Katika maisha ya
wanaadamu wote, kutoka wakati wa ujana na utoto hadi wakati wanapofariki,
ishara za Mwenyezi Mungu mmoja peke Yake wa kweli zinaonyeshwa kwao katika
maeneo yote ya ardhi, hata katika nafsi zao mpaka ibainike kwao kuwa yupo
Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
Mwenyezi Mungu Anasema katika Qur’ani:
“Tutawaonyesha Ishara Zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao
wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako
Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?”
Q 41: 53
Q 41: 53
Hapa tunatoa mfano jinsi Mwenyezi Mungu
Anavyompatia ishara mtu mmoja kwa upotevu kwa kuabudu masanamu. Katika eneo la
kusini mashariki mwa msitu wa Amazon huko Brazil, Amerika Kusini, kabila la
asili lisiostaarabika lilijenga kibanda kipya ili kumpatia makazi sanamu-mtu,
Skwatch, likiwakilisha mungu mkubwa kabisa wa uumbaji wote.
Siku ya pili kijana mmoja aliingia katika kibanda
hicho ili kutoa heshima zake kwa mungu. Alipokuwa katika hali ya kusujudu kwa
jinsi alivyofundishwa kuwa hilo sanamu ni muumba na mlezi wake, na mwenye
kuruzuku, mara aliingia mbwa mzee, hafifu na mwenye upele na aliyejawa na
viroboto kwenye kibanda hicho. Kijana huyo alinyanyua uso wake kwa wakati
muafaka, wakati tu wakumuona mbwa huyo akinyanyua mguu wake wa nyuma na
kulikojolea sanamu hilo.
Kijana alimfukuza mbwa huyo katika hekalu kwa
ghadhabu kubwa mno; lakini hasira na ghadhabu ilipofifia alitambua kuwa sanamu
hawezi kuwa mola wake mlezi wa ulimwengu mzima. Mwenyezi Mungu ni lazima awe
kila pahala, alihitimisha. Ajabu kama inavyoonekana, mbwa kulikojolea sanamu
ilikuwa ni ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kijana huyo. Ishara hii ilikuwa
na risala ya Mwenyezi Mungu kuwa anachokiabudu ni cha uwongo. Tukio hili
lilimuacha huru kijana huyo na utumwa wa kufuata ada alizofundishwa za kuabudu
mungu wa uwongo. Matokeo yake ni kuwa huyu kijana alichaguzishwa: ama kutafuta
mungu wa kweli au kuendelea katika upotevu wa njia zake.
Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatutajia
kiu aliyokuwa nayo Nabii Ibraahim (‘Alayhis Salaam) katika juhudi ya
kumtafuta Mwenyezi Mungu kama mfano wa wale wenye kufuata ishara Zake
jinsi wanavyoongoka (na hivyo kufuata njia nyoofu na ya sawa). Allah (Subhaanahu
wa Ta'ala) Anasema:
“Na kadhaalika Tulimwonyesha
Ibraahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini. Na
ulipomuingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu. Ilipotua
akasema: Siwapendi wanaotua. Alipouona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye
Mola Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu
hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu waliopotea. Na alipoliona jua linachomoza akasema:
Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipotua, alisema: Enyi
watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayofanyia ushirikina. Hakika mimi
nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si
miongoni mwa washirikina” Q 6: 75 – 79
Kama ilivyotajwa hapo awali, Manabii
walitumwa kwa kila taifa na kabila kuunga mkono itikadi ya kimaumbile ya
mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu na mwelekeo wa silica aliozaliwa nao mwanadamu wa
kumuabudu Yeye, vile vile kutilia nguvu ukweli wa kutoka kwa mungu.
Kwa ishara za kila siku
zilizodhihirishwa na Mwenyezi Mungu. Japokuwa mafunzo mengi ya Manabii hawa
yaligeuzwa, sehemu zinazoonyesha vifungu zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu
zimebaki bila ya waa na zimewatumikia wanaadamu kuwaongoza katika kuchagua baina
ya ukweli na uwongo, na haki na batili. Ushawishi wa risala zilizofunuliwa na
Mwenyezi Mungu kupitia kwa zama zote zinaweza kuonekana katika “Amri Kumi”
za Uyahudi katika Taurati ambazo baadaye zilichukuliwa na kuingizwa katika
mafunzo ya Ukristo. Vile vile kuwepo kwa kanuni dhidi ya mauaji, wizi na uzinzi
katika jamii nyingi sana kote duniani, katika zama za kale na sasa.
Matokeo kwa ishara za Mwenyezi Mungu
kwa wanaadamu kupitia kwa zama zote zikichang’anywa na wahyi Wake kupitia kwa
Manabii Wake, wanaadamu wote wamepatiwa fursa ya kumtambua Mwenyezi Mungu mmoja
tu wa kweli.
Kwa hiyo, kila nafsi itahesabiwa kwa
itikadi yake kwa Mwenyezi Mungu na kukubali kwake kwa Dini ya kweli ya Mwenyezi
Mungu, Uislamu, ambayo ina maana ya kunyenyekea na kutii amri za Allah (Subhaanahu
wa Ta'ala).
No comments:
Post a Comment