Thursday, 7 March 2013

Familia YA Mzee Imran (Surat Al I'mran)


Na Kabuga Kanyegeri
Ni asubuhi nyingine baada ya kumaliza kuswali swala ya alfajiri, ninakumbuka maneno ya mwalimu wangu, Sheikh Yaaqub Abdu Ningi. Mwalimu huyu kutoka mjini Lagos, Nigeria kabla ya kuanza kutufundisha somo lake la theolojia alikuwa akituuliza kama siku hiyo tumesoma aya ngapi za Qur’an Tukufu. Alikuwa akitueleza kuwa huwezi kutafakari sawa sawa kama huna utaratibu wa kuisoma Qur’an Tukufu. Aingawa wakati huo alikuwa ameishi Tanzania kwa zaidi ya miaka 7 lakini alikuwa hajaweza kuikamata vizuri lugha ya Kiswahili. Nadhani hiyo ilitokana na kuathiriwa na lugha nyingi alizokuwa akiziongea kama vile Kihausa, Kiingereza, Kiarabu na Kirusi, kwani hata darasani alikuwa hatumii Kiswahili. Kuna mambo mengi sana ninayoweza kumzungumzia mwalimu huyu, lakini muhimu ni miongoni mwa watu walionijengea utamaduni wa kuisoma Qur’an kwa taamuli na tafakuri. Alikuwa akitutaka tusome angalau aya 50 kwa siku. Alhamdulillah niliweza kurithi utamaduni wa kusoma angalau aya hizo kwa siku.

Sasa wiki iliyopita, nilipomaliza kuswali swala ya alfajiri nilifungua surah ya Al-Imran. Pamoja na kukutana na aya nyingi zilizoniachia maswali mengi katika tafakuri, nilivutiwa na aya ya 33 na nyingine kama saba zilizofuata, ambazo hasa ndizo nitakazozizungumzia katika kisa changu huki cha familia yam zee wetu, Mzee Imran. Tafakuri yangu ilijikita katika kuitafiti aya hii kwa undani zaidi.

Ni muhimu nieleze kuwa mpaka sasa bado ninazitafakari, hivyo nitakuwa nikielezea kile ambacho nimekitafakari. Na katika post hii ya kwanza nitaelezea utangulizi juu ya mafunzo yanayopatikana katika tafakuri kama hizi kabla ya kuzama ndani kabisa ya aya hizi.
Aya niliyoanza kuitafakari ni hii ifuatayo:
Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuuhu na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.” Qur’an Surat Al I'mran 3: 33)

Kwanini Huwa Ninayatafakati Maandiko Kama Haya?


Ndugu zangu, kwanza kabisa hatuna budi kufahamu kuwa maisha ni njia na mwanadamu ni msafiri. Mwanadamu anahitaji sana muongozo na maelekezo wakati anaposafiri katika njia hii. Ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndio huo muongozo. Bila kuwepo kwa muongozo huu, wanadamu wanaweza kupotea katika bahari hii isiyo na mwisho na yenye hatari. Muumba aliyemuumba mwanadamu ndiye anayeujua udhaifu na sifa za mwandamu huyo. Muumba mwenye uwezo wa kuumba viumbe wenye maajabu kama mwanadamu halafu akawa hajawajali atakuwa mpuuzi. Qur’an inauliza swali hili:
Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?” (Surat Al-Mulk 67: 14)

Kwa kuwa anawajua viumbe Wake, vivyo hivyo anazijua sifa na udhaifu wa viumbe Wake. Amewawekea viumbe hao miundombinu inayowafaa misingi ya maisha yao. Mwenyezi Mungu amefundisha kuhusu msingi huo kwa ufunuo Wake kupitia kwa mitume. Ufunuo wa Qur’an ndio kinara wa ufunuo wote wa kabla yake, ambao unabeba tunu zisizobadilika za ufunuo wote, na Mtume Muhammad (s.a.w) ndio kizingo cha mwisho cha mnyororo huu wa mitume.

Ufunuo au wahyi ndio mradi wa ujenzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mpokeaji wa ujenzi huu ni mwanadamu. Hii ni kwa sababu mwanadamu ndiye mas-uli (responsible) wa kujenga maisha yanayoendana na malengo ya kuumbwa na kuletwa kwake ardhini.

Lengo la ufunuo katika Qur’an ni kumjenga mwanadamu. Qur’an Tukufu hufanikisha ujenzi wake kwa kutumia nyenzo mbalimbali. Qur’an hujenga taswira ya kila mpokeaji kwa kutumia ramani yake ya fikra. Huzielezea kwa usahihi fikra ambazo tunajengea maisha yetu, kama vile uzuri na ubaya, haki na batili, hakika na kutokuwa hakika, uadilifu na dhulma, kusatawi na kuanguka, kusonga mbele na kurudi nyuma, stahmala na kunyauka, kupata na kukosa, ushindi na kushindwa. Aliyemuwekea mwanadamu maana ya fikra hizi atakuwa Yule aliyemuumba. Kama ufunuo ukiasisi mawazo haya na mwanadamu akayatumia kwa mapana yake, basi Mwenyezi Mungu atayaongeza maarifa na hekma ya mtu huyo. Qur’an huijenga akili ya mpokeaji kwa kutumia mawazo yake. Akili inayofanya kazi vizuri itajengwa juu ya fikra ambayo baadaye itajengwa na tafsiri sahihi ya dhana mbalimbali. Ili maelezo ya “Hili ni zuri....Hili ni baya,” yapate kuwa mawazo sahihi, dhana za “zuri” na “baya” lazima zipate tafsiri sahihi. Wazo ambalo limepata tafsiri sahihi ni zana ya ujenzi wa akili ya mpokeaji.

Qur’an huijenga tabia ya yule anayeipokea kupitia mifano mbalimbali. Huelezea yale mambo mazuri kama vielelezo vya mifano inayotakiwa kuigwa na kuelezea yale mabaya kama onyo na mazingatio ambayo watu wanatakiwa kujifunza. Inamfundisha asili na tabia ya mapambano baina ya haki na batili. Visa vyake vyote vinaakisi kwenye vipengele vyote vya maisha. Ifuatayo ni baadhi ya mifano:

Kisa cha Adamu (a.s) na Ibilisi kimetajwa katika maeneo sabini ndani ya Qur’an Tukufu, kila eneo linawekea mkazo nukta tofauti kuhusu athari na matokeo ya kutenda dhambi. Adamu (a.s) na Ibilisi, wote walitenda kosa. Lakini Adamu (a.s) aliomba toba kwa kosa lake na kusamehewa; Ibilisi aliitetea dhambi yake na kufukuzwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kisa cha mafuriko mkubwa ya zama za Nabii Nuuh (a.s) ni kisa cha mwanadamu aliyetengenza safina kwenye eneo la bara lisilokuwa na hata tone moja la maji kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Alipewa ujumbe ufuatao: “Fanya kile ulichoamrishwa na itakapofika siku ambayo bahari itahitajika, basi Mola aliyeiumba bahari ataileta mbele ya miguu yako.” Kisa hicho kinaonesha kwamba kila palipo na uhalifu na ukiukwaji wa sheria, ni kawaida kwa sehemu hiyo kufikwa na gharika, hivyo tunapswa tujitahidi kuwa kisiwa cha matendo mazuri katikati ya bahari ya madhambi. Mafuriko ni msiba kwa wasiokuwa waumini na ni fursa kwa waumini.

Kisa cha Nabii Ibrahimu (a.s) kinaelezea ulinzi wa Mwenyezi Mungu na kwamba hakuna moto kama wa Namrudh unaoweza kuiunguza na kuichoma imani kama ya Nabii Ibrahimu (a.s). Kisa cha Ibrahimu kumchinja mwanaye ni kisa kinachoelezea utayari wa mtu kukikabili kifo. Kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja kuna maana ya kupokea kitu kikubwa zaidi kuliko kile kilichotolewa. Kama ukimtoa dhabihu mwanao mpendwa Ismail (a.s) kwa ajili tu ya Mwenyezi Mungu, basi sio tu kwamba Mwenyezi Mungu atakurejeshea mwanao huyo bali pia atakuongezea mtoto mwingine, yaani Is-haq (a.s).

Na kisa cha Nabii Yusufu (a.s) kinatoa ujumbe ufuatao: “Usidharau kile kinachoweza kufanywa na mtu mmoja.” Mtu mmoja mwema, mwaminifu, mwenye maarifa, hekima na ujuzi anaweza kubadilisha mustakbali wa jamii nzima. Aidha, ikumbuke hekima ya kuangalia kwa makini nguo yako imechanika sehemu gani?

Kisa cha Nabii Musa (a.s) kinatoa ujumbe kwamba kila Firauni amewekewa Musa wake. Kinasema kuwa pindi Firauni dhalimu anapofika katika tumbo la mama, subiri kumuona Musa katika kasri la Firauni.

Mwenyezi Mungu Mtukufu hamteui mtu bila utaratibu kwa ajili ya jambo analolikusudia. Uteuzi huu unaofanywa na Mwenyezi Mungu sio jambo la siri analolijua Yeye pekee, bali kuna maelezo kwa kila uteuzi anaoufanya, ndani ya kanuni ijulikanayo kama chanzo (cause) na matokeo (effect).
Uhusiano uliopo baina ya chanzo na matokeo yake ni uti wa mgongo wa kanuni hii ya jumla kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ujumbe unaoelezwa katika aya hii hapa unatakiwa kueleweka ndani ya muktadha wa uhusiano baina ya chanzo na matokeo na unatakiwa kutafakariwa na wale wenye moyo unaotafakari kwa dhikri, taaamuli na uchambuzi, mambo ambayo humpeleka mtu kwenye kuhoji mambo.

Matokeo yatokanayo na vitendo hivi vya kuhoji yanatakiwa kutolewa kama masuluhisho ya matatizo yanayoibuka katika zama zetu hizi. Ni pale tutakapofanya hivyo ndipo tutakapoweza kujilinganisha na mashujaa wema waliotajwa katika aya mbalimbali za Qur’an. Tusipofanya hivyo, basi hiyo itakuwa na maana kwamba tunavichukulia vitabu Vitukufu kama maandiko mfu. Ikiwa hivyo, vitabu vitukufu navyo vitawaona kuwa ni wafu wale ambao wamekataa kuutambua ujumbe mtukufu wa kuumbwa kwao na kuwaadhibu kwa kutumia mienendo yao ya kuzitilia shaka nafsi zao wenyewe.

Hakuna mtu anayepaswa kusahau kwamba, Qur’an Tukufu itaendelea kuziweka wazi hekma zake “kwa wale watakaozisoma kwa umakini mkubwa aya zake.” Ni watu wachache tu ndio watakaoweza kuutambua ukweli huu, kwa sababu Qur’an Tukufu ni ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu maandiko yake yalifunuliwa mara moja tu, lakini maana yake imefunuliwa mara nyingi.

1 comment:

  1. Alhudulilah kwa maelezo yako naomba namba zako ibrahim

    ReplyDelete

Qur'an 5:32