Thursday 8 March 2012

Maelezo ya Qur'an Na Ukuaji Wa Mimba.


Mwenyezi Mungu Amesema: 
“Mna nini hamweki heshima ya Mwenyezi Mungu? Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja?” Suratul Nuh 13-14

Kisayansi Ilitambua vipi Jambo Hili:
Mtu wa kwanza kumsoma mtoto wa kuku kwa kutumia lensi ndogo ni Harvey katika mwaka 1651. Pia alidurusu vijusi vya mbawala. Kutokana na ugumu wa kuainisha siku za kwanza za uja uzito, akajua kuwa mtoto si chengine isipokuwa ni takataka za mfuko wa uzazi. Katika mwaka 1672, Graaf akagundua kokwa ndogo ndogo katika mayai ya uzazi ambazo hadi leo zinaitwa kwa jina lake “Graafian Follicles” na akakuta vijiwe vidogo katika tumbo la uzazi la sungura vyenye kufanana na kokwa ndogo ndogo. Akajua kuwa mtoto sio takataka za tumbo la uzazi lakini anatokana na mayai ya uzazi. Muundo huo wa ndani kabisa alioujua Graaf si chengine isipokuwa ni vitundu vidogo katika koja la seli za awali za mtoto (Blastocysts).

Katika mwaka 1675,  Malpighi alikuta kijusi katika yai la kuku akadhani kuwa halihitaji vitu vya kurutubisha toka kwa jogoo. Akadhania kuwa ni lenye kiumbe kidogo chenye kukua na wala hakiumbiki katika maumbo tofauti. Kwa kutumia darubini iliyoendelea zaidi, Hamm na Leeuwenhoek, waligundua mbegu za manii ya binaadamu  kwa mara ya kwanza katika historia mwaka 1677, lakini hawakuelewa ni ipi kazi yake hasa katika uzazi. Pia walidhani kuwa yana binaadamu mdogo anayekua katika tumbo la uzazi  bila ya maumbo maalum ya uumbaji. Katika mwaka 1759, Wolff alikisia kuwa ukuaji wa mtoto unatokana na koja la awali la uumbaji lisilo na umbo la kiumbe kilichokamilika. Katika mwaka 1775, ulimalizika mjadala kuhusu dhana ya uumbaji uliokamilika na ukafikiwa ukweli wa uumbaji katika maumbo.

Majaribio ya Spallanzani kwa mbwa, yakathibitisha umuhimu wa mbegu za manii katika zoezi la uumbaji. Kabla ya hapo, ilitanda fikra ya kuwa mbegu zamanii ni viumbe vya ajabu vinavyoishi kwa kutegemea viumbe vyengine, kwa hiyo wamepewa jina la wanyama wa manii (Semen Animals). Katika mwaka 1827, baada ya kupita miaka 150 ya ugunduzi wa mbegu za manii,  Von Baer alikuta viyai vidogo katika vijiwe vya ovari ya mbwa mmoja.

Katika mwaka  1839, Schleiden na Schwann walithibitisha kuwa uumbikaji wa mwili wa binadamu unatokana na sehemu hai muhimu za uumbaji na matokeo yake, na sehemu hizo zikaitwa Seli . Baadae ikawa ni wepesi kufahamu ukweli wa uumbikaji wa binadamu katika maumbo, kuanzia seli iliyorutubishwa inayotokana na muungano wa manii na ovari.

Hamm na Leeuwenhoek walikuwa wanasayansi wa kwanza kuchunguza chembe hai za manii ya mwanaadamu (spermatozoa) mnamo mwaka 1977, kwa kutumia darubini iliyofanyiwa mabadiliko (zaidi ya miaka 1,000 baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)). Kimakosa, walidhani kuwa chembe hai ya manii ilikuwa na mwanaadamu mdogo sana aliyefanyika kabisa, ambaye alikua baada ya kuwekwa katika eneo la viungo vya uzazi vya mwanamke.

Maelezo Ya Qur'an Juu Ya Ukuaji Wa Kiinitete Cha Mwanaadamu

Ndani ya Qur'an Tukufu, Mwenyezi Mungu Anaeleza hatua za ukuaji wa kiinitete cha mwanaadamu:
“Na kwa yakini Tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo. Kisha Tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti. Kisha Tukaiumba tone kuwa ‘Alaqah (ruba, kitu chenye kusubirishwa, na tone la damu), na Tukaiumba ‘Alaqah kuwa Mudhwghah (kitu kilichotafunwa, yaani pande la nyama)…”
Qur'an 23:12-14)

Kwa uhakika, neno la Kiarabu, ‘Alaqah lina maana tatu:
  1. Ruba
  2. Kitu chenye kusubirishwa, na
  3. Tone la damu
Katika kulinganisha ruba na kiinitete katika hatua ya ‘alaqah, tunaona kuna mlingano baina ya viwili hivi, kama tunavyoweza kuona katika umbo namba 1. Pia, kiinitete katika hatua hii hupata chakula kutoka katika damu ya mama yake, sawa sawa na ruba, ambaye hujipatia chakula chake kutoka katika damu ya wengine.


Umbo na. 1: Michoro yenye kufafanua ulinganifu wa muonekano kati ya ruba na kiinitete cha mwanaadamu katika hatua ya ‘alaqah. (Mchoro wa ruba kutoka katika kitabu Human Development as Described in the Qur'an and Sunnah, Moore na wengine, uk. 37, uliobadilishwa kidogo kutoka katika IntegratedPrinciples of Zoology, Hickman na wengine. Mchoro wa kiinitete kutoka katika Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 73.)

Maana ya pili ya neno ‘alaqah ni “kitu chenye kusubirishwa.” Hicho ndicho tunachoweza kukiona katika maumbo namba 2 na 3, kusubirishwa kwa kiinitete kikiwa katika hatua ya ‘alaqah, tumboni mwa mama.

Umbo na. 2: Katika mchoro tunaweza kuona kusubirishwa kwa kiinitete kikiwa katika hatua ya ‘alaqah tumbo la uzazi (mji wa mimba) la mama. (The Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 66.)


Umbo na 3: Katika Fotomaikrograf (Photomicrograph) hii, tunaweza kuona kusubirishwa kwa kiinitete (alama 8) wakati wa hatua ya ‘alaqah (kadiri ya umri wa siku 15) katika tumbo la uzazi la mama. Kipimo khalisi cha kiinitete ni kadiri ya milimita 0.6. (The Developing Human, Moore, 3rd ed., uk. 66, Kutoka katika Histology, Leeson and Leeson.)

Maana ya tatu ya neno ‘alaqah ni “tone la damu.” Tunakuta kwamba muonekano wa sehemu ya nje ya kiinitete na kifuko chake katika hatua ya ‘alaqah unashabihiana na ulewa tone la damu. Hii ni kutokana na kuwepo kwa kiasi kikubwa cha damu iliyomo ndani ya kiinitete wakati wa hatua hii (angalia umbo na. 4). Kadhalika, katika hatua hii, damu iliyo ndani ya kiinitete haizunguki mpaka mwishoni mwa wiki ya tatu.

Hivyo, katika hatua hii, kiinitete ni kama tone la damu.

Umbo na. 4: Mchoro wa muundo wa kiasili wa mshipa wa damu wa moyo ndani kiinitete katika hatua ya ‘alaqah. Muonekano wa nje wa kiinitete na kifuko chake unalandana na ule wa tone la damu kutokana na kuwepo kwa kiasi kingi cha damu kiuwiano ndani ya kiinitete. (The Developing Human, Moore, 5th ed. p.65)

Hivyo, maana tatu za neno ‘alaqah linaendana sawia na maelezo juu ya kiinitete katika hatua ya ‘alaqah. Baada ya hapo, Ayah imetaja kuwa inafuata hatua ya Mudhwghah. Maana ya neno la Kiarabu, Mudhwghah, ni “kitu kilichotafunwa.” Ikiwa mtu atatafuna kipande cha ubani mdomoni mwake kisha akakilinganisha na kiinitete kilicho katika hatua ya Mudhwghah, tunaweza kupata jibu kuwa kiinitete katika hatua ya Mudhwghah kinalandana kimandhari na kitu kilichotafunwa. Hii ni kwa sababu ya somiti (somites) nyuma ya kiinitete ambayo "kwa namna fulani inafanana na alama za meno katika kitu kilichotafunwa." (angalia umbo namba 5 na 6)

Umbo namba. 5: Picha ya kiinitete chenye umri wa siku-28 katika hatua ya Mudhwghah. Katika hatua hii, kiinitete kinafanana na kitu kilichotafunwa, kwa sababu somiti (somites) zilizo nyuma ya kiinitete, kwa namna fulani zinalandana na alama za meno katika kitu kilichotafunwa. Urefu khalisi wa kiinitete ni milimita 4. (The Developing Human, Moore and Persaud, 5th ed., uk. 82, kutoka kwa Profesa Hideo Nishimura, Kyoto University, Kyotro, Japan.)

Umbo namba 6: Ukilinganishwa muonekano wa kiinitete katika hatua ya Mudghah na kipande cha ubani kilichotafunwa, tutakuta mfanano baina ya viwilio hivyo.
  • A: Mchoro wa kiinitete katika hatua ya Mudhwghah. Hapa tunaweza kuona somiti (somites) nyuma ya kiinitete ambazo zinaonekana kama alama za meno (The Developing Human, Moore and Persaud, 5th ed., uk. 79)
  • B: Picha ya kipande cha ubani uliotafunwa.
Ingewezekana vipi kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuyajua yote haya mnamo karne kumi na nne zilizopita, ilhali wanasayansi wameyagundua hivi karibuni tu, tena kwa kutumia vifaa vya vya kisasa na darubini zenye nguvu , ambavyo vyote havikuwepo katika zama hizo?

Profesa Keith L. Moore ni mmojawapo wa wanasayansi mashuhuri wenye kuheshimika katika uwanja wa anatomia (sayansi inayohusu mwili na viungo vyake jinsi vilivyo) na embriolojia (taaluma ya maisha ya kiinitete), tena ni mwandishi wa kitabu kilichoitwa The Developing Human ambacho kimetafsiriwa katika lugha nane. Kitabu hiki ni kazi ya rejea ya kisayansi na kilichaguliwa na kamati maalumu katika nchi ya Marekani kuwa ni kitabu bora kilichotungwa na mtu mmoja. Dk. Keith Moore ni Profesa wa heshima (baada ya kustaafu) wa anatomia na Biolojia ya Chembe Hai katika Chuo Kikuu cha Toronto, huko Toronto, Kanada. Hapo alikuwa Mkuu Mshiriki wa Sayansi ya Msingi (Basic Sciences) katika Kitivo cha Sayansi ya Tiba na kwa miaka 8 alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Anatomia. Mwaka 1984 alipokea tuzo ya aina yake kabisa iliyotolewa katika fani ya anatomia nchini Kanada, iliyoitwa Tuzo ya J.C.B. Grant kutoka Chama cha Wana-Anatomia wa Kanada. Ameongeza vyama vingi vya kimataifa, kama vile Chama cha Wana-Anatomia wa Kanada na Marekani na Baraza la Muungano wa Sayansi za ki-Biolojia.

Mnamo mwaka 1981, wakati wa Mkutano wa Saba wa Masuala ya Madawa jijini Dammaam, Saudi Arabia, Profesa Moore alisema: “Imekuwa ni furaha kubwa kwangu kusaidia ufafanuzi wa kauli zilizo katika Qur-aan kuhusu ukuaji wa mwanaadamu. Ni dhahiri kwangu kuwa kauli hizi ni lazima zitakuwa zimetoka kwa Mwenyezi Mungu na kumfikia Muhammad kwani elimu hii yote haikugunduliwa mpaka baada ya karne nyingi baadaye. Hili linanidhihirishia kuwa ni hakika kwamba Muhammad ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.” 

Matokeo yake, Profesa Moore aliulizwa swali hili: “Je, Hii inamaanisha kuwa unaamini kwamba Qur'an ni neno la Mwenyezi Mungu?” Akajibu: “Sioni ugumu wa kukubali hivyo.”

No comments:

Post a Comment

Qur'an 5:32