochote; kama vitu hivyo vitakuwa vimemuumiza, kumchukiza, na kumsababishia maumivu na msongo wakati wa matatizo ya wasiwasi wa kisaikolojia, basi vitu hivyo vingeonekana wazi au angalau hata kutajwa kila mahali ndani ya Qur’an. 

Mtazamo halisi wa kisayansi juu ya Qur’an unawezekana, kwa sababu Qur’an imekuja na kitu ambacho hakijapokelewa katika maandiko mengine ya kidini, na hakijaletwa pia na dini nyingine kwa ujumla. Ni kitu kinachohitajiwa na wanasayansi. Leo hii kuna watu wengi wenye mawazo na nadharia kuhusu ulimwengu unavyofanya kazi. Watu hawa wapo kila mahali, lakini jamii ya wanasayansi haisumbuki hata kuwasikiliza. Hii inatokana na sababu kwamba katika kipindi cha karne iliyopita jamii ya wanasayansi (scientific community) iliweka kipimo cha kupima/kuthibitisha ukweli au uwongo wa nadharia fulani (test of falsification). Wakasema, “kama una nadharia, usitusumbue nayo mpaka utapotuletea
nadharia hiyo na njia ya kutuwezesha kuipima kama inamakosa au la  (...unless you bring with that theory a way for us to prove whether you are wrong or not)”. 

Kipimo kama hicho ndio hasa kiliifanya jamii hiyo ya wanasayansi imsikilize Einstein kuelekea mwanzoni mwa karne hiyo. Yeye alikuja na nadharia mpya na kusema, “Ninaamini kuwa ulimwengu (universe) unafanya kazi hivi; na hapa kuna njia tatu za kuthibitisha kama mimi sipo sahihi! 

Hivyo, jamii hiyo ya wanasayansi waliipima nadharia hiyo kwa kutumia vipimo (tests), na ndani ya miaka sita jamii hiyo ilizipitisha njia zote tatu. Hata hivyo, hii haina maana kuwa alikuwa mtu mkubwa, bali yathibitisha kuwa alistahiki kusikilizwa kwa sababu alisema, “Hii ni nadharia yangu; na kama mnataka kujaribu kuthibitisha kama mimi ni muongo, fanyeni hivi au jaribuni vile”.

Hili ndilo hasa lililoletwa na Qur’an, vipimo vya kuthibitisha uwongo au ukweli wa kitu. Baadhi yake ni za kitambo (na hivyo zimeshathibitishwa kuwa ni za kweli), na baadhi bado zipo hadi leo. Kimsingi inasema, “Iwapo kitabu hiki ni kinyume na kinavyodai kuwa, basi mnachotakiwa kufanya ni hiki au hiki au hiki ili kuthibitisha kuwa ni uwongo”. 

Na sasa, katika kipindi cha miaka 1400 hakuna aliyeweza kufanya “Hili au hili au hili,” na hivyo mawazo hayo ya Qur’an yameendelea kuwa kweli na sahihi.

Ninakushauri kwamba ikitokea kubishana na mtu kuhusu Uislamu na akadai kuwa anao ukweli na kwamba wewe uko gizani, achana na hoja zote kwanza na mpe wazo hili.

Muulize:
“Je, katika dini yako kuna kipimo chochote cha kuthibitisha uwongo au ukweli wa jambo fulani?

Je, katika dini yako kuna chochote kinachoweza kuthibitisha kama upo kwenye makosa na iwapo nitaweza kuthibitisha uwepo wa makosa hayo?

Nakuahidi kuwa watu hao hawatokuwa nauthibitisho wowote, hawatokuwa na kipimo, kithibitisho wala chochote! Kwa sababu hawana mawazo kwamba hawatakiwi tu kuwasilisha kile wanachokiamini bali pia wanatakiwa kuwapa wengine nafasi ya kuthibitisha kama wako sahihi katika wanacho kiamini au la. Hata hivyo, Uislamu unatoa nafasi hiyo kwa watu kuthibitisha usahihi wa imani au uwongo wake. Mfano kamili wa namna Uislamu unavyompa mtu nafasi ya kuthibitisha usahihi au “kuthibitisha kuwa hauko sahihi”, mfano huo unapatikana katika Sura ya 4. Kwa kweli kabisa, nilishikwa na mshangao nilipoigundua changamoto hii kwa mara ya kwanza. Sura inasema: 

“Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kama ingekuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi.” 

Hii ni changamoto ya wazi kwa asiyekuwa Mwislamu. Kimsingi inamuita kutafuta kosa hata moja. Kiukweli, uzito na ugumu wa changamoto hii kwa upande mmoja, uwasilishaji hasa wa changamoto hiyo katika sehemu ya kwanza haipo hata katika maumbile ya mwanadamu na hailingani na jinsi mwanadamu alivyo. Mtu hafanyi mtihani shuleni baada ya kumaliza mtihani husika, mwisho akamuandikia mwalimu husika maelezo na kumtaarifu akisema:
Huu mtihani ni mkamilifu. Hakuna makosa hata kidogo. Tafuta kosa hata moja kama unaweza!
Hakuna afanyaye hivyo. Akifanya hivyo mwalimu hatolala mpaka alione kosa! Na sasa hivi ndivyo Qur’an inavyowaambia watu. Msimamo mwingine wa Qur’an unaovutia sana na unaojirudia rudia sana unahusu namna Qur’an inavyomshauri yule anayeisoma. Qur’an inamweleza msomaji kuhusu mambo tofauti tofauti kisha inampa ushauri:
Kama unataka kujua zaidi kuhusu kitu hiki au kile, au kama  una shaka na kinachosemwa, basi waulize wenye elimu na maarifa”. 

Huu ni msimamo unaoshangaza sana. Sio jambo la kawaida kabisa kuona kitabu kutoka kwa mtu ambaye hakusoma jiografia, botania, baiolojia, n.k., anayezungumzia masomo haya kisha akamshauri msomaji kuwauliza watu wenye elimu na maarifa kama atakuwa na shaka juu ya chochote. 

Katika kila zama wamekuwepo Waislamu ambao wamefuata ushauri wa Qur’an na wakafanya ugunduzi wa hali ya juu. Ukizitazama kazi au vitabu vya wanasayansi wa Kiisalmu wa karne kadhaa zilizopita, utavikuta vitabu hivyo vikiwa vimejaa nukuu kutoka ndani ya Qur’an Tukufu. Vitabu hivi vinatoa maelezo kuwa watu hao walifanya utafiti katika mahali fulani, wakitafuta kitu fulani. Na vinathibitisha kuwa sababu iliyowafanya watazame sehemu fulani na sehemu fulani ni kwa kuwa Qur’an iliwaonyesha kwenda upande fulani au uelekeo huo. Kwa mfano, Qur’an yaelezea asili ya mwanadamu na kumwambia msomaji, “Ifanyie utafiti!” Inampa msomaji dokezo au mahali pa kutazama na kisha inamueleza mtu huyo kwamba atafute zaidi kuhusu kitu hicho. Hiki ni kitu ambacho kwa kiasi kikubwa Waislamu wa leo hawakitilii maanani ingawa sio wote, kama inavyoonesha katika mfano ufuatao.

Miaka michache iliyopita, kundi la watu mjini Riyadh, Saudi Arabia walizikusanya aya zote za Qur’an zinazozungumzia embrolojia, maendeleo ya mwanadamu katika tumbo la uzazi. Wakasema: “Hivi ndivyo isemavyo Qur’an. Je, ni kweli?”

Wakachukua ushauri wa Qur’an:Waulizeni wanaojua”. Kama ilivyotokea, wakamteua Profesa asiyekuwa Mwislamu kutoka Chuo Kikuu cha Toronto (Kanada). Jina la Profesa huyo ni Keith Moore, naye ni mtunzi wa vitabu mbalimbali vinavyozungumzia embrolojia ni mtaalamu mashuhuri ulimwenguni katika somo hilo. Walimualika mjini Riadh na kumwambia, “Hivi ndivyo isemavyo Qur’an kuhusu somo lako. Je, ni kweli? Wasemaje?”

Alipokuwa Riyadh, walimpatia kila aina ya msaada aliouhitaji katika kutafsiri na kumpa ushirikiano wote aliouomba. Alishangazwa sana na kile alichokigundua kwa kiasi kwamba alivifanyia mabadiliko vitabu vyake. Katika toleo la pili la mojawapo ya vitabu vyake kiitwacho “Before we are born”, katika toleo la pili kuhusu historia ya emrolojia, aliongeza baadhi ya mambo ambayo hayakuwepo katika toleo la kwanza, kutokana na kile alichokigundua ndani ya Qur’an Tukufu. Kwa hakika jambo hili laonyesha kwamba Qur’an imeutangulia wakati na kwamba wale wanaoiamini Qur’an wanajua mambo ambayo watu wengine hawayajui. 

Nilipata bahati ya kufanya mahojiano kwa ajili ya kipindi cha televisheni na Dr. Keith Moore, na tulizungumzia sana kuhusu suala hili. Alitaja baadhi ya vitu vinavyoelezewa na Qur’an kuhusu ukuaji wa binadamu katika tumbo la uzazi ambavyo vimekuja kujulikana miaka michace tu iliyopita. Alisema kuwa kitu kimoja maelezo ya Qur’an juu ya mwanadamu kuwa “donge lenye muonekano wa luba” (leechlike clot = alaqah) katika hatua moja, lilikuwa ni jambo jipya kwake; lakini alipolitazama kwa utafiti alikuta kwamba ni kweli, na hivyo akakiongeza katika kitabu chake. Alisema, “Hapo kabla sikuwa na fikra kama hiyo”, akaenda kwenye idara ya zuolojia akaomba picha ya luba. Alipokuta kwamba ilifanana na kiinitete cha binadamu, aliamua kuzijumuisha picha zote mbili kwenye mojawapo ya vitabu vyake. Dr. Moore pia aliandika kitabu kuhusu uhalisia wa embrolojia
(clinical embryology), na pindi alipowasilisha habari hizi mjini Toronto, zilisababisha msukosuko ndani ya Kanada nzima. Iliandikwa katika kurasa za mbele za magazeti nchini kote Kanada, na baadhi ya vichwa vya habari vilikuwa ni vyenye kuchekesha. Kwa mfano kichwa kimoja cha habari kilisomeka:
Surprising Thing Found In Ancient Book!” (Kitu Cha Ajabu Chagunduliwa Ndani Ya Kitabu Cha Kale!).

Kutokana na mfano huu inaonekana wazi kuwa watu hawajui hasa kitu hicho ni kitu gani. Mwandishi wa gazeti moja alimuuliza Profesa Moore, “Hufikiri kuwa huenda Waarabu watakuwa wamevijua vitu hivi? Maelezo kuhusu kiinitete, muonekano wake kinavyobadilika na kukua? Huenda hapakuwepo na wanasayansi, lakini huenda watu hao walifanya uchunguzi wao kwa kupasua sehemu za mwili na kuzichunguza na kisha kugundua vitu hivi”.

Bila kuchelewa Profesa akamfahamisha kuwa yeye (yaani huyo mwandishi wa habari) alikuwa amekosa pointi ya msingi sana picha zote za kiinitete (embryo) ambazo zimekuwa zikiioneshwa zimetengenezwa kwa mkanda wa filamu kutoka kwenye picha zilizochukuliwa kupitia hadubini (microscope).

Akaendelea kusema: “Sio tatizo kama mtu alikuwa amejaribu kugundua embrolojia karne kumi na nne zilizopita, wasingeweza kuiona!

Maelezo yote yaliyomo ndani ya Qur’an kuhusu muonekano wa kiinitete yanahusu kitu kinapokuwa bado kidogo sana kwa kiasi cha kutoonekana kwa macho; hivyo inahitajika hadubini (microscope) kukiona. Kwa kuwa kifaa hicho hakina muda wa zaidi ya miaka mia mbili tangu kuwepo kwake, Dr. Moore akasema kwa dhihaka: “Labda karne kumi na nne zilizopita kuna mtu alikuwa na hadubini kwa njia ya siri na akafanya utafiti huu, bila kukosea mahali popote. Kisha kwa namna fulani akamfundisha Muhammad na kumshawishi aziweke habari hizi ndani ya kitabu chake. Kisha mtu huyo akakiharibu kifaa chake hicho (hadubini) na kukifanya kuwa siri daima. Je, kweli waamini hivyo? Kwa hakika hupaswi kuamini hivyo ila kama utaleta uthibitisho kwa sababu hiyo ni nadharia inayochekesha”. Alipoulizwa kuwa: “Unaielezeaje habari hii iliyomo ndani ya Qur’an?” Dr. Moore alijibu: “Habari hii itakuwa tu iliteremshwa na Mwenyezi Mungu”.

Ingawa mfano uliotajwa hapo juu wa mtu kutafuta taarifa zilizomo ndani ya Qur’an Tukufu imefanywa na kuhusishwa na asiyekuwa mwislamu, bado ni sahihi kwa sababu mtu huyo alikuwa miongoni mwa wale wenye maarifa katika mada na maudhui husika. Kama mtu asiye mtaalamu angedai kuwa kinachosemwa na Qur’an kuhusu embrolojia ni kweli, basi bila shaka hakuna mtu ambaye angetakiwa kuyakubali maneno yake. Hata hivyo, kwa sababu ya daraja, heshima na hadhi kubwa wanayopewa wasomi, basi kwa asili, mtu hukubali kwamba kama wanachuoni hao wamefanya utafiti na kufikia hitimisho la utafiti huo, hitimisho hilo litakuwa sahihi. Miongoni mwa walimu wenzi wa Profesa Moore, Bwana Marshall Johnson, anajishughulisha sana na masuala ya jiolojia katika Chuo Kikuu cha Toronto (Kanada).

Alivutiwa na ukweli kwamba maelezo ya Qur’an kuhusu embrolojia ni sahihi, na hivyo akawaomba Waislamu wakusanye maandiko yote ya Qur’an yanayozungumzia na kushughulikia utaalamu wake huo (wa Jiolojia). Kwa mara nyingine watu walishangazwa na
matokeo ya utafiti huo. Kwa kuwa kuna idadi kubwa ya maudhui zilizozungumziwa ndani ya Qur’an, kitahitajika kiwango kikubwa cha muda kuizungumzia sana kila maudhui. Kwa malengo ya mada hii inatosha kueleza kwamba Qur’an inayaweka wazi sana na kwa mukhtasari maelezo mbalimbali kuhusu mada mbalimbali huku ikimshauri msomaji kwa msisitizo kuthibitisha usahihi na ukweli wa maelezo hayo kwa kutumia utafiti uliofanywa na wasomi mbalimbali kuhusu mada husika. Na kama ilivyoonyeshwa na Qur’an, maelezo yake yamedhihirika kuwa sahihi na kweli bila shaka yoyote. 

 Ndani ya Qur’an kuna msimamo na maelezo ambayo hayapatikani mahali popote pengine. Inavutia sana pale Qur’an inapotoa taarifa fulani, ambapo mara zote humwambia msomaji, Hapo awali hukuwa ukilijua hili. Kwa kweli, hakuna maandiko yoyote mengine ya kidini yaliyopo sasa yanayotoa madai kama hayo. Vitabu na Maandiko mengine yote ya zamani ambayo watu wanayo, yanatoa taarifa nyingi tu, lakini mara zote hueleza mahali taarifa hizo zilipotoka. 

Kwa mfano, Biblia inazungumzia historia ya mambo ya kale, inaeleza kuwa mfalme huyu aliishi hapa, huyu alipigana vita fulani, mwingine alikuwa na watoto wengi, n.k. Lakini mara zote inasema kwamba kama unataka taarifa zaidi, basi watakiwa kusoma kitabu kile na kile kwa sababu hapo ndipo taarifa hizo zilipotoka. Kinyume na fikra hii, Qur’an Tukufu humpa msomaji habari fulani na kumweleza kuwa habari hii ni mpya. Hata hivyo, Qur’an imekuwa ikitoa ushauri wa kuifanyia utafiti habari iliyotolewa na kuthibitisha usahihi wake. Inavutia sana kwamba fikra hiyo kamwe haikuhojiwa na wasio Waislamu karne kumi na nne zilizopita. Kwa kweli, makafiri wa Makka walikuwa wakiwachukia sana Waislamu, lakini mara zote waliposikia ufunuo kama huo unaodai kuleta habari mpya;  hawakufungua vinywa vyao na kusema, “Habari hii sio mpya. Tunajua Muhammad alipoitoa habari hii. Habari hii tuliisoma shuleni, n.k.” 

Hawakuhoji usahihi wake kwa sababu ni kweli kuwa habari hizo kwao zilikuwa ni mpya!
Katika kwenda sambamba na ushauri wa Qur’an unaotaka watu waitafiti habari fulani (hata kama ni mpya), pindi Omar alipokuwa Khalifa, aliteua kikundi cha watu na kuwatuma kwenda kutafuta ukuta wa DhulQarnayn. Kabla ya kuteremka kwa Qur’an, Waarabu hawakuwa na taarifa yoyote ya ukuta huo, lakini kwa sababu Qur’an iliuelezea, waliweza kuugundua. Ukuta huo upo katika eneo liitwalo Durbend katika Umoja wa nchi za Kisovieti (Soviet Union). Hapa ni lazima kusisitiza kuwa Qur’an ni sahihi kuhusu mambo yote iliyoyazungumzia, lakini usahihi haumaanishi kwamba kitabu fulani kimeteremshwa na Mwenyezi Mungu. Bali usahihi ni miongoni mwa vigezo vya ufunuo wa Mwenyezi Mungu. 

Kwa mfano, kitabu cha simu ni sahihi, lakini haina maana kuwa kimeteremshwa na Mwenyezi Mungu. Suala la msingi hapa ni kwamba mtu anatakiwa kuweka uthibitisho wa chanzo cha taarifa za Qur’an. Msisitizo umewekwa kwa msomaji.Mtu hawezi tu kukanusha usahihi na ukweli wa Qur’an bila ushahidi na uthibitisho wa kutosha. Kama kweli akikuta kosa, ana haki ya kuiondolea sifa ya usahihi. Hili ndilo linalohamasishwa hasa na Qur’an. Siku moja mtu mmoja alinijia baada ya hotuba niliyoitoa Afrika ya Kusini. Alikuwa
amekasirishwa na kile nilichokisema, na hivyo akasema: “Nitakwenda nyumbani usiku huu na kutafuta makosa ndani ya Qur’an”. Bila kusita nikamwambia: “Hongera! Hilo ulilosema ni jambo la akili sana”. Kwa hakika, hivi ndivyo Waislamu wanavyotakiwa kushughulika na wale wenye shaka ya usahihi wa Qur’an, kwa sababu Qur’an yenyewe yatoa changamoto kama hiyo. Baada ya wao kuikubali changamoto hii na kugundua kwamba ni kweli, lazima wataiamini kwa sababu hawakuweza kuthibitisha uwongo wa yale iliyoyaeleza. Kwa msingi huo, watapata kuiheshimu Qur’an kwa sababu wao wenyewe ndio waliolazimika kuthibitisha usahihi wake. Jambo la msingi ambalo haliwezi kurudiwa kusemwa kuhusu usahihi na ukweli wa Qur’an ni kwamba hali ya mtu mwenyewe kutoweza kufafanua tukio fulani haihitaji yeye kukubali uwepo wa tukio hilo au ufafanuzi wa mtu mwengine kuhusu tukio husika.

Kwa maana kwamba, sababu tu ya mtu kutoweza kufafanua kitu fulani haimaanishi kwamba lazima akubali maelezo ya mtu mwengine. Hata hivyo, hatua ya mtu kuyakataa maelezo na ufafanuzi wa watu wengine humuongezea mzigo wa kutafuta jibu stahili. Nadharia hii ya jumla inahusika katika fikra na mambo mengi katika maisha, lakini inaendana kwa namna ya ajabu na changamoto zinazotolewa na Qur’an, kwani inatengeneza ugumu na uzito kwa yule asemaye, “Siiamini”. Pale tu anapokataa, bila ya kuchelewa huwa ana wajibu wa kutafuta ufafanuzi yeye mwenyewe kama atahisi kwamba majibu ya watu wengine hayajitoshelezi. Katika mojawapo ya aya za Qur’an, ambayo mara nyingi nimeona ikitafsiriwa vibaya katika lugha ya Kiingereza, Mwenyezi Mungu anamtaja mtu aliyeusikia ukweli aliofafanuliwa.

Inaeleza kwamba itabakia ni dhima yake mtu iwapo baada ya kusikia taarifa hiyo aliikubali  bila kuichunguza usahihi wa kile alichokisikia. Kwa maneno mengine, mtu anakuwa ni mwenye hatia kama atakisikia kitu na akakifuata wakati hajakitafiti na kukichunguza kama kina usahihi au la. Anatakiwa kuchambua taarifa zote na kuamua ni zipi ambazo ni takataka zitupwe na zipi yenye faida zihifadhiwe na kutumika katika siku za baadaye.

Mtu hatakiwi kuzizunguusha tu taarifa kichwani bila kujihakikishia ukweli wake. Inatakiwa kuwekwa katika orodha sahihi na kushughulika nayo kwa mtazamo sahihi. Kwa mfano, kama taarifa husika bado ipo katika mazingira ya makisio, basi atatakiwa kutambua iwapo ipo karibu na ukweli au ipo jirani na uwongo. Lakini iwapo mambo yote husika yamewasilishwa mbele yake, basi anatakiwa kuamua hasa kati ya machaguo haya mawili. Na kama hatokuwa chanya kuhusu ukweli na usahihi wa taarifa hiyo, bado analazimika kuchambua taarifa zote na kukiri kwamba hajui kwa uhakika. Ingawa nukta hii ya mwisho yaonekana kutokuwa na maana, kiukweli, inakuwa na faida pindi ufikapo katika hitimisho zuri hapo baadaye, jambo ambalo humlazimu mtu angalau kutambua, kufanya utafiti na kugundua ukweli. Hali hii ya kuwa na mazoea na taarifa hiyo humpa mtu huyo “kinga” pindi ugunduzi unapofanyika hapo baadaye na taarifa za ziada zikawasilishwa. Kitu cha msingi ni kwamba mtu huyakabili mambo na hawezi kuyakimbia kwa kutokuwa na uwezo na kuhisi kutofaidika.

Uhakika halisi wa ukweli wa Qur’an unaonekana wazi katika hali ya kujiamini sana iliyomo kwa wingi ndani yake; na kujiamini huku kunatoka katika maeneo mbalimbali ”kwa kutumia vibadala (alternatives).” Kimsingi, Qur’an inasema, Kitabu hiki kimeteremshwa na Mwenyezi Mungu; kama huliamini hilo, basi ukweli ni upi?” Kwa maneno mengine,
msomaji anapewa changamoto ya kuja na maelezo mengine. Hapa kuna kitabu kilichotengenezwa kwa karatasi na wino. Kilitoka wapi? Kinasema kwamba kiliteremshwa na Mwneyezi Mungu; kama sio, sasa nini chanzo chake? Jambo la kuvutia ni kwamba hakuna mwenye maelezo yanayokubalika.

Kwa kweli, vibadala (alternatives) vyote hivyo vimezungumziwa. Kama inavyokubalika pia na wasioWaislamu, vibadala hivi kimsingi vimepunguzwa na kuwa mambo mawili yanayojumuisha pande mbili za kifikra, msisitizo ukiwekwa kwenye kukubali jambo mojawapo. Kwa upande mmoja, lilijitokeza kundi kubwa la watu lililofanya utafiti kuhusu Qur’an kwa kipindi cha mamia ya miaka na ambalo linadai, “Kitu kimoja tunakijua kwa uhakika kwamba mtu huyo, Muhammad, alikuwa na fikra kwamba yeye ni mtume. Yeye ni mwendawazimu!”

Wanashawishika kwamba Muhammad alilaghaiwa kwa namna fulani. Kisha kwa upande mwengine, kuna kundi jingine linalotoa madai kuwa, “Kwa sababu ya ushahidi huu, kitu kimoja tunakijua kwa uhakika kwamba, mtu huyo, Muhammad, alikuwa mwongo!”  Kwa kejeli, makundi haya mawili kamwe hayaonekani kuwa pamoja bila migongano na kupingana. Kwa kweli, rejea nyingi zinazozungumzia Uislamu kwa kawaida hutoa madai ya nadharia zote mbili. Huanza kwa kudai kwamba Muhammad (s.a.w.) alikuwa mwendawazimu na kisha kuishia kudai kuwa alikuwa mwongo. Kamwe hawaonekani kutambua kuwa asingeweza kuwa na sifa zote hizo mbili (yaani awe muongo na wakati huohuo awe mwendawazimu).

Kwa mfano, kama mtu amehadaiwa na akadhani kweli kuwa yeye ni mtume, basi hawezi tena kukaa usiku kucha akipanga, “Kesho nitawadanganyaje watu ili wafikiri kuwa mimi ni mtume?”  Anaamini kweli kwamba yeye ni mtume, na anategemea kuwa atapewa jibu kwa njia ya ufunuo. Kiukweli, sehemu kubwa ya Qur’an ilikuja kujibu maswali mbalimbali. Mtu alikuwa akimuuliza Muhammad (s.a.w.), na jibu lililetwa na ufunuo. Kwa hakika, kama mtu ni mwendawazimu na akaamini kuwa malaika humnong‟oneza neno sikioni mwake, na kisha mtu atapomuuliza swali fulani, yeye hufikiri kuwa malaika atampa jibu. Kwa sababu yeye ni mwendawazimu, kweli atafikiri hivyo. Hatomwambia mtu aliyemuuliza swali asubiri kidogo na kisha akakimbilia kwa rafiki zake na kuwauliza, “Je, kuna yeyote mwenye jibu la swali aliloulizwa?” Tabia hii ni sifa ya mtu asiyeamini kuwa yeye ni mtume. Kitu ambacho Wasiokuwa Waislamu wanakikataa kukikubali ni kwamba huwezi kuwa na sifa zote mbili. Mtu anaweza kuhadaiwa, au anaweza kuwa muongo. Ima anaweza akawa na sifa moja na asiwe na nyingine, lakini kwa hakika hawezi kuwa na sifa zote mbili! Msisitizo ulipo hapa ni kwamba, sifa hizo mbili haziwezi kupatikana kwa mtu kwa pamoja (yaani awe „mwendawazimu‟ na „muongo‟ kwa wakati mmoja). 

Mukhtasari ufuatao ni mfano mzuri wa aina ya duara ambalo siku zote wasio Waislamu huzunguka humo. Ukimuuliza mmoja wao: “Chanzo cha Qur’an ni kipi?” Atakwambia kwamba Qur’an ilitoka katika akili ya mtu aliyekuwa mwendawazimu. Ukimuuliza tena: “Kama ilitoka katika kichwa chake, taarifa zilizomo ndani ya kitabu hicho alizipata wapi? Kwa hakika Qur’an inaeleza vitu vingi ambavyo havikuwa vikijulikana kwa Waarabu”. Ili kuukabili ukweli ambao umempa, atabadilisha msimamo wake na kusema: “Sawa, huenda hakuwa mwendawazimu. Huenda kuna mtu fulani mgeni alimpa taarifa hizo. Hivyo, alificha jambo hilo na kusema uwongo kwa kuwaambia watu kuwa ati yeye alikuwa mtume”.

Hapo utatakiwa kumuuliza: “Kama Muhammad alikuwa mwongo, alipata wapi hali ya kujiamini (confidence)? Kwa nini alikuwa na tabia ya kana kwamba yeye ni mtume?

Mwishowe akiwa amefika kwenye kona, kama paka, utamuona haraka sana akitupilia mbali jawabu lake la mwanzo alilolitoa akilini mwake. Utamuona akidai, “Vyema, huenda hakuwa muongo. Labda alikuwa mwendawazimu na akaamini kuwa yeye ni mtume”. Na hapo ataanza kurejea mzunguuko wake kwenye duara lake kwa mara nyingine. 

Kama ilivyokwishaelezwa hapo awali, ndani ya Qur’an kuna taarifa na habari nyingi ambazo chanzo chake hakiwezi kuwa kingine zaidi ya Allah. Kwa mfano, nani aliyemwambia Muhammad kuhusu ukuta wa DhulQarnayn ulioko umbali wa mamia ya maili huko kaskazini? Nani aliyemwambia kuhusu embrolojia? Watu wanapokusanya mambo na ukweli kama huu, iwapo hawataki kuuhusisha na Mwenyezi Mungu, utawaona wanakimbilia kufikiri na kudhani kuwa kuna mtu aliyempa Muhammad taarifa hizi na kwamba alizitumia kuwahadaa watu. Hata hivyo, fikra hiyo yenye chuki na inda inaweza kubatilishwa kwa urahisi kwa swali moja jepesi:

“Kama Muhammad alikuwa muongo, aliipata wapi hali ya kujiamini (confidence)? Kwanini aliwaambia watu papo kwa papo yale ambayo watu wengine hawakuweza kuyasema?”

Hali kama hiyo ya kujiamini, moja kwa moja, inategemea uwe na uhakika usiokuwa na shaka kwamba kweli unapewa ufunuo na Mwenyezi Mungu. Kwa mfano: Mtume (s.a.w.) alikuwa na Ami yake aliyeitwa Abu Lahab. Mtu huyu alikuwa akiuchukia sana Uislamu kwa kiasi kwamba alikuwa akimfuata Muhammad popote alipokwenda kwa lengo la kuwafanya watu wasimuamini. Anapomuona Mtume (s.a.w.) akizungumza na mtu mgeni, husubiri mpaka wanapoagana na kisha yeye (Abu Lahab) huenda kwa mtu huyo na kumuuliza, “Alikwambia nini? Je, alikwambia rangi Nyeusi? Basi sio kweli, bali ni Nyeupe. Je, alisema Asubuhi? Sio hivyo, ni usiku”.

Alikuwa akisema kinyume kabisa na kile alichomsikia Muhammad (s.a.w.) na Waislamu wakikisema. Hata hivyo, miaka kumi kabla ya Abu Lahab kufariki dunia, Muhammad aliteremshiwa Sura moja ndogo. Sura hiyo ilisema wazi kuwa Abu Lahab ataenda Motoni (Jahannam). Kwa maneno mengine, ilithibitisha kwamba kamwe asingekuwa Mwislamu na hivyo angelaaniwa milele. Kwa kipindi chote hicho cha miaka kumi, Abu Lahab angetakiwa kusema...

“Nimesikia kwamba Muhammad amefunuliwa ya kwamba kamwe sintobadilika kwamba sintosilimu na nitaingia Jahannam. Sasa nataka kuwa Mwislamu. Mwasemaje?

Sasa mnaufikiriaje ufunuo wenu uliotoka kwa Mungu?” Lakini abadan hakufanya hivyo. Kwa kuwa alikuwa akifanya juhudi za kuupinga Uislamu ilitarajiwa kwamba angefanya hivyo (yaani angesilimu) ili afanikishe lengo lake la kuonyesha watu kuwa Uislamu hausemi ukweli. Kimsingi, Muhammad (s.a.w.) alimwambia: 
Je, wanichukia na wataka kunimaliza? Sema haya maneno (kwamba umeukubali Uislamu), utakuwa umenimaliza. Tamka maneno hayo!” 

Lakini Abu Lahab kamwe hakuyatamka. Miaka kumi! Na katika kipindi hicho chote hakuukubali Uislamu au hata kuwa na huruma juu ya dini ya Kiislamu. Kama kweli Muhammad hakuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwezaje kujua kwa uhakika kwamba Abu Lahab angeyafanya maneno ya Qur’an yathibitike kuwa ya kweli? Aliwezaje kujiamini sana kwa kiasi cha kumpa mtu miaka kumi ya kuyaadhiri madai yake ya utume? Jibu pekee
ni kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; kwani ili kuwasilisha changamoto kama hiyo mbele ya watu, mtu huyo anatakiwa awe na uhakika wa moja kwa moja, usiokuwa na shaka kwamba anapewa ufunuo na Mwenyezi Mungu.

          Mfano mwingine wa hali ya kujiamini aliyokuwa nayo Muhammad (s.a.w.) katika utume wake na kwa hiyo imani aliyokuwa nayo ya yeye na ujumbe wake kulindwa na Mwenyezi Mungu ni wakati wa kuhamia Madina pale alipoikimbia Makkah na kujificha pangoni pamoja na Abu Bakr. Kama kweli Muhammad (s.a.w.) angekuwa mrongo, mdanganyifu na mtu aliyejaribu kuwalaghai watu waamini kwamba ni mtume, katika mazingira hayo ya pangoni angetarajiwa kumwambia rafiki yake, “Eeh! Abu Bakr, tafuta sehemu ya kujificha humu pangoni”. Au “Chuchumaa katika ile kona na ukae kimya”. Lakini, hakika alichomwambia Abu Bakr kinaonesha wazi hali ya kujiamini aliyokuwa nayo. Alimwambia: “Tulia! Allah yu pamoja nasi, na Allah atatuokoa!” 
 Sasa basi, kama mtu anajua kwamba anawalaghai watu, aina hii ya msimamo anaitoa wapi? Kwa kweli, aina ya hali hii ya akili sio sifa ya mtu muongo au mdanganyifu hata kidogo. Hivyo, kama ilivyoelezwa hapo awali, wasio Waislamu wanazunguukazunguuka katika duara, wakitafuta njia ya kutokea njia ya kufafanua matokeo ya utafiti wa mambo yaliyomo ndani ya Qur’an bila kuyahusisha na chanzo chake halisi. Kwa upande mmoja, siku ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa watakwambia: “Mtu huyu alikuwa muongo”, na kwa upande mwingine, siku ya Jumanne, Alhamisi na Jumamosi watakwambia: “Alikuwa mwendawazimu”. Wanachokataa kukubali ni kwamba mtu hawezi kuwa na hali zote mbili wakati mmoja; lakini wanapenda tu kutumia hoja ya visingizio hivyo viwili kuelezea habari zilizomo ndani ya Qur’an.

Kiasi cha miaka saba iliyopita, nilitembelewa na mchungaji mmoja nyumbani kwangu. Katika chumba tulichokuwemo ilikuwepo Qur’an juu ya meza ikiwa imeelekea upande wa sakafuni, na hivyo mchungaji huyo hakuwa akijua kuwa kitabu hicho ni kitabu gani. Katikati ya maongezi yetu niliunyosha mkono wangu upande wa Qur’an na kusema: “Sina shaka na kitabu kile”. Akiiangalia Qur’an bila kujua kuwa ni kitabu gani, alijibu: “Ninakwambia, kama kitabu hicho sio Biblia, basi kiliandikwa na mwanadamu!” Katika kuyajibu maelezo yake hayo nikasema: “acha nikuelezee baadhi ya mambo yaliyomo ndani ya kitabu hiki”. Na ndani ya dakika tatu au nne nilimhadithia vitu vichache vilivyomo ndani ya Qur’an. Baada ya dakika hizo tatu au nne, alibadilisha kabisa msimamo wake na kusema: “Uko sahihi. Kitabu hiki hakikuandikwa na mwanadamu. Shetani ndiye aliyekiandika!” Kwa kweli, kushikilia msimamo kama huo ni kitu cha bahati mbaya sana kutokana na sababu nyingi. Kwanza, ni kisingizio cha harakaharaka na dhaifu sana. Ni mlango mwepesi wa kutokea kwenye hali isiyofurahisha. Kuna kisa mashuhuri katika Biblia kinachoelezea jinsi siku moja Wayahudi walishuhudia namna Yesu alivyomfufua mfu. Mtu huyo alikuwa amekufa siku nne kabla, na Yesu alipofika alisema: “Amka!” na mtu huyo akainuka na kutembea. Baadhi ya Wayahudi walioshuhudia tukio hilo walisema wakiwa hawaamini kilichotokea, Huyu ni shetani. Shetani ndiye aliyemsaidia!” Leo hii kisa hicho hukaririwa mara nyingi makanisani ulimwenguni kote, na watu hulia kwa uchungu wakisema: 

Oh, lau ningekuwepohapo, nisingekuwa mpumbavu kama Wayahudi!” Watu hawa wanastaajabisha, kwani hufanya kile kile kilichofanywa na Wayahudi. Pale unapowaonyesha sehemu ndogo tu ya Qur’an husema: “Oh, Shetani ndiye aliyetunga. Shetani ndiye aliyekiandika kitabu hicho!” Kwa kuwa wamebanwa kwenye kona na hawana jibu jingine lenye kujitosheleza, hukimbilia kwenye kisingizio cha harakaharaka na cha rahisi. Mfano mwingine wa watu wanaotumia msimamo huu dhaifu, unaweza kuonekana katika maelezo ya washirikina wa Makka kuhusu chanzo cha ujumbe wa Muhammad. Walikuwa wakisema: “Mashetani ndio wanaomletea Muhammad hiyo Qur’an!” Lakini kila yalipotolewa madai mapya, Qur’an hutoa jibu. Aya mojawapo yasema: 

“Na wanasema: Hakika yeye ni mtu aliyevamiwa (na shetani). Na hayakuwa haya (yaani Qur’an, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote” 
Qur’an 68: 5152

Kwa hivyo,  Qur’an inatoa hoja katika kujibu fikra na madai hayo. Kwa kweli, kuna hoja nyingi ndani ya Qur’an katika kujibu madai na tuhuma kwamba mashetani ndio waliomletea Muhammad (s.a.w.) ujumbe wake. Kwa mfano, katika Sura ya 26, Allah anasisitiza:
“Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo, Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi, Hakika hao wametengwa na kusikia”
Qur’an 26: 210212

Na sehemu nyingine ya Qur’an, Allah anatuelekeza: 

“Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni”. 
Qur’an: 16 : 98

Sasa je, hivi ndivyo Shetani anavyoandika kitabu? Anamwambia mtu kwamba: “Kabla ya kusoma kitabu changu, mwombe Mwenyezi Mungu akulinde dhidi yangu”? Hili ni gumu sana, tena sana. Mtu angeweza kuandika kitu kama hiki, lakini je sheteni angeweza kufanya hivi? Watu wengi wanaonesha wazi kuwa hawawezi kuafikiana katika mada hii. Kwa upande mmoja, wanadai kwamba Shetani asingeweza kufanya kitu kama hicho na hata kama angeweza, Mwenyezi Mungu asingemruhusu; lakini kwa upande mwengine, wanaamini pia kwamba Shetani ana uwezo kidogo ulio chini ya uwezo wa Mungu. Kimsingi wanadai kwamba yumkini Shetani akaweza kufanya kile kinachoweza kufanywa na Mungu. Na kutokana na msimamo wao huo, wanapoitazama Qur’an, hata wanaposhangazwa na jinsi ilivyo ya ajabu, huendelea kusisitiza, “Shetani ndiye aliyetengeneza!” Alhamdulillah, Waislamu hawana msimamo kama huo. Ingawa Shetani anaweza kuwa na uwezo fulani, lakini uwezo huo ni mdogo mno kuulinganisha na uwezo wa Mungu. Na hakuna Mwislamu awezaye kuwa Mwislamu kama hatoamini kwamba Shetani hana uwezo wowote kwa Mwenyezi Mungu. Inafafahamika kwa kila mtu hata kwa wasio Waislamu kwamba Shetani anaweza kufanya makosa kiurahisi kabisa, na ingetarajiwa kwamba angetoa taarifa zinazopingana na kuhitilafiana kama angeandika kitabu. Kwani Qur’an yasema:

“Je, hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi”
Qur’an 4: 82

Sambamba na visingizio vinavyotolewa na wasio Waislamu katika majaribio yao ya kipuuzi ya kuhalalisha maelezo ambayo hayapo ndani ya Qur’an, kuna shambulio jingine litolewalo mara kwa mara linaloonekana kuwa ni muunganiko wa fikra za kwamba Muhammad (s.a.w.) alikuwa mwendawazimu na muongo. Kimsingi, watu hawa wanadai kwamba Muhammad alikuwa na wazimu, na kutokana na maono yake ya uwongo, aliwadanganya na kuwapotosha watu. Kuna jina la kitu hiki katika saikolojia. Kinajulikana kama maithomania (mythomania). Humaanisha  kwamba mtu aseme uwongo na kisha yeye mwenyewe akauamini huo uwongo kuwa ni kweli. Hili ndilo wasemalo wasiokuwa Waislamu kuwa ndio lililokuwa likimsumbua Muhammad (s.a.w.). Lakini tatizo pekee la wazo hili ni kwamba mtu anayesumbuliwa na mythomonia hawezi kabisa kushughulika na mambo ya hakika na kweli, na lakini Qur’an yote mwanzo mpaka mwisho  imesimama kwenye misingi ya ukweli. Kila kilichomo ndani yake kinaweza kufanyiwa utafiti na kugunduliwa kuwa ni kweli. Kwa kuwa mambo ya kweli ni tatizo kwa mtu mwenye mythomania, basi mwanasaikolojia anapojaribu kumtibu mtu anayesumbuliwa na hali hiyo, huendelea kumkabili kwa mambo ya ukweli. Kwa mfano, kama mtu ni mgonjwa wa akili na akadai kuwa: “Mimi ndiye mfalme wa Uingereza”, mwanasaikolojia hamwambii “hapana, wewe siye. Wewe ni mwendawazimu!”. Hafanyi hivyo. Badala yake, humkabili kwa mambo ya hakika na kweli na kumwambia, “Sawa, wasema wewe ni mfalme wa Uingereza. Sasa niambie malkia yu wapi sasa. Na yu wapi waziri wako mkuu? Na walinzi wako wapo wapi?”. Sasa, mtu huyo anapokuwa na taabu ya kujaribu kujibu maswali haya, hujaribu kutoa visingizio mbalimbali, akisema, “Ah… malkia…amekwenda kwa mama yake. Ah… waziri mkuu …oh..amekufa”. Na hapo hapo huwa anapona kwa sababu hawezi kupambana na mambo ya uhakika na ukweli. Iwapo mwanasaikolojia huyo ataendelea kumkabili kwa mambo mengi ya hakika na ukweli, mwishowe huukubali ukweli na kusema, “Nahisi mimi sio mfalme wa Uingereza”. Qur’an Tukufu humkabili kila anayeisoma kwa katika njia sawa na ile ya mwanasaikolojia anayemtibu mgonjwa wa maradhi ya mythomania. Kuna aya moja ndani ya Qur’an isemayo: 

“Enyi watu! Yamekujieni mawaidha (yaani Qur’an) kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini.”
Qur’an 10: 57

Kwa mara ya kwanza, maelezo haya huonekana kuwa yasiyo wazi, lakini maana ya aya hii huwa wazi pale inapotazamwa kwa kutumia mfano uliotajwa hapo juu. Kimsingi, mtu huponywa dhidi ya maono yake ya uwongo kwa kuisoma Qur’an. Kimsingi, Qur’an ni tiba. Huwaponya kabisa watu wenye maono ya uwongo (waliohadaiwa) kwa kuwakabili kwa ukweli na mambo ya uhakika. Msimamo ulio mashuhuri ndani ya Qur’an ni ule usemao, “Enyi watu, mwasema hiki na kile kuhusu jambo hili; lakini vipi kuhusu hiki na hiki? Mwawezaje kusema hiki wakati mwajua kile?” na kuendelea. Qur’an humlazimisha mtu kutafakari jambo husika na wakati huohuo ikimtibu na kumponya dhidi ya maono ya uwongo aliyonayo kwamba mambo ya kweli yaliyoletwa na Mwenyezi Mungu kwa wanadamu yanaweza kutolewa visingizio kiurahisi kwa fikra, mawazo na visingizio hafifu.

Ni aina hii ya msimamo kuwakabili watu kwa ukweli  ambayo kwamba imeziteka fikra na macho ya watu wengi wasio Waislamu. Kwa hakika, kuna marejeo yanayovutia sana kuhusu mada hii ndani ya Ensaiklopidia Mpya ya Kanisa Katoliki.

Katika makala moja chini ya mada ya Qur’an, Kanisa Katoliki lasema: Kwa muda wa karne nyingi, zimetolewa fikra nyingi kuhusu chanzo cha Qur’an… Leo hii  hakuna mtu mwenye akili anayekubaliana na fikra yoyote katika fikra hizo! Sasa hili ni Kanisa kongwe la Kikatoliki, ambalo limekuwepo kwa karne nyingi, likikanusha majaribio haya ya kipuuzi yanayofanywa katika kuitolea visingizio Qur’an Tukufu. Kwa kweli Qur’an ni fumbo kwa Kanisa Katoliki. Linasema kwamba ni kitabu cha Mungu (ufunuo), hivyo wanaidurusu. Hakika wangependa kupata uthibitisho ambao sio, lakini haiwezekani. Hawawezi kupata kisingizio kinachojitosheleza. Lakini angalau wamekuwa waaminifu katika utafiti wao na hawayakubali maelezo ya mwanzo ambayo hayakuthibitishwa. Kanisa hilo linasema kuwa kwa kipindi cha karne kumi na nne hayajawasilishwa maelezo ya ufafanuzi wenye kukubalika kiakili. Angalau kanisa hilo linakiri kwamba Qur’an sio suala linaloweza kuachwa kiurahisi. Kwa kweli watu wengine hawaaminiki sana. Hudai kwa namna ya harakaharaka, “Oh, Qur’an ilitokea hapa. Qur’an ilitokea pale”. Na hawapimi hata uaminifu wa yale wayaelezayo muda wote. Hata hivyo, maelezo hayo ya Kanisa Katoliki humuacha Mkristo wa kawaida katika taabu. Huenda akawa na mawazo binafsi kuhusu chanzo cha Qur’an, lakini akiwa kama mfuasi mmoja wa Kanisa, hawezi kabisa kuifanyia kazi fikra yake binafsi. Kwani kwa kufanya hivyo aweza kwenda kinyume na utiifu, uaminifu na utii kwa kanisa. Kwa sababu ya kuwa mwanakanisa, anatakiwa kukubali kile kilichotangazwa na Kanisa Katoliki bila kuhoji na atekeleze mafundisho yake kama sehemu ya maisha yake ya kila siku. Hivyo, kimsingi, Kanisa katoliki kwa ujumla wake linasema: "Msizisikilize taarifa hizo zisizothibitishwa dhidi ya Qur’an", sasa kipi kinachoweza kusemwa kuhusu mtazamo wa Kiislamu? Hata wasio Waislamu wanakiri kwamba kuna kitu kwenye Qur’an  kinachotakiwa kutambuliwa  sasa kwanini watu wanakereheka, kuchukia na kuudhika sana pindi Waislamu wanapotoa mtazamo kama huo? Kwa hakika hiki ni kitu ambacho watu wenye akili wanatakiwa kukitaamali kitu ambacho watu wenye ufahamu na uelewa wanatakiwa kukitafakari.

Hivi karibuni, msomi mkubwa wa Kanisa Katoliki –aitwaye Hans  aliisoma Qur’an na kutoa maoni yake kuhusu alichosoma. Mtu huyu amekuwepo kwa muda fulani, na anaheshimika sana katika Kanisa, na baada ya kufanya uchunguzi kwa umakini, aliripoti matokeo ya utafiti wake, akihitimisha kwa kusema : “Mungu ameongea na mwanadamu kupitia kwa mtu, Muhammad”. 

Haya ni matokeo mengine ya utafiti uliofanywa na chanzo kisichokuwa cha Kiisalmu msomi mkubwa anayeheshimiwa na Kanisa Katoliki! Sidhani kuwa Papa anakubaliana naye, lakini hata hivyo, maoni ya mtu huyo mashuhuri, anayeheshimiwa na umma wa watu lazima yatakuwa yamebeba uzito mkubwa katika kutetea msimamo wa Waislamu. Anatakiwa kuungwa mkono kwa kuukubali ukweli kwamba Qur’an sio kitu kinachoweza kutupiliwa mbali kiurahisi, bali kwa hakika Mungu ndiye chanzo cha Maneno haya (yaani Qur’an). Kama inavyoonekana katika taarifa iliyopita, kila uwezekano umezungumzwa kwa undani, hivyo nafasi ya kutafuta uwezekano mwingine wa kuipuuza Qur’an haipo kabisa. Kwani kama kitabu hiki sio ufunuo wa Mungu, basi itakuwa ni udanganyifu; na kama ni udanganyifu, mtu lazima aulize, “Ni kipi chanzo chake?” na ni wapi Qur’an inapotudanganya?” 

Kwa kweli, majibu ya kweli ya maswali haya yatatoa mwanga juu ya usahihi na ukweli wa Qur’an na kuyanyamazisha madai yasiyothitishwa ya makafiri. Kiukweli, kama watu wataendelea kusisitiza kwamba Qur’an ni udanganyifu, basi watatakiwa kuleta ushahidi unaounga mkono madai yao. Mzigo wa kuthibitisha ni wa kwao, sio wetu! Kwani mtu hatakiwi kutoa fikra na nadharia fulani bila ushahidi wenye uthibitisho; hivyo ninawaambia hao watu: “Nionyesheni udanganyifu hata mmoja! Nionyesheni sehemu ambayo Qur’an inanidanganya! Nionyesheni, la sivyo, msiseme kwamba Qur’an ni udanganyifu!”. Sifa ya kuvutia iliyonayo Qur’an Tukufu ni namna inavyoshughulikia matukio ya kushangaza ambayo sio tu kwamba yanahusiana na zama za kale bali pia yanahusiana na wakati wa sasa. Kimsingi, Qur’an sio fumbo la zamani. Limeendelea kuwa fumbo hata sasa   ni fumbo kwa wasio Waislamu. Kwani kila siku, kila wiki, kila mwaka huleta ushahidi kwamba Qur’an ni nguvu ambayo watu wanapaswa kuitambua  yaani usahihi na ukweli wake hauhitaji tena kuhojiwa au kushindaniwa! Kwa mfano, aya moja ndani ya Qur’an Tukufu yasema:
”Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibandua? Na tukajaalia kutokana na maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?”
Qur’an 21: 30

Inashangaza kuona kuwa, taarifa hii ndiyo hasa iliyowafanya watoe tuzo ya Nobel kuwapa makafiri  mtu na mkewe  mwaka 1973. Qur’an inaeleza chanzo cha ulimwengu namna ilivyoanza kutoka kwenye kipande kimoja na mwanadamu ameendelea kuthibitisha ukweli wa ufunuo huu mpaka leo. Aidha, ukweli ni kwamba kusema uhai wote asili yake ni maji isingekuwa jambo rahisi kuwafanya watu wa karne kumi na nne zilizopita waliamini. Kwa kweli, kama miaka 1400 iliyopita ungesimama jangwani na kumwambia mtu kuwa , “Yote hii, unaona (ukijiashiria mwenyewe), kwa kiasi kikubwa inatokana na maji”, hakuna mtu ambaye angekuamini. Uthibitisho wa jambo hilo haukuwepo mpaka pale ilipovumbuliwa hadubini (microscope). Walilazimika kusubiri ili kuugundua huo uteseli (cytoplasm), sehemu ya kiini cha seli (cell), inayotengenezwa na 80% ya maji. Hata hivyo, ushahidi ulikuja, na kwa mara nyingine Qur’an ikafaulu majaribio na mitihani ya wakati huu.

Tukirudi kwenye vipimo vya kuthibitisha usahihi wa kitu (falsification tests) vilivyotajwa hapo awali, inavutia kufahamu kuwa, vipimo hivyo pia vinahusika na mambo ya zamani na ya wakati wa sasa. Baadhi yake yalitumika kuonyesha kudura (omnipotence) na Elimu ya Mwenyezi Mungu, wakati mengine yakiendelea kusimama kama changamoto  mpaka leo. Mfano wa hilo la kwanza ni maelezo yaliyotolewa na Qur’an kuhusu Abu Lahab. Maelezo hayo yanaonyesha wazi wazi kwamba Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa mambo ya siri, alijua kwamba Abu Lahab asingebadili msimamo wake na kuukubali Uislamu. Hivyo, Mwenyezi Mungu akatangaza kwamba (Abu Lahab) angelaaniwa milele mpaka atakapoingia katika moto wa Jahannam. Sura hiyo inaonyesha mambo yote mawili yaliyoelezwa hapo juu , yaani hekima ya Mwenyezi Mungu na kuwaonya wale waliokuwa kama Abu Lahab.

Mfano unaovutia wa aina ya pili ya kipimo cha kuthibitisha yaliyomo ndani ya Qur’an ni aya inayoelezea mahusiano baina ya Waislamu na Wayahudi. Aya hiyo imekuwa makini kutopunguza eneo lake kwa mahusiano tu ya mtu mmoja mmoja katika watu wa dini hizi mbili, badala yake inatoa mukhtasari wa mahusiano kati ya makundi hayo mawili ya watu kwa ujumla wao. Kimsingi, Qur’an Tukufu inaeleza kuwa siku zote Wakristo wataamiliana vizuri na Waislamu kuliko Wayahudi wanavyoamiliana na Waislamu. Kwa kweli, athari ya maelezo hayo inaweza kuonekana baada tu ya kutafakari kwa makini maana halisi ya aya hiyo. Ni kweli kwamba kuna Wakristo wengi na wayahudi wengi ambao wamekuwa Waislamu, lakini Jamii ya Kiyahudi kwa ujumla wake itaendelea kutazamwa na kuonekana kama adui mkubwa wa Uislamu. Aidha, ni watu wachache ndio wanaotambua kile kinachonadiwa na tangazo hilo la wazi la Qur’an. Kimsingi, ni fursa nyepesi kwa Wayahudi kuthibitisha kwamba Qur’an ni uwongo kwamba sio ufunuo wa Mungu. Wanachotakiwa kufanya ni wao kujikusanya, waamiliane vizuri na Waislamu na kisha waseme: “Sasa kitabu chenu kitukufu kinasemaje kuhusu yule ambaye ni rafiki yenu wa kweli ulimwenguni je, ni Wayahudi au Wakristo? Angalieni kile ambacho sisi Wayahudi tumekufanyieni!” Hayo tu ndiyo wanayotakiwa kuyafanya ili kukanusha usahihi na ukweli wa Qur’an, lakini hawajafanya hivyo kwa kipindi cha mika 1400. Na zaidi ya hapo, siku zote, changamoto hiyo bado ipo na nafasi ya wao kuthibitisha uwongo wa Qur’an bado ipo wazi!

Mifano yote iliyokwishatolewa kuhusu mitazamo mbalimbali ambayo mtu anaweza kuidurusu Qur’an bila shaka imekuwa mifano ya ndani (subjective) kwa asili; hata hivyo kuna mtazamo mwingine, miongoni mwa mifamo mingi, ambao ni wa nje (objective) na wenye msingi wa kimahesabu. Inashangaza sana jinsi Qur’an inavyokuwa ya ajabu na ya kweli pindi mtu anapolinganisha vitu vinavyoweza kutumika kama orodha ya makisio mazuri. Kimahesabu, inaweza kufafanuliwa kwa kutumia mifano ya kukisia (kubahatisha) na kutabiri. Kwa mfano, kama mtu ana machaguo mawili (yaani, chaguo moja sahihi na jingine lisilokuwa sahihi), na kwakuyafunga macho yake na akachagua, hivyo nusu ya atakavyochagua (yaani mara moja kati ya mara mbili) atapatia. Nafasi moja kati ya mbili angepatia katika kuchagua na angeweza kukosea katika kuchagua. Sasa, kama mtu huyo huyo ana nafasi mbili kama hiyo (yaani aweze kupatia au kukosea kuhusu hali namba moja, na akapatia au kukosea kuhusu hali namba pili), na akayafunga macho yake na kubahatisha, atakuwa sahihi katika moja ya nne ya muda husika (yaani mara moja katika mara nne). Sasa ana nafasi moja katika nne kwa sababu sasa kuna namna tatu za yeye kukosea na moja tu ya yeye kupatia. Kwa lugha nyepesi, anaweza kukosea katika hali namba moja na kisha anaweza kukosea tena katika hali  namba mbili; AU anaweza kukosea kuchagua katika hali namba moja na kupatia kuchagua katika hali namba mbili; AU anaweza kupatia katika hali namba moja na kisha akakosea katika hali namba mbili; AU anaweza kupatia katika hali namba moja na kupatia kuchagua katika hali namba mbili. Bila shaka, mfano pekee ambapo anaweza kupatia moja kwa moja ni katika eneo la mwisho ambapo anaweza kukisia kiusahihi katika hali zote mbili. Mategemeo ya makisio yake sahihi moja kwa moja yamekuwa makubwa kwa sababu idadi ya hali ya yeye kuweza kukisia imeongezeka; na mlinganyo wa kimahesabu unaowakilisha mpangilio huo ni 1/2x 1/2 (yaani, nafasi moja katika nafasi mbili kwa hali ya kwanza ikizidishwa kwa nafasi moja katika mbili za hali ya pili).

Tukiendelea na mfano huo, kama mtu huyo huyo atakuwa na hali tatu ambazo anatakiwa kubahatisha kabisa (blind guess), uwezo wake wa kupatia ni moja ya nane kwa muda wote (yaani mara moja katika nane au 1/2 x 1/2 x 1/2). Kwa mara nyingine mategemeo ya kufanya chaguo sahihi katika hali zote tatu yameongeza nafasi yake ya kupatia moja kwa moja na kuwa mara moja tu katika nane. Ieleweke kwamba idadi ya kubahatisha inapoongezeka, nafasi za kupatia  hupungua, kwani matukio hayo mawili yana uwiano unaoenda kinyume.

Sasa tukiuhusisha mfano huu na hali za ndani ya Qur’an, kama mtu akitengeneza orodha ya mada zote ambazo Qur’an imetolea maelezo yaliyothibitishwa kuwa sahihi, itabainika wazi kuwa haielekei kabisa kwamba yote yalikuwa ya kubahatisha tu (blind guesses). Kwa kweli, maudhui zilizozungumziwa ndani ya Qur’an Tukufu ni nyingi, na hivyo kama mategemeo (odds) ya mtu ni kupatia katika kuyabahatisha yote  kwa kweli kimatendo huwa ni sifuri. Kama kuna njia milioni moja za Qur’an kutokuwa sahihi, lakini Qur’an ikawa sahihi, basi haielekei kwamba kuna mtu aliyekuwa akibahatisha. Mifano mitatu ifuatayo ya mada ambazo kwamba  Qur’an imetoa maelezo yaliyo sahihi yote kwa pamoja inaonyesha jinsi Qur’an inavyoendelea kuyashinda makisio (odds).

Katika Sura ya 16 Qur’an yasema kwamba nyuki jike huyaacha makazi yao kwenda kukusanya chakula. Sasa, mtu aweza kubahatisha juu ya hilo, akisema, “Nyuki mnayemuona akirukaruka mahali mbalimbali anaweza kuwa nyuki dume, au inawezekana akawa nyuki jike. Nafikiri nitabahatisha kuwa ni jike”. Kwa hakika ana nafasi moja katika mbili ya kuwa sahihi. Hivyo, hutokea kwamba Qur’an ikawa sahihi. Lakini pia yaweza kutokea kwamba hicho sicho kilichokuwa kikiaminiwa na watu wakati Qur’an ilipoteremshwa. Waweza kueleza tofauti kati ya nyuki jike na nyuki dume? Sawa, inahitaji mtaalamu kufanya hivyo, lakini imegunduliwa kwamba nyuki dume kamwe hayaachi makazi yake kwenda kukusanya chakula. Hata hivyo, katika mchezo wa Shakespeare, Henry the Fourth, baadhi ya wahusika wanazungumzia nyuki na kutaja kwamba nyuki ni askari na wana mfalme. Hivyo ndivyo walivyofikiria watu katika zama za Shakespeare kwamba nyuki wanaoonekana kurukaruka mahali mbali mbali ni nyuki dume na kwamba wao hurudi nyumbani na kuwajibika kwa mfalme. Lakini, hiyo sio sahihi hata kidogo. Ukweli ni kwamba nyuki hao ni nyuki jike, na wanawajibika kwa malkia. Lakini ni katika kipindi cha miaka 300 tu iliyopita ambapo kwamba utafiti wa kisasa wa sayansi uliweza kugundua kuwa hii ndio hali halisi.

Hivyo, tukirudi kwenye orodha ya kubahatisha kwa usahihi (good guesses), kuhusu mada ya nyuki, Qur’an ilikuwa na nafasi ya 50/50 ya kuwa sahihi, na makisio (odds) yalikuwa moja kwa mbili.

Pamoja na maudhui ya nyuki, Qur’an pia yazungumzia jua na namna linavyosafiri katika anga (space). Kwa mara nyingine, mtu anaweza kubahatisha kwenye maudhui hiyo. Pindi jua linapotembea katika anga, kuna mambo mawili: linaweza kutembea kama jiwe
litembeavyo pale linapotupwa, au linaweza kutembea kwa hiari yake. Qur’an Tukufu inataja hiyo hali ya pili kwamba linatembea kutokana na mwendo wake lenyewe. Katika kufanya hivyo, Qur’an imetumia neno maalumu ”sabaha” kuelezea mwendo wa jua katika anga. Ili kumwelewesha vizuri msomaji kuhusu matumizi ya kitenzi hiki cha Kiarabu, tunatoa mfano ufuatao. Mtu awapo ndani ya maji na kitenzi hiki “sabaha” kikatumika katika kuelezea mwendo wake, hufahamika kuwa anaogelea, akisogea kwa hiari yake na sio kutokana na nguvu ya moja kwa moja inayotumika kwake. Hivyo kitenzi hiki kinapotumika kuelezea mwendo wa jua katika anga, hakimaanishi hata kidogo kwamba jua linaelea angani bila mpangilio kutokana na kutupwa au kitu kama hicho. Bali humaanisha tu kwamba jua linajigeuza na kuzunguka (turning and rotating) wakati likisafiri. Sasa, hili ndilo linalothibitishwa na Qur’an. Lakini je, kilikuwa kitu rahisi kugunduliwa? Je, mtu wa kawaida aweza kueleza kuwa jua linazunguka? Ni hivi karibuni tu ambapo kilitengenezwa kifaa cha kutoa na kudhihirisha picha ya jua ili mtu aweze kulitazama bila kuwa amefumba macho. Na kupitia mchakato huu iligunduliwa kuwa sio tu kwamba kuna vituo vitatu kwenye jua lakini vituo hivi husogea mara moja kila baada ya siku 25. Mwendo huu hujulikana kama mzunguko wa jua kwenye mhimili wake na kwa ujumla huthibitisha kwamba, kama Qur’an ilivyoeleza miaka 1400 iliyopita, kweli jua hujizungusha wakati wa kusafiri katika anga.

Na tukirudi kwa mara nyingine kwenye mada ya kubahatisha vizuri (good guesses), mategemeo (odds) ya kupatia kuhusu mada zote mbili mada ya jinsia ya nyuki na mwendo wa jua ni moja katika nne! 

Tukitazama nyuma karne kumi na nne zilizopita yumkini watu hawakuwa wakijua sana kuhusu kanda zinazogawa masaa (time zones), maelezo ya Qur’an kuhusu maudhui hii ni ya kushangaza sana. Fikra ya kwamba familia moja inakula kifungua kinywa wakati jua linapoinuka wakati familia nyingine inafurahia hali ya hewa ya usiku mwanana (brisk night air) kwa hakika ni kitu cha maajabu, hata katika zama za sasa. Kwa kweli, karne kumi na nne zilizopita, mtu asingeweza kusafiri zaidi ya maili thelathini kwa siku moja, na hivyo ilimchukua miezi mingi kutoka India mpaka Morocco, kwa mfano. Na yumkini, wakati akila chakula cha jioni Morocco, alikuwa akijifikiria, “Wakati huu huko nyumbani India wanakula chakula cha jioni pia”. Hii inatokana na kwamba hakutambua kwamba, katika harakati za safari yake, alipitia kwenye ukanda unaogawa masaa (time zone).  Lakini, kwa kuwa ni maneno ya Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa yote, Qur’an Tukufu inalijua na kulitambua tukio hilo. Katika aya moja inayovutia sana inaeleza kwamba historia itakapofikia kikomo na ikawadia Siku ya Hukumu, yote yatatokea mara moja; na tukio hili la mara moja litawakuta baadhi ya watu wakiwa katika wakati wa mchana na wengine wakiwa katika wakati wa usiku. Hii inaonyesha waziwazi Hekima na Elimu ya Mwenyezi Mungu isiyokuwa na mwanzo wala mwisho juu ya uwepo wa kanda za masaa (time zones), japokuwa uvumbuzi huu haukuwepo kabla ya karne kumi na nne zilizopita. Kwa hakika, kitu hiki sio kitu kinachoweza kuonekana na macho ya mtu au kwa uzoefu wa mtu, na jambo hili la hakika, ni ushahidi na uthibitisho tosha wa ukweli na usahihi wa Qur’an.

Tukirudi kwa mara ya mwisho kwenye mada ya bahati nzuri (kupatia katika kuchagua) kwa ajili ya mfano uliopo, mategemeo (odds) kwamba mtu alipatia katika kubahatisha kwenye mada zote tatu zilizotangulia jinsia ya nyuki, kutembea kwa jua na uwepo wa ukanda wa masaa  mategemeo hayo ya kubahatisha kwa usahihi ni moja katika nane!

Kwa kweli, mtu anaweza kuendelea zaidi na mfano huu, akiorodhesha orodha ndefu na kubwa ya mambo ya bahati nzuri; na bila shaka, mategemeo ya kukosa (odds) yatakuwa makubwa zaidi na zaidi kwa kila ongezeko la mada ambayo anaweza kuibahatisha. Lakini hakuna awezaye kukanusha yafuatayo; mategemeo kwamba Muhammad ambaye hakuwahi kusoma wala kuandika, alipatia katika kubahatisha na kukisia kuhusu maelfu na maelfu ya maudhui na mada, bila kufanya hata kosa moja, ni jambo gumu sana. Na kwamba mawazo ya kusema yeye ndiye aliyeandika Qur’an ni ya kutupiliwa mbali kabisa yatupiliwe mbali hata na maadui wakubwa wa Uislamu!

Kwa hakika, Qur’an inatarajia aina hii ya changamoto. Bila shaka, iwapo mtu anapoingia katika ardhi ya kigeni akamwambia mtu fulani kwamba, “Ninamjua baba yako. Nimekutana naye”, bila shaka huyo mwenyeji atatilia shaka maneno ya mgeni na kusema, “Umefika hapa sasa hivi. Ulimjuaje baba yangu”. Na hivyo atamuuliza, “Niambie, je baba yangu ni mrefu, mfupi, mweusi, mweupe? Ni upi muonekano wake?” Na hapo kama mgeni ataendelea kuyajibu maswali yote kwa usahihi, mtu yule mwenye shaka hatokuwa na chaguo jingine zaidi ya kusema, “Ninahisi wamfahamu baba yangu. Sijui umemfahamu vipi, lakini naamini unamfahamu!”. Hali ni hiyo hiyo kwa Qur’an. Inaeleza kwamba inatoka kwa Yule aliyeumba kila kitu. Hivyo kila mtu ana haki ya kusema, “Nithibitishie! Kama kweli mwenye kitabu hiki ndiye aliyeumba uhai na kila kitu katika mbingu na ardhi, basi atakuwa anajua kuhusu hiki, kuhusu kile, na kadhalika”. Na kwa hali hiyo, baada ya kuidurusu na kuitafiti Qur’an, kila mtu atapata kugundua ukweli kama huo. Aidha, sote tunafahamu kwa uhakika kwamba: Hatuwajibiki sisi wote kuwa wataalamu ili kuthibitisha yale yanayothibitishwa na Qur’an Tukufu. Imani ya mtu hustawi pale anapoendelea kuchunguza na kuuthibitisha ukweli uliomo ndani ya Qur’an. Na mtu anatakiwa kuendelea kufanya hivyo katika maisha yake yote.

Mwenyezi Mungu amuongoze kila anayeukurubia ukweli


NYONGEZA
Mhandisi mmoja katika Chuo Kikuu cha Toronto (Canada) aliyekuwa akishughulika na masuala ya Saikolojia na ambaye alikuwa amesoma mambo mengi kuhusu mada hiyo na kuifanyia utafiti aliandika kitabu juu ya Ufanisi wa Kujadiliana katika Makundi. Lengo la utafiti wake ilikuwa kutafuta namna watu wanavyoweza kufanikiwa zaidi wanapojikusanya
na kujadiliana katika makundi ya watu wawili wawili, watatu, kumi, n.k. Matokeo ya utafiti wake yalionesha kuwa: Watu hufanikiwa zaidi wanapozungumza katika makundi ya watu wawili wawili. Ugunduzi huu wote ulikuwa kinyume na matarajio yake, bali ni ushauri uliotolewa na Qur’an tangu zamani.

Aidha, Sura ya 89 ya Qur’an inautaja mji fulani uitwao „Iram (mji wa maguzo), ambao haukuwa ukijulikana katika historia ya zamani na haukuwepo kwa kiasi cha kuwashughulisha wanahistoria. Hata hivyo, katika mwezi wa Desemba 1978 idara ya Taifa ya Mambo ya Kijiografia ilitoa taarifa za kuvutia zilizoeleza kwamba mwaka 1973, mji wa Elba ulikuwa umegunduliwa nchini Syria. Mji huo uligundulika kuwa na umri wa karne 43, lakini hili sio lilokuwa la kushangaza zaidi. Watafiti walikuta katika maktaba ya mji wa Elba orodha ya miji yote iliyokuwa ikifanya biashara na mji wa Elba. Amini usiamini, katika orodha hiyo lilikuwepo jina la mji wa „Iram. Watu wa Elba walikuwa wakifanya biashara na watu wa „Iram! 

“Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu  ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawiliwawili na mmojammoja; kisha mfikiri.....” 

Katika kuhitimisha ninawaomba mtafakari kwa umakini haya yafuatayo: 

“Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao amini”
Qur’an 29:50


3 comments:

 1. KUAMINI MAKADIRIO YA MWENYEZI MUNGU

  Hakuna raha wala utulivu kwa mja katika dunia hii isipokuwa ni kule kuamini kwake mapitisho ya Mwenyezi Mngu na makadirio Yake. Nako ni kuamini kuwa chochote.swahiliminbar.com

  ReplyDelete
 2. It's very important to read the Quran, and if you learn Quran with tajweed, it's much better for you. Tajweed means improvement and this term refers to the improvement of the Quran reading process. You have to read according to rules if you want to improve your recitation. The rules will help you learn the right Arabic letter pronunciation.For children and adults we offer the best online tajweed courses. Kids can also know tajweed, so they can quickly memorize the rules — the best way to become an online reciter. We provide the best learning platform for young people and adults.

  ReplyDelete
 3. It's very important to read the Quran, and if you learn Quran with tajweed, it's much better for you. Tajweed means improvement and this term refers to the improvement of the Quran reading process. You have to read according to rules if you want to improve your recitation. The rules will help you learn the right Arabic letter pronunciation.For children and adults we offer the best online tajweed courses. Kids can also know tajweed, so they can quickly memorize the rules — the best way to become an online reciter. We provide the best learning platform for young people and adults.
  https://alhamdislamictutor.com/course/nazira-tul-quran

  ReplyDelete

Qur'an 5:32