Kuhusu Tovuti


Assalamu Alaikum Wa Rahmatu Allah Wa Barakatuh

Katika tovuti hii, nakusudia kukumbushana utukufu wa Mwenyezi Mungu (swt). Utukufu ambao ameuonesha kwetu sisi, kupitia vitu mbali mbali, tunavyo viona na tusivyo viona. Kuanzia vijidudu vidogo vidogo tunavyoviona, mpaka madubwana makubwa kabisa yaliyoko katika makundi ya nyota (Garaxy) na sayari zilizo kubwa kabisa kuliko jua letu hili.

Qur’an ni maneno halisi ya Mwenyezi Mungu, ambayo aliyashusha kwa Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kupitia Malaika Jibrill.

Qur’an ambayo ilihifadhiwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye akawasomea Qur’an hiyo wafuasi wake. Nao, kwa zamu, waliihifadhi, kuiandika, na kuipitia pamoja na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Zaidi ya hayo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliipitia Qur’an pamoja na Malaika Gibril (Gabriel) kila mwaka mara moja na katika mwaka wa mwisho wa uhai wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), waliipitia mara mbil.

Tangu wakati iliposhushwa. Qur’ani, mpaka leo hii, daima kumekuwepo na idadi kubwa nno ya Waislam ambao wamehifadhi Qur,an yote, neno kwa neno. Baadhi yao wameweza kuhifadhi nzima wakiwa na umri wa miaka kumi. Hakuna hata herufi moja ya Qur’an iliyo badilishwa ingawa karne nyingi zimepita.

Qur’an, iliyoshushwa karne kumi na nne zilizopita, imeelezea mambo ya hakika ambayo yamevumbuliwa au kuthibitishwa na wanasayansi hivi karibuni tu. Hii bila ya shaka inathibitisha kuwa Qur’an ni lazima itakuwa ni maneno halisi ya Mungu, yaliyofunuliwa naye kwenda kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa hiyo Qur’an haikutungwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au na mtu yeyote. Hii pia inathibitisha kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mtume wa kweli alietumwa na Mwenyezi Mungu.

Haingii akilini kuwa mtu yeyote wa miaka elfu moja na mia nne iliyopita aliyeishi jangwani angelijua hakika hizi zilizogunduliwa au kuthibitishwa hivi karibuni tu kwa kutumia nyenzo na njia za kisayansi za kisasa...!

Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma na Mwingi wa Ukarimu ambaye ni m’bora katika kuumba na kutengeneza anasema katika Qur’an kuwa;

Akika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi na kukhitilafiana kwa usiku na mchana ….”na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni …na akaeneza umo kila aina ya wanyama….na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, Bila shaka zipo ishara kwa watu wanaozingatia.
Qur'an  2:164

Aya hii ina mazingatio makubwa kabisa kama itafanyiwa kazi. Kwani baina ya mbingu na ardhi kuna vitu vingi sana ambavyo wanasayansi wa leo wanavigundua kuwa vipo na vina faida kubwa kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine kwa ujumla.

Na bado Mwenyezi Mungu (swt) anatubainishia zaidi katika Qur’an 45:13 kuwa 

Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, vyote vimetoka kwake. Akika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao fikiri. 
Qur'an 45: 13         

Je ni vitu gani hivyo ambavyo vimewekwa kututumikia vilivyomo mbinguni na ardhini? Basi na tuwe wenye subra kubwa na wenye tafakuri za kina tunaposoma kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt) yaani Qur’an tukufu ili tupate mazingatio ni nini Allah (swt) amekusudia, kutufahamisha waja wake. Basi yaliyoko katika tovuti hii ni baadhi ya maajabu machache tu kati ya chungu ya miujiza yaliyomo ndani ya Qur’an tukufu.

Basi In-sha-Allah katika kuperuzi tovuti hii ndogo, Mwenyezi Mungu (swt), atujaalie iwe ni chachu ya kumcha Allah (swt) katika kiwango kile kinacho takiwa mja awe nacho. In-sha-Allah.
Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha?
Limetukuka jina la Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na ukarimu
Qur'an 55: 77-78

Nakaribisha michango ya hali na mali, mawazo yenu ndio mafanikio ya site hii...
 
Rejea za Qur’an:
Tafadhali, tambua kwamba blog hii inatumia tafsiri tu ya maana ya Qur'an kwa Kiswaili ya Sheykh Ali Muhsin Al-Barwani. Qur'an yenyewe ipo katika lugha ya Kiarabu na unaweza kuipata kwenye mitandao mbalimbali kwenye tovuti.

No comments:

Post a Comment

Qur'an 5:32