Sunday 27 October 2013

Hoja za wakanao kuwepo Mwenyezi Mungu

Makafiri wanadai kuwa suala la imani juu ya Mungu Muumba (Mwenyezi Mungu (s.w.) ni suala la kibubusa (la kufuata mkumbo pasina hoja yoyote). Comforth, ni miongoni mwa wanachuoni wa kilahidi wanaokataa wazi wazi kuwepo kwa Mwenyezi Mungu (s.w.), na ameandika, katika kitabu chake, The Dialectical Materialism uk.21 kwamba:

"Conception of supernatural spiritual being seem to have their justification not of course in any evidence of the senses (but)......"

"..... Fikra juu ya Mungu Muumba kwa ujumla haina ushahidi wowote unaotokana na milango ya fahamu (lakini)....."

Sababu i zilizowapelekea makafiri wa kale na wa leo kudai kuwa hapana Mola Muumba ni hizi zifuatazo: 
  1. Mwenyezi Mungu hayupo kwa sababu haonekani wala hadirikiki kwa milango ya fahamu. 
  2. Mwenyezi Mungu amefanywa kuwepo na mwanaadamu kutokana na fikra finyu na uduni wa maendeleo ya sayansi na teknologia. 
  3. Hapana Muumba bali vitu vyote vimetokana na maada iliyopitiwa na mabadiliko ya kidogo kidogo. 
  4. Kama Muumba yupo ni ipi nasaba yake au alitokeaje. 
Wakati wa Nabii Musa Makafiri walidai kumuona Mwenyezi Mungu kama inavyobainika katika aya zifuatazo: 
"Na walisema (makafiri wa Kiquraish kumuambia Muhammad (s.a.w.)." Hatuwezi kukuamini mpaka utububujishie chemchem katika ardhi (hii ya Makka) au... utuletee Mwenyezi Mungu (na malaika uso kwa uso." 

Makafiri wa zama hizi, kama akina Cornforth, wanadai kuwa: 
"..... Fikra juu ya Mungu Muumba kwa ujumla haina ushahidi wowote unaotokana na milango ya fahamu....."1

Udhaifu wa Hoja hii ya makafiri uko wazi kama ifuatavyo: 

i) Milango ya fahamu ina udhaifu na mipaka finyu kiasi kwamba si lazima ujuzi unaopata kupitia milango ya fahamu, kila mara uwe wa kweli. Kwa mfano mtu anapokuwa mbali na kitu anachokitazama, huonekana kidogo kuliko umbile lake halisi na kila kinapozidi kuwa mbali hupungua umbile lake machoni na hatimaye kutoweka kabisa machoni. Tukiendelea na mfano huu wa mlango wa kuona, utaona kuwa kitu tunachokiangalia kikiwa kidogo sana hatuwezi kukiona. Kwa mfano vijidudu (virusi) mbali mbali vinavyotusumbua katika miili yetu, hatuvioni kwa macho ya kawaida ila mpaka tutumie darubini (microscope). Hali kadhalika milango ya fahamu wakati mwingine hudanganya, yaani huleta picha isiyo ya kweli isiyolingana na hali halisi. Ili kuthibitisha hili hebu turejee mifano miwili ifuatayo: 

Mfano wa Kwanza

Ni muiko wa mwanga (Refraction of light) Muiko wa mwanga hufanya vitu vilivyo majini vionekane vikubwa kuliko umbile lake halisi na vionekanae kuwa karibu zaidi kuliko kina halisi.

Mfano wa Pili

Ni ule wa mazigazi (mirage). Wakati wa jua kali katika barabara iliyonyooka, kwa mbali panaonekana kama kuna bwawa la maji, lakini ukikaribia pale huyakuti maji.

Udhaifu huu haupatikanai kwenye mlango wa kuona tu bali ukichunguza utaona kila milango wa fahamu una udhaifu. Kwa mfano masikio yetu yana mipaka. Hayawezi kunasa mawimbi yote ya sauti yaliyomo angani mpaka tuwe na nyenzo za kunasia sauti hizo kama vile Radio, T.V. n.k. Baadhi ya wanyama hasa wanyama pori wanauwezo zaidi wa kusikia sauti zetu zikiwa mbali kuliko sisi. Pua zetu zinauwezo mdogo sana wa kutambua harufu ya kila kitu. Mbwa anatuzidi sana katika kutambua harufu.

Kutokana na udhaifu huu wa milango ya fahamu, si busara kudai kuwa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) hayupo kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kumdiriki kwa milango ya fahamu kama vile kuona, kusikia, kunusa, kwa sababu kuna vitu chungu nzima tusivyoweza kuiviona, kuvisikia, kuvinusa, kuvionja au kuvigusa (kuvihisi) na bado tunakiri kuwepo kwavyo kwa ushahidi mbali mbali.

Ni vema tufahamu kuwa milango ya fahamu, sio njia pekee ya kufahamia mambo. Wakati mwingine tunafahamu mambo mbali mbali kwa kutumia mantiq, uzoefu na majaribio.

Je, tutakataa kuwa dunia ni Mviringo na inazunguka kwa kuwa hatuioni na hatuhisi mzunguko wake?

Je, tutakataa kuwepo kwa hewa ya aina ya "Oxygen" kwa kuwa hatuwezi kuiona, kuinusa, kuionja au kuigusa?  

No comments:

Post a Comment

Qur'an 5:32